Loading...

Chama cha wafanyakazi wa sekta ya huduma za mtandao na mawasiliano Tanzania (Tewuta), waishtaki menejimenti ya TTCL Rais Magufuli.


Rais Dr John Pombe Magufuli.

Dar es Salaam. Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao na Mawasiliano Tanzania (Tewuta), wameishtaki menejimenti ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa Rais John Magufuli na kumuomba aizue kuwaadhibu wafanyakazi wake wanaoanika majipu yanayohitaji kutumbuliwa ndani ya kampuni hiyo.

Pia, chama hicho kimepinga kauli ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kutaka kuinyang’anya TTCL usimamizi wa mkongo wa taifa wa mawasiliano kwa madai kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuweka rehani ulinzi na usalama wa nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Junus Ndaro alisema yeye na mwenyekiti wake, Pius Mkuke ni waajiriwa wa kampuni hiyo na kwamba baada ya kuanza kuanika uozo unaofanyika TTCL, ajira zao ziko shakani.

“Sisi na wafanyakazi wengine tunaohisiwa kutoa taarifa zinazohusisha utendaji mbovu wa menejimenti tunaambuliwa kupewa barua za kujieleza kwanini tusifukuzwe kazi,” alisema na kuongeza: “Menejimenti imedhamiria kuwaadabisha viongozi wa Tewuta, kuwafukuza kazi wafanyakazi ambao hawako tayari kuficha maovu ndani ya kampuni, hilo limeanza Novemba mwaka jana.”

Alisema walichukua uamuzi huo baada ya kuona kasi ya Rais Magufuli ya kutumbua majibu na kumtaka kuanza na kampuni hiyo ambayo utendaji wake unasuasua. 

“Ndani ya TTCL kuna muundo mbovu wa uendeshaji na utendaji usioendana na biashara ya soko la mawasiliano, ukosefu wa muundo wa utumishi unaozingatia usawa katika ajira na ukosefu wa muundo wa mishahara ili kuondoa matabaka na mgawanyo wa wafanyakazi,” alisema.

Alisema kampuni hiyo ili ipate ufanisi lazima iwe na menejimenti inayochapa kazi na kufuata misingi na miiko ya uongozi.

Alibainisha kuwa lengo la Tewuta na wafanyakazi wote wa TTCL ni kuona kampuni hiyo ikipata mafaniko na kufanya kazi kibiashara ili kushindana na kampuni binafsi za simu nchini. 

“Ndani ya kampuni kuna ombwe la uongozi ambao hauendani na kasi ya ushindani katika biashara ya mawasiliano. Uongozi uliopo umeshindwa kuongoza, kusimamia, kuleta ufanisi, utulivu na tija ndani ya kampuni,” alisema Ndaro.

Kwa upande wake, Mkuke alisema: “Chama cha wafanyakazi kazi yake ni kuisimamia menejimenti itekeleze majukumu yake. Wapo waliopewa barua ya onyo na kuitwa kujadiliwa ili kutimuliwa kazi.”

Alisema baada ya kuibua suala la wafanyakazi kuonywa kwa kueleza uozo wa kampuni hiyo, menejimenti ya TTCL ikaliweka kiporo suala hilo.

Kuhusu usimamizi wa mkongo huo, alisema kauli kuwa TTCL imeshindwa kuuhudumia kikamilifu na kufikisha huduma za mawasiliano vijijini, haina mashiko. “Iwapo mkongo utaondolewa mikononi mwa kampuni na kupewa kampuni binafsi ama wakala wa kuusimamia utakuwa uamuzi wa kukurupuka na kuiadabisha TTCL,” alisema.

Chama hicho kimemuomba Rais Magufuli kutoa idhini kwa taasisi za umma kutumia huduma zinazotolewa na Shirika la Posta Tanzania na TTCL. Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemus Mushi alisema hawezi kuzungumzia kwa kuwa hajayaona licha ya madai kutolewa kila mara.




ZeroDegree.
Chama cha wafanyakazi wa sekta ya huduma za mtandao na mawasiliano Tanzania (Tewuta), waishtaki menejimenti ya TTCL Rais Magufuli. Chama cha wafanyakazi wa sekta ya huduma za mtandao na mawasiliano Tanzania (Tewuta), waishtaki menejimenti ya TTCL Rais Magufuli. Reviewed by Zero Degree on 2/22/2016 11:23:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.