Loading...

Jiji latangaza ‘smart area’, na kutoa rai kwa wananchi kujiandaa kushirikiana na mamlaka zao katika utekelezaji wa mpango huo.


Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam limepanga kutumia Sh500 milioni kutekeleza mpango wa kuboresha huduma za usafi wa mazingira katika eneo maalumu litakalojulikana kama ‘smart area’.

Akizungumzia mpango huo, Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano wa Umma wa halmashauri hiyo, Gaston Makwembe alisema mpango huo utakaosimamiwa na mkurugenzi wa jiji na kuratibiwa na katibu tawala mkoa utahusisha maeneo ya makutano ya barabara za Uhuru hadi Morocco, barabara ya Ali Hassani Mwinyi eneo la Morocco hadi Daraja la Selanda kuelekea fukwe za Ocean Road.

Pia, utahusisha maeneo ya Kivukoni, Bandari hadi makutano ya Barabara ya Kilwa na Mandela na vilevile Barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara hadi makutano ya Barabara ya Kawawa na Uhuru pamoja na maeneo yote ya kitalii na fukwe.

Vilevile mpango huo utahusu njia kuu ya mapokezi ya wageni katika Barabara ya Nyerere kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Barabara ya Mwai Kibaki hadi Hoteli ya Whitesands kupitia Barabara ya Mbezi chini na Morogoro pamoja na barabara zote za mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi (Dart).

Makwembe alisema mpango huo utakapoanza biashara zisizo rasmi kama bodaboda, maguta na mikokoteni havitaruhusiwa katika maeneo hayo.

“Pia majengo chakavu na mabovu hayatahitajika, utupaji taka katika maeneo yasiyo rasmi utadhibitiwa kwa kufuata sheria, ombaomba, wamachinga na wanaopanga bidhaa zao nje ya maduka na wanaowasha moto na kupika katika maeneo yasiyo rasmi hawataruhusiwa,”alisema.

Shughuli nyingine ambazo hazitakiwi kuendelea katika maeneo hayo ni gereji bubu, uegeshaji ovyo wa magari, kujisaidia, kutema mate na uwapo wa mabango yaliyochakaa.

Pia, alisema kubandika matangazo bila kibali maalumu, kuunganisha mfumo wa majitaka kwenye mifereji ya mvua, uoshaji magari katika maeneo hayo havitaruhusiwa.

“Kusababisha kelele na muziki wa sauti ya juu bila kibali, kuingiza malori ya tani zaidi ya 10 ni baadhi ya mambo yaliyo katika shughuli zitakazopigwa marufuku katika maeneo hayo,” alisema.

Mkuu wa idara ya Udhibiti wa Jiji, Membe Membe alisema wananchi wanapaswa kujijengea utaratibu wa kutunza mazingira sambamba na utupaji taka katika maeneo yaliyoainishwa.

“Tunawaomba makandarasi walio na tenda za usafi kuhakikisha wana vifaa vya kutosha, ili maeneo hayo yawe safi kama ilivyopangwa na jiji,” alisema.

“Tunatoa rai kwa wananchi kujiandaa kushirikiana na mamlaka zao katika utekelezaji wa mpango huo na maeneo ambayo hayajatajwa yataendelea kusimamiwa na mamlaka husika kwa mujibu wa sheria na wananchi washirikiane nazo ili kuboresha usafi katika maeneo yao,” alisema.



ZeroDegree.
Jiji latangaza ‘smart area’, na kutoa rai kwa wananchi kujiandaa kushirikiana na mamlaka zao katika utekelezaji wa mpango huo. Jiji latangaza ‘smart area’, na  kutoa rai kwa wananchi kujiandaa kushirikiana na mamlaka zao katika utekelezaji wa mpango huo. Reviewed by Zero Degree on 2/06/2016 12:03:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.