Magufuli: Ole wao wawekezaji waliotelekeza mashamba na viwanda.
Rais John Magufuli
Morogoro. Rais John Magufuli amewataka wale wote waliotelekeza mashamba na viwanda walivyouziwa na Serikali, kuhakikisha wanavifufua mapema iwezekanavyo, kabla ya kunyang’anywa na kupewa wanaoweza kuviendesha.
Akizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika eneo la Msamvu wakati akisafiri kwa gari kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, alisema Mkoa wa Morogoro ulikuwa na viwanda vingi na mashamba mengi makubwa ambayo kama waliouziwa wangeyaendeleza, yangezalisha ajira.
“Kama nilivyowaahidi wakati wa kampeni na leo narudia, wote walioamua kutumia mashamba na viwanda walivyouziwa na Serikali kwa ajili ya kuchukulia mikopo kwenye mabenki badala ya kufanya uzalishaji wavifufue haraka, vinginevyo tutawanyang’anya” alisisitiza Rais Magufuli huku akishangiliwa na wananchi.
Rais Magufuli pia alisimamishwa na kuwasalimu wananchi wa Wami Dakawa, Magole na Dumila ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa atatekeleza ahadi yake ya kuwapa mashamba atakayonyang’anya kutoka kwa walioyatelekeza, amewataka kuachana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji na badala yake watatue migogoro hiyo kwa kutumia njia za kisheria.
Aidha, amewataka viongozi wote wa mkoa hadi vitongoji kushirikiana kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kabla haijasababisha madhara akionya kuwa migogoro hiyo ikileta madhara itakuwa ni kigezo tosha kuwa viongozi hao wameshindwa kutekeleza wajibu wao na wanapaswa kuachia ngazi.
Amewahimiza wananchi hao kuchapa kazi kwa juhudi hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinanyesha, akisema wahakikishe kuwa watoto wote wanaopaswa kuandikishwa shule wanapelekwa, hasa baada ya Serikali kuamua kutoa elimu bure ya kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
“Tumeamua kutoa elimu bure na tutatoa elimu bure na jambo hili limeonyesha mafanikio makubwa kwa kuwa hata shule zilizotarajia kuandikisha wanafunzi 45 zimejikuta zikiandikisha hadi wanafunzi 600 kwa darasa moja,” alisema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amekagua kipande cha barabara Kuu ya Morogoro - Dodoma kilichoharibiwa na maji ya mvua katika eneo la Kibaigwa mkoani Dodoma na kujionea kazi za ukarabati zinazofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).
Alimwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuongeza makandarasi wa kukarabati eneo hilo ili kazi ikamilike haraka badala ya kusubiri miezi miwili iliyopangwa na wizara.
Leo, Rais Magufuli atashiriki maadhimisho ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika katika Uwanja wa Namfua, Singida.
Credits: Mwananchi Communications
ZeroDegree.
Magufuli: Ole wao wawekezaji waliotelekeza mashamba na viwanda.
Reviewed by Zero Degree
on
2/06/2016 11:46:00 AM
Rating: