Loading...

Mbowe atangaza baraza la mawaziri vivuli, wajue wanaounda baraza hilo hapa.


Dodoma. Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe ametangaza baraza kivuli lenye mawaziri 19 na naibu mawaziri 29, huku Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akiteuliwa kwa mara ya pili kuwa mnadhimu wa kambi hiyo. 

Mawaziri hao vivuli wanatoka katika vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Vyama hivyo vilitia saini ya makubaliano ya ushirikiano mwaka 2014, wakati wa Bunge la Katiba na tangu wakati huo vimekuwa vikiunda kambi hiyo.

Mbowe alisema idadi ya wizara hizo inafanana na ya wizara za Serikali ya Awamu ya Tano ambazo zipo 19.

Mbali na kutangazwa kwa majina hayo, Bunge lilifanya uchaguzi wa wajumbe wa kuliwakilisha kwenye taasisi mbalimbali za kibunge.

Wajumbe hao ni wa Tume ya Utumishi wa Bunge, Bunge la Afrika (PAP), Jukwaa la Wabunge wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-PF), Kamati ya Utendaji wa Bunge la Jumuiya ya Madola (CPA) na Umoja wa Wabunge Duniani (IPU).

Katika baraza kivuli, Mbowe pia amemteua Hamad Juma Omari kuwa Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni na Ally Saleh Ally kuwa Naibu Mnadhimu.

Akitangaza majina hayo bungeni jana mchana, Mbowe alisema waziri kivuli wa Nchi, Ofisi ya Rais –Tamisemi ni Jaffary Michael na naibu wake ni Joseph Makundi (wote Chadema).

“Waziri Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ni Ruth Mollel (Chadema). Ally Salehe Ally (CUF) anakuwa waziri kivuli wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, makamu wake ni Pauline Gekul (Chadema).

“Fedha na Mipango waziri kivuli ni Halima Mdee na naibu wake ni David Silinde (wote Chadema). Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, ni Ester Bulaya (Chadema) na manaibu wake ni Yusuph Kaiza Makame na Maftah Abdallah Gachuma (wote CUF),” alisema.

Alisema Waziri Kivuli wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ni James Mbatia (NCCR-Mageuzi), na naibu wake ni Willy Quambalo, huku John Mnyika akiteuliwa kwa mara ya pili kuwa waziri kivuli wa Nishati na Madini akisaidiwa na John Heche (wote Chadema).

Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ambaye alikuwa waziri kivuli wa Maliasili na Utalii katika baraza kivuli lililopita, amehamishiwa wizara ya Mambo ya Nje. Naibu wake ni Riziki Mngwali (CUF).

“Wizara ya Ulinzi itaongozwa na Juma Hamad Omar (CUF) na naibu wake ni Mwita Waitara (Chadema) na wizara ya Mambo ya Ndani waziri kivuli ni Godbless Lema na naibu wake ni Masoud Abdallah Salim (CUF),” alisema Mbowe.

Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare ameteuliwa kuwa waziri kivuli Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na naibu wake ni Salma Mohamed Mwasa (CUF).

Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko amekuwa waziri kivuli wa wizara ya Maliasili na Utalii huku naibu wake akiwa Cecilia Pareso (wote Chadema).

“Antony Komu atakuwa waziri wa Viwanda, Biashara na Uchumi na naibu wake ni Cecil Mwambe. Wizara ya Elimu atakuwa Susan Lyimo na naibu wake ni Dk Ally Suleiman Yusuf. Wizara ya Maji na Umwagiliaji ni Hamidu Hassan Bobali na naibu wake ni Peter Lijualikali,” alisema Mbowe.

Alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto waziri kivuli ni Dk Godwin Mollel na naibu wake ni Zubeda Sakul, Katiba na Sheria waziri kivuli ni Lissu na naibu wake ni Abdallah Mtolea (CUF).”

Uchaguzi wa wajumbe

Akitangaza wabunge walioshinda katika uchaguzi huo, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema idadi ya wajumbe waliorudisha fomu za kuwania nafasi hizo ilikuwa inalingana na idadi ya nafasi zilizokuwa zikiwaniwa, hivyo kuwafanya wote kupita bila kupigiwa kura.

Tume ya Utumishi wa Bunge

Kangi Lugola, Fakharia Shomar Khamis, Mary Chatanda, Mussa Azzan Zungu, Salim Hassan Turky, Magdalena Sakaya na Peter Msigwa.

Bunge la Afrika

Mboni Mhita, Asha Abdullah Juma, Dk Faustine Ndugulile, Stephen Masele na David Silinde.

Jukwaa la Wabunge wa SADC

Jamal Kassim Ali, Esther Mmasi, Selemani Zedi na Ally Abdallah Saleh.

Kamati ya Utendaji ya Bunge la Jumuiya ya Madola

Amina Mollel, Maria Kangoye, Zainab Vullu, Khamis Mtumwa Ali, Salum Rehani, Japhet Hasunga, Josephat Kandege, Dk Raphael Chegeni, Jitu Soni, Immaculate Semesi, Juma Hamad Omar na Tundu Lissu.

Umoja wa Mabunge Duniani Dk Pudenciana Kikwembe, Juma Othman Hija, Mohamed Mchengwerwa, Peter Serukamba na Susan Lyimo.



ZeroDegree.
Mbowe atangaza baraza la mawaziri vivuli, wajue wanaounda baraza hilo hapa. Mbowe atangaza baraza la mawaziri vivuli, wajue wanaounda baraza hilo hapa. Reviewed by Zero Degree on 2/06/2016 11:42:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.