Loading...

JK kumkabidhi Magufuli CCM mapema.


Mwenyekiti wa CCM na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akiwasili kwenye Ofisi ya CCM mkoa wa Singida jana kwa ajili ya kuongoza maadhimisho ya Miaka 39 ya CCM, ambayo kilele chake kitaifa ni leo. Kushoto ni Mama Salma Kikwete, na wengine ni Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Mbunge wa Mtama Nape NNauye na Kaimu Katibu wa CCM mkoa wa Singida Mary Maziku.

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete ametangaza rasmi kwamba sherehe za leo za maadhimisho ya miaka 39 tangu chama hicho kianzishwe ni za mwisho kwake akiwa mwenyekiti.

Kikwete alisema ana furaha kwa kuwa alianzia kazi ya kuitumikia CCM kwa mara ya kwanza mjini Singida Aprili, 1975 na anamalizia Singida.

Alisema hayo jana jioni wakati akizungumza na wazee wa Manispaa ya Singida katika ukumbi wa mikutano wa Kanisa Katoliki mjini hapa.

Kauli hiyo ya Kikwete inadokeza kuwa huenda akaachia mapema uenyekiti wa chama kwa Rais John Magufuli kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake. Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliachia mapema nafasi hiyo kama alivyoachiwa na aliyemtangulia, Ali Hassan Mwinyi.

Kulingana na kalenda ya chama hicho, Mkutano Mkuu CCM wa kumchangua mwenyekiti unapaswa kufanyika mwaka 2017, lakini endapo Kikwete ataamua kuachia mapema nafasi hiyo unaweza kufanyika mapema zaidi.

Mwenyekiti huyo akiambatana na mkewe, Mama Salma, alitembelea na kupiga picha kwenye nyumba aliyoishi alipokuwa Katibu msaidizi wa Tanu Wilaya ya Singida Mjini mwaka 1975.

Aliwashukuru wazee wa Singida kwa juhudi zao za kuisaidia CCM kupata ushindi katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

“Mkutano mkuu uliopita ulijaa changamoto nyingi na kwa kifupi, ulikuwa mgumu mno. Bila busara zenu ninyi wazee, kwa sasa pengine tungekuwa tunazungumza hadithi nyingine. Mmefanya kazi kubwa, msichoke endeeni kukitetea chama chenu ili amani na utulivu iendelee kudumishwa,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa miaka yote Mkoa wa Singida umeendelea kuwa ngome imara ya CCM, kwa hali hiyo aliwataka wazee wasiache sifa hiyo ikapotea. Akizungumzia Serikali ya Awamu ya Tano, Kikwete alisema anaiunga mkono na kuitakia kila la heri katika kuwatumikia wananchi.

“Niwaombe na ninyi wazee na wakazi wote wa Mkoa wa Singida, muiunge mkono Serikali hii ya Awamu ya Tano imeonyesha dalili nzuri katika kutekeleza majukumu yake. Mkiacha kuiunga mkono, mtaikatisha tamaa na kwa hali hiyo itashindwa kuwatumikia wananchi ipasavyo,” alisema. 

Hotuba hiyo ya Kikwete ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 39 ya chama hicho yanayofikia kilele chake leo ambapo viongozi mbalimbali akiwamo Rais John Magufuli watahudhuria.

Credits: Mwananchi




ZeroDegree.
JK kumkabidhi Magufuli CCM mapema. JK kumkabidhi Magufuli CCM mapema. Reviewed by Zero Degree on 2/06/2016 11:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.