Mgogoro wa mlima watatuliwa.
Sengerema. Mgogoro wa ardhi kati ya Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Karumo, Tiba Magambo na mmiliki wa Mlima Lwepsi, Tiba Nsiyonka, umemalizika baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuingilia kati.
Mgogoro huo wa mlima uliopo Kitogoji cha Chigoto wilayani hapa, umemalizika baada ya Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Simon William kuwafafanulia sheria inavyotaka.
Akizungumza kwenye mkutano wa kijiji jana, William alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 na ile ya Mazingira ya mwaka 2004, mtu asipoitumia ardhi yake kwa miaka 12 itakuwa siyo mali yake na kwamba, milima, mito au maziwa ni rasilimali za Taifa.
“Sheria hairuhusu mtu kuwa na umiliki wa milima au vyanzo vyovyote vya maji mfano maziwa au mito,” alisema.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Yanga Makaga aliwataka wananchi waliovamia maeneo ya wazi kuondoka kabla sheria haijachukua mkondo wake.
Hata hivyo, Nsiyonka alisema hakubaliani na uamuzi huo, anatarajia kwenda mahakamani.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, walikiri eneo la mlima huo miaka ya 1950 alikuwa akiishi mzee Wahalalika Nsiyoka hadi alipofariki na kurithisha watoto wake.
ZeroDegree
Mgogoro wa mlima watatuliwa.
Reviewed by Zero Degree
on
2/03/2016 06:22:00 PM
Rating: