Mradi wa mabasi yaendayo kasi bado ‘kizungumkuti’
Dar es Salaam. Licha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuagiza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka uwe umeanza kazi tangu mwezi uliopita, hakuna dalili kama huduma hiyo ya usafiri itatolewa jijini hapa katika siku za karibuni.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo Desemba 19 mwaka jana aliposema mradi huo uwe umeanza kazi ifikapo Januari 11, lakini ilishindikana kutokana kukosekana mwafaka wa tozo ya nauli.
Kutokana na mkwamo huo, Majaliwa aliwaagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa pamoja na wadau kukutana kupanga upya viwango hivyo na kama watashindwa, Serikali itaendesha mradi huo.
Serikali haikuridhishwa na viwango vya nauli ya mabasi hayo ambavyo vilikuwa; kutoka Mbezi hadi Kimara Sh700, Mbezi – Kariakoo Sh1,200 na Mbezi – Mwenge Sh1,400 na wanafunzi kulipa nusu ya viwango hivyo vya nauli.
Meneja wa Miundombinu wa Dart, Mohamed Kuganda alisema kinachokwamisha kuanza kwa mradi huo ni mchakato wa nauli unaoshughulikiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
“Upande wetu kila kitu kipo tayari na tunasubiri tu, wamalize masuala yanayokwamisha... Hapa ofisini hatuna kazi kwa sababu kama ni miundombinu tayari jambo hilo limekamilika,” alisema.
Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alisema: “Sisi hatujachelewesha kuanza kwa mradi wa Dart, sheria inaturuhusu kupanga nauli ndani ya siku 60 baada ya kupokea maoni ya wadau. Kwa hiyo, bado tuko ndani ya wakati na tunajitahidi kufanya kazi kwa haraka ili uanze.”
Alisema hata kama Sumatra ikitoa nauli elekezi, mradi huo hauwezi kuanza mara moja kwa sababu kuna mambo mengi yanayochelewesha kuanza kwake, ikiwamo kukosekana kwa mabasi yenyewe.
“Hata tukitangaza nauli leo, hayo mabasi ya kuanza kazi yako wapi? Hili siyo suala la taasisi moja tu, sisi kwa upande wetu tunashughulikia suala la nauli, pamoja na leseni...,” alisema Mziray.
Mwenyekiti Mtendaji wa Simon Group, Robert Kisena hakupatikana jana alipofuatwa ofisini na alipopigiwa simu hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu.
Simbachawene alipoulizwa jana kuhusiana na mchakato wa kuanza kwa mradi huo, alisema tatizo ni mwekezaji.
Hata hivyo, alisema jambo muhimu ni kuhakikisha mradi huo unaanza kwa ufanisi na kukidhi matarajio ya wananchi.
ZeroDegree.
Mradi wa mabasi yaendayo kasi bado ‘kizungumkuti’
Reviewed by Zero Degree
on
2/04/2016 11:53:00 AM
Rating: