Loading...

Uchaguzi wa meya Kinondoni naTemeke kurudiwa tena.


Dodoma. Uchaguzi wa mameya katika manispaa za Temeke na Kinondoni, Dar es Salaam utarudiwa katika kipindi kifupi kuanzisha sasa baada ya Serikali kutangaza wilaya sita mpya zikiwamo mbili za mkoa huo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alipokuwa akitangaza rasmi kuanzishwa kwa Mkoa wa Songwe unaomegwa kutoka Mbeya pamoja na wilaya hizo.

Hata hivyo, alisema mchakato wa kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam unaendelea na uchaguzi utafanyika Februari 8 kama ilivyopangwa.

“Suala la kuwa watakuja kurudia uchaguzi, hilo halikwepeki kwani Serikali inafanya haraka kuanzisha mamlaka na ukishakata eneo la utawala lazima uchaguzi utatakiwa kufanyika siyo jambo geni hilo,” alisema Simbachawene.

Alibainisha kuwa hata uchaguzi wa Meya wa Jiji unaweza kurudiwa kwa kuwa mara baada ya uchaguzi katika halmashauri hizo, ni wazi kuwa waliochaguliwa watataka kuhoji. Kinondoni hivi sasa inaongozwa na meya wa Chadema kupitia Ukawa, Charles Kuyeko na Temeke meya wake, Abdallah Chaurembo anatoka CCM.

Akizungumzia hatua hiyo, Katibu wa Chadema, Kanda ya Dar es Salaam, Henry Kilewo alisema uamuzi huo wa Serikali hauwaumizi kichwa kwa sababu hata ukifanyika uchaguzi wa mameya wa Ubungo na Kinondoni, Ukawa itaibuka kidedea. “Mgawo huu walioufanya itakula kwao. 

Tuliujua mchezo huu mapema, kwa hiyo hivi sasa tunasubiri tu watuambie uchaguzi unafanyika lini,” alisema Kilewo. Alisema baada ya kuitangaza Manispaa ya Ubungo, kimahesabu bado Ukawa ipo juu ya CCM kutokana na idadi ya wajumbe wa baraza la madiwani katika manispaa hizo mbili isipokuwa Kigamboni. 

Kwa upande wake, Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alisema endapo uchaguzi utarudiwa atalazimika kugombea nafasi hiyo Ubungo na kwamba ana uhakika atashinda. “Nitakwenda kugombea nafasi hii Ubungo. 

Hata hivyo, Kinondoni pia itabaki chini ya Ukawa kwani tuna hazina ya madiwani wa kutosha wakiwamo wa viti maalumu,” alisema Jacob.

Katibu wa Uenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba ‘Gadaffi’ alipoulizwa kuhusiana na hatua hiyo, alisema asingeweza kuzungumza kwani alikuwa katika kikao.

Akizungumzia kuanzishwa kwa mkoa huo na wilaya hizo, Simbachawene alisema mchakato wake ulianza muda mrefu na sasa Rais ameridhia.

 Alizitaja wilaya zilizoanzishwa ambazo mchakato wake unaanza mara moja kuwa ni Ubungo na Kigamboni (Dar), Tanganyika (Katavi), Kibiti (Pwani) Songwe (Songwe) na Malinyi (Morogoro).

Alisema Sheria ya Uanzishaji wa Mikoa na Wilaya, Sura ya 397 inamwelekeza Rais taratibu za kufuata anapotaka kuanzisha mkoa na wilaya.

 “Kwa kutumia madaraka hayo ya kikatiba, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete mnamo tarehe 18/10/2015 alitangaza nia ya kuugawa Mkoa wa Mbeya na kuanzisha mkoa mpya wa Songwe kwa tangazo la Serikali Na. GN 461,” alisema Simbachawene.

Alisema Rais katika tarehe hiyohiyo alitoa tangazo GN. 462 lililokusudia kuanzisha wilaya za Songwe, Kibiti, Ubungo, Kigamboni, Malinyi na Tanganyika na kwamba ilipofika Januari 18, Rais John Magufuli alisaini rasmi amri ya kuanzishwa kwa maeneo hayo ya kiutawala.

Waziri aliwaagiza wakuu wa mikoa ambako kumeanzishwa maeneo mapya ya kiutawala, kuanzisha mchakato wa haraka wa kutafuta majengo ya kuanzia ofisi zake na kwamba wakati wowote Serikali itawateua watu muhimu katika kuanzisha shughuli za kiserikali.

Akizungumzia ongezeko la maeneo ya utawala kama ni kubana au kuongeza matumizi, Waziri alisema siyo shida kwani cha muhimu ni kusogeza huduma karibu na wananchi.


Credits: Mwananchi





ZeroDegree.
Uchaguzi wa meya Kinondoni naTemeke kurudiwa tena. Uchaguzi wa meya Kinondoni naTemeke kurudiwa tena. Reviewed by Zero Degree on 2/04/2016 11:46:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.