Vigogo 11 wa Kampuni ya Reli Tanzania [ TRL ] wakifikishwa Mahakamani kwa ununuzi wa mabehewa feki 25.
Dar es Salaam. Vigogo 11 wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), akiwamo mkurugenzi mtendaji aliyesimamishwa, Kipallo Kisamfu wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka tisa, saba ya matumizi mabaya ya madaraka na mawili ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri wao.
Akisoma mashtaka hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru, mwendesha mashtaka wa Takukuru, Maxi Ali aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni mhasibu mkuu, Jasper Kisiraga na mhandisi mkuu, Mathias Massae.
Wengine ni Muungano Kaupunda, ambaye ni kaimu mhandisi mkuu wa mitambo, Ngoso Ngosomwiles (mhandisi mkuu wa mitambo), Pachal Mafikiri (mhandisi wa mitambo), Kedmon Mapunda (mhandisi wa mitambo), Felix Kashaigili (kaimu mhandisi wa mawasiliano), Lowrand Simtengu (mkuu wa usafirishaji wa reli), Joseph Syaizyagi (msanifu mkuu), na Charles Ndege, ambaye ni meneja uchukuzi.
Akisoma hati ya mashtaka jana, Maxi alidai kuwa kati ya Februari 1, 2013 na Juni 30, 2014, Kipallo akiwa mkurugenzi mtendaji wa TRL alishindwa kusimamia mkataba wa zabuni kama inavyotakiwa kwenye masharti na vigezo vya Sheria ya Manunuzi ya Umma na kusababisha kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industries Limited kunufaika.
Mwendesha Mashtaka huyo wa Takukuru pia alidai kuwa kati ya Julai mosi na Agosti 31, 2013, Mafikiri aliidhinisha michoro ya mabehewa yanayotumika kubeba kokoto za kutengenezea njia ya reli yajulikanayo kama Ballast Hopper Wagons iliyoandaliwa na kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industries Limited, kinyume na vigezo na masharti ya mkataba.
Alidai pia kuwa Kisiraga na Mathias Agosti 5, 2014 walitumia madaraka yao vibaya kuidhinisha malipo ya dola 1,280,593.75 za Kimarekani 1,280,593.75 kupitia makubaliano ya barua ya kibenki (sight Irrevocable letter of credit) kwa kampuni hiyo ya M/S Hindusthan bila ya kuthibitisha kiwango cha ubora wa mabehewa hayo 25 katika muda waliopewa.
Katika shtaka jingine, Kisiraga anadaiwa kuidhinisha malipo ya dola 1,280,593.75 za Marekani kabla ya kuisha kwa muda wa uangalizi wa mabehewa hayo.
Muungano anadaiwa kuiidhinisha kampuni ya M/S Hindusthan kuingiza mabehewa hayo 25 kati ya Januari Mosi na Februari 28,2014 bila ya kufuata masharti ya zabuni na Sheria ya Manunuzi ya Umma. Pia anadaiwa kutoa ripoti ya uongo kwa mwajiri wake kuhusu ubora wa mabehewa hayo bila kuyafanyia ukaguzi akifahamu kuwa ni uongo.
Mshtakiwa mwingine, Ngoso anadaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Mei 31, 2014 aliidhinisha kampuni hiyo kusafirisha mabehewa hayo 25 kwa meli bila kuhakikisha kama yametengenezwa katika viwango na ubora unaokubaliwa kulingana na mkataba.
Ngoso pia anadaiwa kuwa, akiwa mhandisi mkuu wa mitambo na meneja wa ajira wa TRL, alitoa ripoti ya uongo kuhusu mabehewa katika ukaguzi na utengenezwaji wake.
Pia Muungano, Kedmon, Felix, Lowland na Joseph wanadaiwa kuwa wakiwa wajumbe wa bodi ya zabuni, kati ya Januari Mosi na Februari 28, 2013 waliruhusu kuingizwa kwa mabehewa ambayo hayakidhi vigezo vya ubora.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Washtakiwa watatu kati yao wako nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana.
Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Vigogo 11 wa Kampuni ya Reli Tanzania [ TRL ] wakifikishwa Mahakamani kwa ununuzi wa mabehewa feki 25.
Reviewed by Zero Degree
on
2/13/2016 12:00:00 PM
Rating: