Loading...

Watu wasiojulikana wamvamia diwani [ wa kimwani wilayani Muleba mkoa wa Kagera ] na kumuua kwa mapanga.


Muleba. Diwani wa Kimwani wilayani Muleba Mkoa wa Kagera, Sylvester Muliga (CUF) amefariki dunia baada ya kuvamiwa na watu wasiojulika usiku wa kuamkia juzi nyumbani kwake na kumjeruhi kwa mapanga.

Mkuu wa Polisi wilayani Muleba, Salvas Makweli alikiri kutokea kwa tukio hilo huku akisema wanamshikilia mtu mmoja ambaye amewataja wenzake waliokimbia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Joseph Mkude alisema diwani huyo alifariki dunia jana saa saba usiku wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kagondo.

Mkude alisema taratibu za mazishi zinafanywa na uongozi wa halmashauri kwa kushirikiana na viongozi wa vyama vya siasa ili aweze kuzikwa kijijini kwake Kagulamo.

Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kyota, Kata ya Kimwani, Daudi Kiluma alisema watu wasiojulikana walimvamia diwani huyo saa mbili usiku.

“Watu hao walimtaka afungue mlango, watoto walipowafungulia, walimkata mapanga mawili kichwani kisha kukimbia, wananchi walifika na kumuwahisha hospitali kwa matibabu lakini alifariki dunia,” alisema Kiluma.

Kiluma alisema mtu mmoja anayedaiwa kuhusika na tukio hilo amekamatwa anaendelea kuhojiwa polisi.

Alisema kwa mujibu wa polisi, mtuhumiwa huyo alikuwa na wenzake ambao waliahidiwa kupatiwa Sh1.5 milioni na kwamba walitanguliziwa Sh150,000 ili wakamilishe kazi.

Mwenyekiti wa Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Wilaya ya Muleba, Alhaji Khalid Hussein (Chadema) ambaye pia ni Diwani wa Kasharunga amelaani mauaji hayo na kutaka polisi kuwasaka wahusika.

Alhaji Hussein alisema mauaji hayo yanadaiwa kuhusishwa na masuala ya kisiasa kutokana na msimamo wa Muliga kuibana halmashauri kutoa haki za wananchi katika kutekeleza miradi ya maendeleo.



ZeroDegree.
Watu wasiojulikana wamvamia diwani [ wa kimwani wilayani Muleba mkoa wa Kagera ] na kumuua kwa mapanga. Watu wasiojulikana wamvamia diwani [ wa kimwani wilayani Muleba mkoa wa Kagera ] na kumuua kwa mapanga. Reviewed by Zero Degree on 2/02/2016 04:56:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.