Loading...

Kitendo cha Polisi kuingia bungeni chapingwa kila kona.


Askari wakiwatoa wabunge wa kambi ya upinzani kwenye Ukumbi wa Bunge Dodoma hivi karibuni baada ya kudaiwa kukaidi amri ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ya kuwataka watoke.



Moshi. Wasomi wameunga mkono kauli ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo aliyoitoa juzi ya kutaka mhimili wa Serikali usiingilie wa Bunge.

Kauli za wasomi na Askofu Shoo zilisukumwa na tukio la wiki iliyopita la polisi zaidi ya 50 kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge kuwatoa wabunge wa upinzani.

Askofu huyo alisema: “Sisi Watanzania tunatarajia kuona na kusikia hoja zikijadiliwa kwa uwazi na katika hali ya kistaarabu. Kwa kuchezeachezea heshima hii ya Bunge sasa tunaona juzijuzi tu jeshi linaingia bungeni.”

Akizungumzia kauli hiyo, Profesa wa Chuo Kikuu cha St Augustine (Saut), Mwesiga Baregu alisema kama mwingiliano huo utaendelea, ipo hatari ya Bunge kupoteza hadhi yake kitaifa na kimataifa.


 Alisema kitendo hicho cha Polisi ambao ni mhimili wa Serikali kuingizwa ndani ya ukumbi wa Bunge ni aibu kubwa ambayo inadhalilisha chombo hicho alichoita kitakatifu.

“Bunge lina hadhi yake, lina kinga, lina haki zake na lina wajibu wake. Sasa kama halipati haki zake ni wazi litashindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba, polisi bungeni ambako hata raia wa kawaida kuingia kwao kunahitaji ruksa fulani ni udhalilishaji,” alisema.

Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ambaye sasa ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Makumira (Tuma) Arusha, Lawrence Mchome alisema mwingiliano wa mihimili ni jambo lisilokubalika.

“Kitendo cha kuingiza polisi ndani ya Bunge si sahihi lakini hata kuweka Spika na naibu ambao ni wabunge wanaotokana na vyama vya siasa siyo sahihi na matatizo yanaanzia hapo,” alisema.

Jaji Mchome alisema kwa nchi nyingine, mtu akichaguliwa kuwa Spika anapaswa kujiuzulu ubunge na uanachama wa chama cha siasa ili awe kama refa akitolea mfano wa Uganda.

“Tatizo letu tunafanya maigizo. Huwezi kuchagua Spika ambaye ni mwanachama wa CCM halafu utegemee atende haki. Itafika mahali lazima asimamie masilahi ya chama chake,” alisema.

Jaji Mchome alisema kinachoonekana Tanzania haitaki kukomaa kidemokrasia kwani baadhi ya wanasiasa hasa kutoka CCM kuwa bado na mawazo ya mfumo wa chama kimoja.

“Hili la kuleta mapolisi kunafanya Bunge lionekane kama ni kikundi cha watu wasiostaarabika wakati sisi tunalichukulia kama mhimili muhimu sana wa watu walio makini kimaamuzi,” alisema.

Mhadhiri msaidizi wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii Chuo Kikuu Iringa (IOU), Emaniel Damalo, alisema kilichotokea bungeni ni tatizo la Tanzania kutokuwa na Katiba bora.

 “Hili ni tatizo la Katiba. Nchi yetu haijafikia mahali pa kutofautisha kati ya Bunge na Serikali. Kuna mambo mengi yanatokea chini ya zulia ambayo sisi hatuyaoni,” alisema.

Damalo alisema suluhisho la uhuru wa mihili ya dola ni kupatikana kwa Katiba bora itakayotoa uhuru wa kweli kuliko ilivyo sasa.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Andrew Temu alisema uamuzi wa kuingiza polisi ndani ya Bunge ulikuwa ni wa pupa. 

“Ilitakiwa kuwepo miongozo ya kutosha kwanza au hata kuahirisha Bunge lakini ule uamuzi wa kuingiza mhimili wa pili (Serikali) bungeni naona ulifanyika kwa haraka. “Tunategemea wabunge hawawezi kukubaliana tu kirahisi lakini siyo wakishindwa kukubaliana harakaharaka tu unaingiza jeshi. Hii si sahihi.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Mocu), Eligius Danda alisema kinachotokea bungeni ni kuumiza demokrasia na wanaoumizwa zaidi na mvutano huo ni wananchi.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dk Hosea Lunogelo alisema Taifa linapaswa kujiuliza kwa nini wabunge wanafanya mambo yanayolazimisha polisi wa ziada kuingia bungeni.

“Maana bila shaka kama Spika angeachia fujo bungeni na kuleta majeraha kwa wabunge bado angelaumiwa kwa nini hakuita msaada wa ziada,” alisema Dk Lunogelo: “Tushughulikie sababu zinazowafanya baadhi ya wabunge wa upinzani kufanya fujo na sababu gani zinawafanya baadhi ya wabunge wa CCM wasipende kusikiliza hoja za wapinzani hata kama zina mantiki.”

Dk Lunogelo alisema inawezekana mojawapo ya sababu ni kukosa malezi na makuzi ya mijadala ya kidemokrasia miongoni mwa wabunge ambao ni vijana.

Mwenyekiti wa Tanganyika Law Society (TLS), tawi la Moshi, David Shilatu alisema hakuona sababu ya Serikali kuingiza polisi bungeni wakati hapakuwa na fujo yoyote.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema: “Kitendo kile hakikutupendeza kwa sababu katika misingi ya utawala bora, kuna vitu vitatu ambavyo ni utawala wa sheria, mgawanyo wa madaraka na uhuru wa Mahakama. Ni lazima haya yaheshimiwe.”

Henga alisema misingi hiyo ya utawala bora inataka kila mhimili wa dola ufanye mambo yake kwa uhuru bila kuingiliana lakini kitendo cha kuingiza hadi mbwa Bungeni ni kuushusha thamani mhimili wa Bunge.




ZeroDegree.
Kitendo cha Polisi kuingia bungeni chapingwa kila kona. Kitendo cha Polisi kuingia bungeni chapingwa kila kona. Reviewed by Zero Degree on 2/02/2016 09:32:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.