Loading...

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aahidi kuzifutilia mbali Halmashauri zote zitakazoshindwa kukusanya mapato asilimia 80.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema halmashauri itakayokusanya mapato chini ya asilimia 80 ya bajeti yake itafutwa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (Alat), Majaliwa alisema mamlaka hiyo ya serikali za mitaa zina jukumu la kukusanya na kusimamia mapato yote ya halmashauri.

“Halmashauri nchini ambayo itashindwa kukusanya mapato asilimia 80, inayo sababu ya kufutwa,” alisema.

Alisema kisheria halmashauri ni vyombo vya usimamizi wa ukusanyaji wa mapato na matumizi.

Kadhalika, Waziri Mkuu alisema kwa muda wa miaka 17 Serikali imekuwa ikizijengea uwezo halmashauri kukusanya na kusimamia mapato yake, lakini si halmshauri zote zimeweza kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi.

Alisema anazo taarifa kuwa baadhi ya watumishi wa halmashauri ndiyo wanamiliki kampuni za ukusanyaji wa mapato, kwenye halmashauri zao na hivyo kufanya utekelezaji wa mfumo wa elektroniki kukwama.

Alisema ikibainika kuna ukweli katika jambo hilo, watumishi hao watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Kuhusu rushwa, Majaliwa alisema kumekuwapo kwa tatizo la rushwa ambapo maeneo yanayolalamikiwa ni pamoja na ardhi, elimu, afya na utoaji wa leseni katika serikali za mitaa.

“Wananchi wanakosa haki zao na maisha yao kuwa duni kutokana na hali inayojitokeza ya dhuluma, ufisadi na jeuri wanaofanyiwa na watoaji na wapokeaji rushwa,”alisema Majaliwa.

Akizungumzia migogoro ya ardhi, Majaliwa alisema inasababishwa na mipango mibovu ya ardhi katika halmashauri.

Aliwataka mameya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri kuhakikisha kuwa wanapanga mipango ya ardhi ili kuepuka migogoro hiyo.

Mwenyekiti wa Alat, Gulam Mukadam alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni ucheleweshaji wa ruzuku na fedha za miradi ya maendeleo.

Pia alimwomba Majaliwa kuangalia posho za madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Alisema posho hizo zilikuwa ni Sh120, 000 lakini ikapandishwa na kufikia Sh350,000.




ZeroDegree.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aahidi kuzifutilia mbali Halmashauri zote zitakazoshindwa kukusanya mapato asilimia 80. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aahidi kuzifutilia mbali Halmashauri zote zitakazoshindwa kukusanya mapato asilimia 80. Reviewed by Zero Degree on 4/09/2016 05:31:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.