Loading...

Donald Ngoma aomba kuondoka Yanga, Mbuyu Twite afungasha.


Dar es Salaam. Wakati mshambuliaji Donald Ngoma akiuomba uongozi wa Yanga kumuuza, mchezaji mwenzake Mbuyu Twite amesema chanzo cha kuondoka kwake ni kocha Hans Pluijm na katibu Mkuu, Baraka Deusdedit.

Maombi hayo ya Mzimbabwe huyo yanatokana na kuwepo kwa taarifa kwamba Al Ahly ya Misri, ambayo imeshatwaa ubingwa wa Afrika mara nane, na klabu nyingine kutoka Uturuki na Yugoslavia zimevutiwa na kiwango chake.

Mmoja wa viongozi wa Yanga aliliambia gazeti hili kuwa Ngoma ameuangukia uongozi wa Yanga akiutaka umpe nafasi ya kwenda kucheza soka nje ya Tanzania iwapo itatokea timu itakayofikia dau lake.

“Ngoma anataka kuondoka. Tayari ameshautaarifu uongozi juu ya hilo, lakini bado uongozi unasita kumruhusu kutokana na mchango na umuhimu wake mkubwa kikosini,” alisema mmoja wa watu walio karibu na uongozi ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

“Ukitaka kulithibitisha hilo, tazama ukurasa wake wa Instagram, soma kwa umakini ujumbe ambao mara nyingi amekuwa akitoa. Ni wazi kuwa unaashiria anataka kuondoka.”

Miongoni mwa ujumbe alioandika Ngoma kwenye ukurasa huo wa mtandao wa kijamii ni “ndoto zinachelewa, ila haziaihirishwi”, wakati mwingine unasema “siku yangu ya kwanza Tanzania, ya mwisho ipo njiani”, ikiambatana na picha yake akitoka katika mlango wa kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kocha Pluijm alikataa kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba si siku ya kazi.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro aliwatoa wasiwasi wanachama na mashabiki wa timu hiyo akiwataka watulie.

“Kipindi kama hiki watasikia mengi, lakini watambue kuwa uongozi wao upo makini katika kuhakikisha timu inaendelea kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa. Hizo ni tetesi tu ambazo hazina ukweli wowote,” alisema Muro.

Twite afungasha Yanga


Katika hatua nyingine, Twite ameachana rasmi na Yanga huku kukiwa na taarifa kuwa kuondoka kwake kumechangiwa na Pluijm na katibu mkuu.

Mbuyu anayeishi Magomeni jijini Dar es Salaam alilithibitishia gazeti hili kuachana na mabingwa hao wa Bara.

“Nilijua nitaongeza mkataba baada ya ule wa awali kumalizika, lakini kocha na katibu walinifuata na kuniambia kiwango changu kimeshuka,” alisema Twite.

“Siamini kama kweli kiwango changu kimeshuka, lakini siwezi kuwakatalia wala kubishana na mtazamo wao.”

Lakini Deusdedit alikana kuwapo na suala hilo.

“Mimi nafuata maelekezo ya benchi la ufundi. Hata hivyo siwezi kumwambia mchezaji eti kashuka kiwango, hata kocha sidhani kama anaweza kufanya hivyo,” alisema.

“Ninachojua tuna mpango wa kumuongezea mkataba Mbuyu Twite.”

Hata hivyo hakueleza kama wameanza mazungumzo.

Twite alisejiliwa na Yanga baada ya kutamba kwenye michuano ya Kombe la Kagame na Chalenji na alitamba msimu uliopita akicheza upande wa kulia wa ngome na wakati mwingine kuhamishiwa katikati, lakini msimu huu amekuwa akitumika kwa nadra.

Source: Mwananchi




ZeroDegree.
Donald Ngoma aomba kuondoka Yanga, Mbuyu Twite afungasha. Donald Ngoma aomba kuondoka Yanga, Mbuyu Twite afungasha. Reviewed by Zero Degree on 5/30/2016 03:59:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.