Loading...

Hizi hapa Sababu za Bandari ya Dar es Salaam kukosa mizigo.


Dodoma. Kamati ya Bunge ya Miundombinu imebaini sababu sita ambazo zimesababisha kupungua kwa shehena za mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kodi zinazotozwa kwa watoa huduma zitolewazo kwenye mizigo ya nje.

Sababu hizo zilibainishwa jana na mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Norman Sigalla alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Alizitaja sababu nyingine kuwa ni kutozwa kwa pamoja kwa tozo za ‘Port Storage na Custom Warehouse Rent’. Pia, ushindani mkubwa katika kupakua na kupakia mizigo. Wakati katika Bandari ya Dar es Salaam inachukua siku tisa bandari nyingine kama Durban ni siku nne tu.

Sababu nyingine zilizotajwa na Dk Sigalla ni pamoja na kuwapo kwa mamlaka nyingi ambazo zinasababisha ucheleweshwaji wa uondoshwaji wa mizigo bandarini akitolea mfano Sumatra, Ewura, Wakala wa Vipimo, TRA, TBS, TFDA na Maabara ya Kemia ya Serikali.

“Sababu nyingine ni kutofautiana kwa gharama za tozo za bandari baina ya nchi na nchi ambapo za Tanzania ziko juu,” alisema Dk Sigalla na kumalizia kuwa sababu nyingine ni shehena inayosafirishwa nje ya nchi kupewa siku 30 tu tofauti na bandari nyingine shindani bila kujali mazingira ya usafirishaji wa barabara ndani na nje ya nchi iendako.

Dk Sigalla alisema kama Serikali haitazifanyia kazi changamoto hizo, kuna uwezekano wa Tanzania kupoteza wateja wengi waliokuwa wakitumia Bandari ya Dar es Salaam na kuhamia katika bandari nyingine shindani za Mombasa – Kenya, Beira – Msumbiji, Durban – Afrika Kusini na Walvis Bay – Namibia ambazo zimeweka mazingira rafiki na wafanyabiashara na kuwavutia wengi.

“Pamoja na malengo mazuri ya Serikali katika jitihada za kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za utendaji hafifu wa reli kufikia asilimia moja kwa mwaka ikilinganishwa na asilimia 10 mwaka 2008, jambo linalosababisha mizigo mingi kusafirishwa kwa njia ya barabara,” alisema Dk Sigalla ambaye pia ni Mbunge wa Makete.

Alisema msongamano katika jiji la Dar es Salaam unaathiri uondoshaji wa mizigo kutoka bandarini pamoja na ubovu wa barabara zinazoingia na kutoka bandarini na zile zinazounganisha bandari na bandari kavu.

“Changamoto nyingine ni kutokuwapo kwa maegesho kwa ajili ya magari yanayoenda kupakia mizigo bandarini,” alisema Dk Sigalla.




ZeroDegree.
Hizi hapa Sababu za Bandari ya Dar es Salaam kukosa mizigo. Hizi hapa Sababu za Bandari ya Dar es Salaam kukosa mizigo. Reviewed by Zero Degree on 5/18/2016 10:36:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.