Loading...

Unazijua sababu za Simba kukosa ubingwa..?? Soma hapa sababu 4 zilizotolewa na Rais wa Simba, Evance Aveva.


Dar es Salaam. Rais wa Simba, Evance Aveva ametoa sababu nne zilizoikosesha klabu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu msimu huuna kuwaomba radhi wanachama na mashabiki kwa yote yaliyotokea.

Aveva alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na wanahabari akieleza kuwa wao (viongozi) walijitahidi kuhakikisha timu inapata maandalizi mazuri kabla ya kuanza msimu, hata hivyo bado hawakupata kile walichotarajia.

Alisema walikuwa na sababu za msingi za kufikia malengo kabla ya msimu kuanza, lakini kuna sababu nne za kutofikiwa kwa malengo yao.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni; wachezaji kutoendana na maadili ya klabu,ushindani wa ligi, utendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na usajili mbovu, hasa kwa wachezaji wa kigeni.

1. Wachezaji kutoendana na maadili ya klabu

“Simba ndiyo klabu inayotoa bonasi kubwa kwa wachezaji pia tulijaribu kuanzisha tuzo ya mchezaji bora wa kila mwezi ili kuwapa motisha wachezaji kufanya vizuri na tumekuwa tukiwahamasisha kila mara, lakini pamoja na vitu vyote hivyo bado hatukufikia malengo.

“Tumekuwa na baadhi ya wachezaji ambao hawakuendana na maadili ya klabu na hawakuipenda timu na kuipigania kwa moyo kwani kuna matukio wanafanya mpaka yanaumiza.

“Mfano, Hassan Kessy kwenda Yanga wakati bado ana mkataba, pia Ibrahim Ajib anacheza rafu jioni kwenye mechi anapewa kadi nyekundu, usiku unatumiwa ujumbe mfupi wa simu kuwa kesho anaondoka saa nne kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio,” alisema.

Aliongeza: “Sasa unajiuliza, alikata saa ngapi tiketi ya ndege kama hiyo safari hakuipanga mapema, je, alifanya makusudi kucheza rafu ili apate kadi ndipo aondoke kwenda kufanya majaribio, ni mambo yanayoumiza.

“Wengine wanawashinikiza wenzao wagome wasiende kucheza mechi Songea, kisa mshahara umechelewa, tena ushahidi tunao, kwani mshahara kuchelewa ndiyo ugome,” alisema.

2. Usajili mbovu wachezaji wa kigeni

“Nikiri msimu huu hatukuzitendea haki nafasi saba za wachezaji wa kigeni,wengi hawakuwa katika ubora unaotakiwa, lakini niahidi msimu ujao tutasajili wachezaji watakaokidhi matakwa ya klabu, iwe wa ndani au nje ya nchi,pia tutaboresha benchi zima la ufundi,”alisema Aveva.

3. Ushindani wa ligi kuwa mkubwa

“Nikiri ushindani uliopo sasa kwenye ligi ni mkubwa tofauti na zamani ulikuwa unaifikiria timu moja, yaani Yanga.

“Sasa ligi imebadilika,timu nyingi zinapambana, hivyo mashabiki wa Simba inabidi tuelewe kuwa sasa hivi kuna upinzani kwenye ligi kwani watu wamewekeza kwenye timu nyingi.Hivyo sasa inabidi tujikite kupambana hasa katika hali kama hiyo” alisema.

4. Utendaji mzima TFF.

“Utendaji wa TFF siyo makini kwani upangaji wao wa ratiba umekuwa na changamoto kubwa, haiwezekani inafikia wakati timu inakuwa nyuma kwa michezo minne dhidi ya mwenzake.

“Jambo hilo ilichangia kutumaliza kwani kuna kipindi tuliongoza ligi kwa kushinda mechi mfululizo, lakini baadaye tukapotea kutokana na ratiba mbovu ya TFF .

“Pia, TFF kutojibu malalamiko yetu sijui kwa nini,tuliwapelekea malalamiko mengi, wamekaa kimya, sijui wanataka tuamini kwa sababu viongozi wengi wa shirikisho ni wa upande wa pili (Yanga),” alidai.

Aveva alitumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa kushindwa kupata ubingwa msimu huu, akiwataka kutofanya vitendo visivyo vya kiungwana.

“Niwaombe radhi wanachama, wapenzi wa Simba kwa kutofikia malengo tuliyojipangia awali, mwanzoni mwa msimu tulisema ifikapo Mei tutakuwa mabingwa wa ligi na mabingwa wa Kombe la Shirikisho (FA).

“Hata hivyo, tunashukuru mashabiki kwa kuiunga mkono timu, tunawaomba waache vitendo visivyo vya kiunamichezo, ikiwamo kuwapiga viongozi au hata kupiga mawe basi na kuwaumiza wachezaji,” alisema rais huyo wa Simba.




ZeroDegree.
Unazijua sababu za Simba kukosa ubingwa..?? Soma hapa sababu 4 zilizotolewa na Rais wa Simba, Evance Aveva. Unazijua sababu za Simba kukosa ubingwa..?? Soma hapa sababu 4 zilizotolewa na Rais wa Simba, Evance Aveva. Reviewed by Zero Degree on 5/18/2016 10:45:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.