UJUMBE aliotaka kuufikisha Godbless Lema kwa Rais.
Godbless Lema
Hofu ya Mussa Azzan Zungu, Mwenyekiti wa Bunge kuruhusu Hotuba ya Godbless Lema, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni pamoja na maneno yaliyotumika kwenye hotuba hiyo.
Pamoja na vipengele vingine Bunge limedai kwamba, maneno yaliyotumika kwenye hotuba hiyo kuhusu tabia ya Rais John Magufuli hayafai,ifuatayo ni sehemu ya hotuba ya Lema katika kipengele hicho.
6.3 Tabia ya Rais Magufuli na Usalama wa Nchi.
Mheshimiwa Spika, wakati Taifa letu linapita kwenye changamoto nyingi kama vile ukosefu wa sukari, umeme, umaskini, mizigo kupungua bandarini, madini ya Tanzanite kuanguka bei na ubadhirifu uliokithiri katika mfumo wa utawala Rais mwenyewe ameonekana kufuatilia na kufanyia kazi habari za kwenye mitandao ya kijamii.
Rais Magufuli
Kwa tabia hii ya Rais Magufuli, kama Taifa tunahitaji maombi haraka, kwani Rais ataumiza watu wengi sana kwa kufuatilia maneno ya mitaani kwa njia mbali mbali , kwani kwa madaraka aliyonayo Rais bila shaka ataumiza watu wengi. Mfano, Sakata la Mke wa Waziri Mahiga na Trafiki barabarani,ni jambo dogo sana na la karaha kuona linazingatiwa na Rais.
Mheshimiwa Spika, haikuwa busara Rais kukemea familia ya Waziri wake mbele ya Vyombo vya Habari na kuagiza askari huyu kupandishwa cheo bila kujua historia ya utumishi wake.
Mheshimiwa Spika , kwa nini mambo haya ni muhimu kuyasema na kwani ni hatarishi kwa usalama wa nchi, tulipoanza vikao vya Kamati za Bunge, Vyombo vya Habari vilimnukuu Rais akielezea mpango wake wa kuanza kurekodi Mawaziri wake wanaolalamika juu ya staili yake ya uongozi, kwa hiyo leo ukienda kwenye Ofisi za Mawaziri, unaona hofu, mashaka, kutokujiamini, mambo yatakayopunguza ufanisi, ubunifu na uhuru katika utendaji wao, jambo linalopeleka Taifa kuzorota katika nyanja zote kwa utumishi wa umma jambo ambalo ni hatari kwa Taifa.
Source: Mtembezi
ZeroDegree.
UJUMBE aliotaka kuufikisha Godbless Lema kwa Rais.
Reviewed by Zero Degree
on
5/18/2016 10:59:00 AM
Rating: