Hizi hapa sababu za Rais John Magufuli kuzuia uagizaji sukari nje ya nchi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni, mjini
Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema sababu za Rais John Magufuli kusitisha uagizaji wa sukari kutoka nje ulitokana na uagizaji huo kuwa wa kiholela na unaovuruga viwanda vya ndani ambavyo vilianza kutishiwa na wingi wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, kulikuwa na uagizwaji wa sukari usiofuata taratibu zilizotakiwa na hivyo kutishia kwa sehemu kubwa viwanda vya ndani.
Akijibu katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu bungeni jana, Majaliwa alisema kwa sasa wameamua kuagiza sukari tani 70,000 ambayo wamejiridhisha kuwa haitaleta madhara kwa viwanda vya ndani ambavyo uzalishaji wake unategemewa kuanza Julai.
Katika swali lake, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe alitaka kujua utaratibu ambao Rais Magufuli aliutumia kuzuia uagizwaji wa sukari kutoka nje ya nchi.
Pia, Mbowe alimtaka Waziri Mkuu kulieleza Bunge ni kwanini Serikali imeshindwa kuliendeleza shamba la miwa la Bagamoyo ambalo lingeweza kusaidia kuzalisha sukari.
“Uamuzi wa kiutawala ni lazima ufanyiwe utafiti, ni kwa namna gani Serikali imeshindwa kuliendeleza shamba la Bagamoyo ambalo uanzishwaji wake ulianza tangu mwaka 2006 ambapo tungezalisha tani 120,000?” alihoji Mbowe.
Pia alihoji sababu za Serikali kuagiza tena sukari kutoka nje akitaka kujua ni kwa mamlaka ya nani na kwa utaratibu upi kwani kumekuwa na mgongano mkubwa.
Majaliwa alisema bodi ya sukari ndiyo iliyoratibu na kuagiza sukari tani 70,000 na hicho ni kiasi kinachotakiwa baada ya kufanya utafiti ikiwamo kujua mahitaji ya mfungo wa Mwezi Mtukufu. Awali, ilikuwa iagize tani 50,000 lakini ikaongeza kwa sababu hiyo.
Kuhusu upangaji wa bei elekezi, alisema Serikali ilipanga bei baada ya kukutana na wadau na kupitia ununuzi wa nje, usafiri na gharama zote ikiwamo kodi ndipo wakajua ni jinsi gani wafanyabiashara watapata faida.
Alisema itachukua zaidi ya miaka mitatu kufikia lengo linalotakiwa la kuzalisha sukari tani 420,000 ambazo ndiyo mahitaji halisi ya Watanzania badala ya tani 320,000 zinazozalishwa sasa.
Kuhusu shamba la Bagamoyo, alisema Serikali imeamua kuachana na mpango huo baada ya kushauriwa na kamati ya Bunge. Alisema shamba hilo linapakana na mbuga ya Saadan ambayo ina wanyama wanaotumia maji ya Mto Wami uliokuwa ukitegemewa katika shamba hilo, hivyo wakaona ni bora kutafuta maeneo mengine ili waache maji hayo yatumike kwa wanyama.
Katika swali jingine, Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Saumu Kheri Sakala alimtaka Waziri Mkuu kulieleza Bunge ni kwa namna gani Serikali inawasaidia wakulima wanaopunjwa mazao yao katika mauzo ya mtindo wa lumbesa.
Waziri Mkuu alisema kutumia vipimo hivyo ni kosa ambalo halitakiwi kufumbiwa macho kwani utaratibu huo unawanyima wakulima haki yao.
Alisema maeneo ya vijijini ndiko lumbesa zinakotumika zaidi kwa kuwa hakuna vipimo sahihi vya mazao. Aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kutumia kamati za ulinzi na usalama na watendaji wa kata na vijijini kuhakikisha wanapambana na wafanyabiashara hao.
ZeroDegree.
Hizi hapa sababu za Rais John Magufuli kuzuia uagizaji sukari nje ya nchi.
Reviewed by Zero Degree
on
5/20/2016 06:59:00 PM
Rating: