Hospitali ya Taifa ya Muhimbili [ MNH ], sasa yafanya upasuaji wa moyo bila mashine.
Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza kufanya upasuaji mkubwa wa kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo bila kutumia mashine.
Upasuaji huo ulioanza na wagonjwa 18 kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umeokoa zaidi ya Sh180 milioni kama wangepelekwa nje ya nchi kufanyiwa upasuaji.
Upasuaji huo mkubwa ni wa kwanza na wa aina yake kufanyika nchini na kanda ya Afrika Mashariki na Kati baada ya madaktari bingwa wa JKCI kwa kushirikiana na wa Hospitali ya BLK ya India kufanya kambi hiyo ya siku mbili kwa ajili ya kazi hiyo.
Wataalamu hao wa taasisi hizo wameweza kutoa tiba ya moyo bila kupasuliwa kwa kutumia mtambo wa Cathlab kwa kuzibua mishipa iliyoziba (BMV PROCEDURE). Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa Magonjwa ya Moyo, Dk Peter Kisenge alisema awali walikuwa wanatumia upasuaji wa kufungua vifua hali iliyowalazimu kutumia mashine kusimamisha moyo na mapafu.
Alisema wakati wa upasuaji huo, mgonjwa anaweza kutolewa mishipa ya damu miguuni au mikononi kulingana na ukubwa wa tatizo lake.
Alisema wamewafanyia upasuaji wagonjwa wanane ambao kama mgonjwa mmoja angesafirishwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu angetumia zaidi ya Sh27 milioni, lakini kwa Tanzania mgonjwa huyo ametumia Sh9 milioni.
Alisema kwa siku mbili wanatarajia kuwafanyia upasuaji zaidi ya wagonjwa 18 na kuokoa zaidi ya Sh180 milioni kama wangepelekwa nje ya nchi.
Alisema hali za wagonjwa hao zinaendelea vizuri na hakuna hata mmoja aliyepoteza maisha.
Akizungumzia aina hiyo mpya ya upasuaji, Dk Kisenge alisema njia hiyo ni nzuri na inaokoa muda tofauti na zamani.
Akizungumza na waandishi, Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu, Dk Bashir Nyangasa alisema kwa mwaka 2015, taasisi hiyo imefanya upasuaji kwa wagonjwa 471.
ZeroDegree.
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili [ MNH ], sasa yafanya upasuaji wa moyo bila mashine.
Reviewed by Zero Degree
on
5/25/2016 12:47:00 PM
Rating: