Loading...

Magari ya washawasha yaibua mvutano mkubwa Bungeni, UKAWA wadai pesa zilizotumika zingenunua ambulance kila kata.


Dodoma. Magari ya washawasha yaliyonunuliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika Uchaguzi Mkuu uliopita, jana yaliibua mvutano bungeni kati ya Serikali na Kambi ya Upinzani.



Akichangia hotuba ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo alisema Serikali ilinunua magari 777, ambayo fedha zake zingetosha kununua magari ya wagonjwa kila kata.

“Kama tuliweza kununua magari ya washawasha 777 lakini ni 50 tu yaliyotumika kwenye uchaguzi na gari moja lina gharama ya Sh150 mpaka 400 milioni. Hivi kipaumbele chetu ni nini? Bilioni 420 ambazo zimenunua magari haya zingegawanywa kwa kata 3,990 tulizonazo kila kata ingepata gari la wagonjwa na ikizingatiwa gari moja linauzwa Sh103 milioni,” aliongeza:

“Tunajiuliza kipaumbele cha nchi hii ni nini, ni afya ya Mtanzania au ni kitu gani. Magari 77 yangeweza kubaki lakini yale 700 yaliyobaki fedha zake zingetosha ambulance kila kata”

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu akisema mbunge huyo alikuwa ametoa takwimu zisizo sahihi akisema ni magari 32 tu ya washawasha yaliyonunuliwa na yalisaidia kuimarisha usalama kipindi chote cha uchaguzi.

“Hivi ninavyozungumza kuna mazungumzo yanaendelea kati Jeshi la Polisi na Zimamoto ili magari haya yaweze kutumika kwa ajili ya shughuli za kuzima moto,” alisema Masauni.

Kuhusu madai ya Lyimo kuwa magari hayo yaliligharimu Taifa Sh420 bilioni, Masauni alisema taarifa hizo si sahihi na kuomba mwongozo juu ya hatua dhidi ya mbunge huyo.

Akijibu mwongozo huo, Zungu alisema kanuni za Bunge zilitungwa na wabunge wenyewe hivyo akamtaka Lyimo ambaye wakati huo hakuwapo ukumbini, kufuta kauli yake au kuithibitisha.

“Mwongozo wangu kwa Susan Lyimo ni kuwa atakaporudi jioni aweze kufuta maneno yake au ayathibitishe ndani ya Bunge” alisema Zungu ambaye alichaguliwa kushika wadhifa huo juzi.

Katika hoja nyingine, Lyimo aliitaka Serikali kueleza zilipokwenda Sh200 milioni ambazo zilichangwa kwa ajili ya sherehe ya wabunge Novemba 20 mwaka jana ambazo Rais John Magufuli aliagiza ziende Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kununua vitanda vya wagonjwa.

Baada ya agizo hilo, siku mbili baadaye Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Lauren Bwanakunu, alikaririwa akisema ofisi yake imekabidhiwa fedha hizo na tayari vitanda 300 vimenunuliwa. Lakini jana wakati akichangia bungeni, Lyimo alisema anajua vitanda 300 vilivyopelekwa Muhimbili vilitoka sehemu nyingine hivyo kuitaka Serikali ieleze fedha za wabunge ziliko. “Tumekwenda Muhimbili ile CT-Scan ilitoka Udom. Hivi Wagogo na watu wengine hawana haki?. Tunajua hata vitanda vilitoka sehemu nyingine tunataka kujua zile fedha zilienda wapi,” alihoji.

Bima ya Afya kurekebishwa


Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Serikali itawasilisha muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Bima ya Afya ili kuongeza ulazima wa wananchi wote kujiunga na bima hiyo hasa kwa watu wote wenye uwezo wa kuchangia.

Aliwaomba wabunge kuunga mkono muswada huo pindi utakapowasilishwa bungeni.

Wizara hiyo pamoja na taasisi zake, imeomba kuidhinishiwa Sh845.1 bilioni, kati ya hizo Sh317.7 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh527.3 bilioni za miradi ya maendeleo.

Upinzani wagusia bajeti kidogo 


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imehoji hatua ya Serikali kutenga Sh65.1 bilioni za ununuzi wa dawa nchi nzima, kiasi ambacho umesema kinatosha mahitaji ya mwezi mmoja na nusu.

Msemaji wa kambi hiyo, Dk Godwin Mollel alisema kwa kukadiria, Tanzania ina watu milioni 49.8 wanaohitaji matibabu lakini kiasi hicho kinatosha kutibu watu milioni 5.6 tu kwa mwaka.

Kambi hiyo imeishauri Serikali iongeze bajeti ya dawa kutoka asilimia 11 ambayo ni Sh65.1 bilioni mpaka angalau asilimia 50 ya mahitaji ambayo ni sawa na Sh295.9 bilioni. Alisema hadi Machi, MSD ilikuwa ikidai Sh131 bilioni lakini Serikali imetenga Sh108 bilioni kulipa deni la nyuma hivyo kubakiza deni la Sh23 bilioni.

Kambi hiyo imehoji vigezo vilivyotumiwa na Serikali kununua Bajaji 400 ili zitumike kama magari ya wagonjwa, ikisema ni matumizi mabaya ya fedha za umma na ni dhihaka kwa wajawazito.

Dk Mollel alisema licha ya kwamba Bajaji hizo si rafiki kubeba wajawazito lakini nyingi zimekufa au kutelekezwa kutokana na changamoto nyingi za kijiografia.

Kuhusu vifo vya wajawazito nchini, Dk Mollel alisema kina mama 1,255 hufariki dunia kila mwezi kutokana na matatizo ya kujifungua au baada ya kujifungua ikiwa ni sawa na kina mama 42 kila siku.

“Kama ukiwakusanya hawa kina mama wanaofariki ni zaidi ya basi la abiria aina ya Toyota Coaster wanakufa kila siku. Tunataka Serikali kufanya tathmini, ije na idadi kamili ya vifo,” alisema.

Kambi hiyo imeitaka Serikali kuhakikisha inawasilisha mpango madhubuti na ulio rahisi katika kuutekeleza na kutaka suala hilo sasa lifanywe kama ajenda ya kitaifa.



Source: Mwananchi




ZeroDegree.
Magari ya washawasha yaibua mvutano mkubwa Bungeni, UKAWA wadai pesa zilizotumika zingenunua ambulance kila kata. Magari ya washawasha yaibua mvutano mkubwa Bungeni, UKAWA wadai pesa zilizotumika zingenunua ambulance kila kata. Reviewed by Zero Degree on 5/12/2016 11:31:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.