Loading...

Tani 2,500 za sukari zakamatwa Dar, mmiliki adai ni kwa ajili ya matumizi ya kiwanda.


Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Dar es Salaam. Sakata la sukari limeendelea kutikisa nchi safari hii likimgusa mfanyabiashara maarufu nchini, Gulam Dewji, ambaye jana sukari yake tani 2,500 ilikutwa kwenye ghala katika ukaguzi uliofanywa na Kamati ya Ulinzi ya Mkoa wa Dar es Salaam ambayo mwenyewe alisema aliihifadhi kwa ajili ya matumizi ya viwandani. 

Gulam alikiri kumiliki tani hizo lakini akasema sukari hiyo si kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Bidhaa hizo ziligundulika kwenye ghala la kampuni ya Mohamed Enteprises lililoko Vingunguti wilayani Ilala wakati wa ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na kamati hiyo ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutokana na agizo la Rais John Magufuli kutaka wafanyabiashara wanaoficha sukari na kusababisha upungufu uliofanya bei kupanda kusakwa.

Sukari hiyo ilizua maswali zaidi kutokana na kuonyesha kuwa inatokea nchini Brazil, lakini inafungashiwa Dubai.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Dewji alisema sukari hiyo nyeupe ni kwa ajili ya matumizi ya viwanda na si kwa matumizi ya kawaida.

Kutokana na utata huo, Makonda aliiagiza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), na Shirika la Viwango (TBS) kuanza uchunguzi wa sukari hiyo ili kubaini usalama wake na akazuia isisambazwe kwanza.

Makonda alidai kushangazwa na mifuko iliyohifadhi sukari hiyo kuonyesha kupakiwa kutoka Dubai na si Brazil.

“Ni kawaida kwa sukari kusafirishwa kwa meli kutoka Brazil na kufungashwa Dubai. Imekutwa ikiwa inasafirishwa kihalali kwa sababu vibali vyote na leseni zipo,” alisema Dewji.

Awali, kamati hiyo ilikuta kontena 115 za bidhaa hiyo kwenye bandari kavu ya PMM iliyopo eneo la Vingunguti ambako Makonda alifika na wajumbe hao asubuhi na kutaka kujua bidhaa zilizokuwapo.

Alisema uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa kwenye bandari hiyo kuna kontena 164 lakini baadaye wamiliki walidai zipo kontena 115, hali iliyomfanya kuanza upekuzi.

Mkuu wa bandari hiyo, Hosea Kakwaya aliingia katika mabishano na Makonda, akidai kuwa hajui idadi ya kontena zenye sukari katika bandari hiyo.

Hata hivyo, makontena hayo ya sukari yaliyokuwa yanasubiri kusafirisha kwenda Uganda, yalikuwa na utata wa umiliki jambo lililomlazimu Makonda kuiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kufanya uchunguzi.

Juzi, Makonda alibaini kilo 4,000 za sukari mali ya Bushir Haroun zilizokutwa eneo la Kinondoni.

Tangu Rais atangaze msako huo, wafanyabiashara kadhaa wamekamatwa kwa tuhuma za kuficha sukari, lakini baadaye wamiliki walitoa nyaraka zilizoonyesha kuwa wanamiliki kihalali.




ZeroDegree.
Tani 2,500 za sukari zakamatwa Dar, mmiliki adai ni kwa ajili ya matumizi ya kiwanda. Tani 2,500 za sukari zakamatwa Dar, mmiliki adai ni kwa ajili ya matumizi ya kiwanda. Reviewed by Zero Degree on 5/12/2016 11:21:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.