Loading...

Naibu spika azima hoja ya mbunge wa Nzega mjini, Hussein Bashe [ CCM ] kuhusu sukari.


Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amezima hoja ya Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) aliyeomba suala la kupanda bei ya sukari lijadiliwe bungeni. 



Wakati hayo yakitokea wananchi wa Mkoa wa Mbeya wameviomba vyombo vya dola kupekua malori yanayotokea Malawi, kwa madai yanabeba sukari ya magendo na kuingiza nchini.

Kutoka bungeni, Dodoma, Bashe aliomba idhini ya kiti cha Spika ya kuahirisha shughuli za Bunge kwa siku ya jana, ili kwa maslahi ya wananchi wabunge wajadili tatizo la kupanda kwa bei ya sukari.

Hata hivyo, kabla hajamalizia kuzungumza, Dk Ackson alimkatiza Bashe, akisema suala hilo lilishafanyiwa kazi Alhamisi wiki iliyopita, wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

“Mtakumbuka Waziri Mkuu Alhamisi ya wiki iliyopita, alitoa maelezo na akatoa maelekezo kuwa sukari itaruhusiwa kuingizwa nchini kwa kiasi ambacho alitaja,”alisema.

Alisema pamoja na udharura wake kwasababu ilishatolewa maelekezo, wabunge wasubiri yale maagizo ya Waziri Mkuu kuuliza kama sukari imeingia ama haijaingia na kama hajaingia lini inaingia.

Kutoka Mbeya, wananchi jijini hapa wamevitaka vyombo vya dola kuyapekua malori yanayotokea nchi jirani ya Malawi, kwa kile walichodai yanabeba sukari ya magendo na kuingiza nchini.

Wakizungumza na gazeti hili, kwa sharti la kutotajwa majina yao, walisema hivi karibuni kuna malori manane ya kampuni moja (jina tunalo) yalibeba shehena ya sukari yakitokea Malawi na yaliegesha kwenye moja ya kituo cha mafuta cha Uyole kwa lengo la kutafuta wateja.

Mkazi mwingine wa Mtaa wa Soweto, Hamphrey Lyoto alisema suala la uingizwaji wa sukari, linafanywa mchana ambapo malori yanapeleka sukari kwenye nyumba ya mfanyabiashara mmoja eneo hilo aliyejiwekea kiwanda cha kuweka sukari kwenye mifuko ya kilo moja moja na nusu kilo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Emmanuel Lukula alipoulizwa juu la suala hilo, alisema hafahamu lolote kwa kuwa ameanza kazi hivi karibuni, lakini aliahidi kulifutalia.

Kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro, wananchi wamelalamikia kitendo cha kupanda bei ya sukari, hali inayowafanya wakose uhakika wa kunywa chai na uji kwa watoto wao. Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kupanda kwa bei ya sukari katika maduka mbalimbali mjini hapa.




ZeroDegree.
Naibu spika azima hoja ya mbunge wa Nzega mjini, Hussein Bashe [ CCM ] kuhusu sukari. Naibu spika azima hoja ya mbunge wa Nzega mjini, Hussein Bashe [ CCM ] kuhusu sukari. Reviewed by Zero Degree on 5/05/2016 09:47:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.