Loading...

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, aitemea cheche Serikali...


Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye 


Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amepinga kitendo cha Bunge kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria akisema Serikali yoyote ambayo haitaki kukosolewa ni ya kidikteta.


Badala yake, alisema Serikali ya kidemokrasia inaruhusu uhuru wa watu kupata taarifa na kutoa maoni ambayo yatawasaidia viongozi katika kufanya uamuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani jana, Sumaye alinukuu ibara ya 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayosema:

“Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”

Alisema Tanzania ni nchi ya kidemokrasia kwa sababu Katiba imeainisha hivyo, lakini akaeleza kushangazwa kwake na hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuzuia matangazo ya Bunge kwa kutoa hoja dhaifu.

“Serikali imetoa hoja kwamba imesitisha matangazo ya moja kwa moja ili kubana matumizi. Wakati huohuo, wanasema wataanzisha studio ya Bunge ambayo itarusha matangazo hayo. Hapo hakuna kubana matumizi kwa sababu gharama zilizokuwa zinatumiwa na TBC zitahamia Ofisi ya Bunge.”

Alisema kitendo cha Serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ni kuvunja Katiba ya nchi na kuwanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kupata habari.

Sumaye ambaye alijiunga na Chadema wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana, alisema vikao vya Bunge vikionyeshwa moja kwa moja, wananchi watapata haki yao ya kidemokrasia, sambamba na taarifa juu ya mambo yanayowahusu.

Alisema Serikali yoyote makini ingependa mambo yake yajulikane kwa umma kwa sababu ndiyo waliyoichagua na kwamba Serikali ya kidikteta inapenda kusifiwa wakati wote na mabaya yake kufunikwa.

“Kama Serikali yetu inajiamini kwamba imechaguliwa kidemokrasia, kwa nini inaona vigumu kuweka wazi mijadala ya Bunge ili wananchi wawaone wabunge wao wanavyowawakilisha huko?” alihoji Sumaye.

Alisema ni jambo la kawaida kwa Serikali kusemwa kwa mazuri na mabaya na kwamba kujaribu kuwanyamazisha wakosoaji ni udikteta ambao utarudisha nyuma maendeleo ya Taifa na watu wake.

Alisema: “Isije ikaonekana mtu kuwa na maoni tofauti na Rais ni dhambi. Serikali ya Tanzania ni ya kidemokrasia na imewekwa na wananchi, kwa hiyo lazima ikosolewe.”

Awageukia waandishi.

Kiongozi huyo mwandamizi katika Serikali ya Awamu ya Tatu, aliwataka waandishi wa habari kuzingatia weledi katika kazi zao ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza katika jamii huku akivitaka vyombo vya habari kutoyumbishwa na nguvu za wanasiasa wala rushwa wakati wakitekeleza kazi zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Siasa Tanzania (Taporea), George Maziku alisema maadhimisho hayo yanalenga kuwakumbusha waandishi wa habari juu ya wajibu wao na kuwakumbuka waliouawa kama kielelezo cha matokeo ya kukosekana na uhuru wa vyombo vya habari.

Alisema changamoto kubwa inayoikabili tasnia ya habari ni rushwa na kusema inadumaza ukuaji wa taaluma ya uandishi kwa sababu wanazuiliwa kufanya uchunguzi kwa baadhi ya mambo.

“Zaidi ya waandishi wa habari 800 wameuawa duniani kote ndani ya miaka 10 iliyopita. Kwa hapa nchini, waandishi wawili waliuawa ndani ya miaka minne tu. Hiyo ni idadi kubwa ambayo leo inatuleta pamoja na kudai uhuru katika kazi yetu,” alisema Maziku.


Credits: Mwananchi



ZeroDegree.
Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, aitemea cheche Serikali...  Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, aitemea cheche Serikali... Reviewed by Zero Degree on 5/04/2016 12:26:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.