Michango ya harusi sasa ni balaa.
Ukumbi ukiwa umepambwa kwa ajili ya sherehe za harusi jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam/Mikoani. Unapenda kuoa, kuolewa au kuhudhuria harusi? Kama unapenda hayo, jiandae kupukutisha mifuko yako; unaweza kutumia kati ya Sh500,000 hadi 2,000,000 kuchangia harusi pekee.
Hapo bado hujalipia kodi ya pango, ada za watoto, ankara za umeme na maji na fungu la nauli ya kwenda kazini kila siku, achilia mbali wale wenye magari madogo.
Michango ya harusi imekuwa sehemu ya maisha ya Mtanzania, hasa anayeishi mjini na ni shida kuiepuka.
Wakati michango ikizidi kuwakamua wachangiaji ama kwa kupenda au kulazimika tu, matumizi katika harusi hiyo yamekuwa ‘ya kufa mtu’ kwa shughuli hiyo inayochukua takriban saa nne, nyingi huanza saa 1:00 jioni na kumalizika saa 5:00 usiku au saa 6:00 usiku.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa bajeti za harusi za kawaida kwa sasa zinaanzia Sh10 milioni na kuendelea kulingana na uwezo wa wahusika, na si ajabu kukuta nyingine zinafikia hadi Sh80 milioni, Mwananchi inaweza kukuhakishia.
Mchango kwa harusi za kawaida imewekewa kiwango cha chini. Ili uweze kwenda na mwenzi wako, utalazimika kuchangia angalau Sh100,000 wakati anayetaka kuhudhuria bila mwenza huwekewa Sh70,000.
Fedha zinazopatikana hutumika kwa ajili ya kulipia kumbi, mapambo, vinywaji, chakula, usafiri, keki, picha za video na mnato, MC na muziki na mbwembwe nyingine nyingi.
“Tanzania kuna harusi nyingi za kifahari, pengine zipo zinazozidi hata zinazofanywa nchini Uingereza, licha ya kwamba wenzetu kule wapo juu kiuchumi, na pia gharama hubebwa na familia na wageni waalikwa huwa wachache kulingana na uwezo walionao. Sasa huku hata kiwango cha michango ni kikubwa,” alisema mwanasaikolojia Rabikira Mushi alipoulizwa na Mwananchi maoni yake kuhusu suala hilo.
Hata hivyo, wanasaikolojia na sosholojia wanasema michango haikwepeki katika tamaduni za Kitanzania.
Watu wengi waliohojiwa na Mwananchi walisema wanachangia harusi kuanzia Sh500,000 hadi Sh2 milioni kwa mwaka, na wengine hufikia hata Sh9 milioni.
Saida Hassan, mkazi wa mjini Geita alisema kwa mwaka anachangia zaidi ya Sh9 milioni kwenye harusi na sherehe za zawadi kwa bibi harusi (kitchen part) na hiyo inatokana na nafasi aliyonayo kwenye jamii.
“Nafanya kazi ya kupiga picha za video kwenye harusi, hivyo napata kadi tano hadi sita kwa mwezi na zote lazima nichangie,” anasema.
Saida anasema kuna miezi ambayo harusi huwa nyingi na kuna miezi mingine harusi huwa chache, hivyo wingi wa kadi unategemea na kipindi.
“Kwa mfano mwezi huu nimepata kadi sita za harusi na mbili za kitchen part. Kati ya hizo, kadi moja ya harusi nimechanga Sh200,000 na nyingine nimechanga Sh100,000, hivyo mwezi huu pekee nimechangia Sh700,000, hiyo ni harusi pekee,” anabainisha.
Anasema kwa upande wa kichen part, amechangia Sh100,000 kwa maana alipata kadi mbili na kila moja amechangia Sh50,000. Jumla ni Sh800,000 kwa mwezi Mei pekee.
Anasema kwa Juni tayari ana kadi mbili.
Ally Chirukile, ambaye ni dakatri wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Kairuki, jijini Dar es Salaam, anasema mara nyingi anachangia watu muhimu kwake na kwa mwezi Mei amechangia kadi mbili za harusi kwa Sh100,000 kila moja, hivyo Sh200,000 zimeondoka.
“Unaweza kupata hadi kadi 10, lakini nilishajiwekea malengo, nachangia mbili au tatu za muhimu tu,” anasema.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Jane Martine aliguna kwanza na kucheka.
“Kwa kweli mpaka (kadi) nyingine nazikimbia. Nahisi zinafika 20, maana napata kadi nyingi na si kwamba nachangia zote, nachagua zilizo muhimu,” alisema.
“Kwa mwezi huu (Mei) nimechangia kadi sita kwa Sh100, 000 kila moja. Niseme mwezi huu nimetumia Sh600,000 na bado nina kadi nyingine mbili za Juni na zenyewe natakiwa kuchanga Sh100, 000 kila moja.”
Jane anasema kuna wakati kadi zinafululiza na unaweza kujikuta mshahara wako wote unaishia kwenye michango ya harusi.
Lakini, Faida Muyomba wa Geita anaonekana tofauti kwa kuwa huwa hachangii kabisa harusi.
“Niliacha zamani sana kuchangia harusi baada ya kuona nafirisika, huwa naletewa kadi naishia kuzipokea na kuzitupa,” anasema.
Wakati Faida akisema hayo, Hassan Amri, mkazi wa Tandika, Dar es Salaam anasema kwa mwezi anapata kadi tatu au nne, na kwa Mei alipata kadi tatu na amechangia Sh50,000 kila moja.
“Niseme mwezi huu nimechangia Sh150,000 na nikisema kwa mwaka wastani nachangia kama Sh2 milioni,” anasema.
Kwa upande wake, Frank Fungo ana msimamo kama wa Muyomba.
“Nachangia shughuli za maendeleo kama vile kusomesha watoto au mtu ana mradi wake anahitaji kusaidiwa,” anasema na kuongeza:
“Watanzania wengi bado tumelala. Huwezi ukachangia fedha kila siku kwa ajili ya starehe ya mtu wakati wewe hunufaiki na chochote. Hiyo nilishaikataa mimi.”
Si wote wenye msimamo kama huo Ada Odhuno, muuguzi wa Hospitali ya Kairuki anasema analazimika kuchangia ili atakapopata shughuli kama hiyo, pengine ya mtoto wake, naye achangiwe.
“Ujue dada hali ya maisha ya sasa inabadilika, tunakoelekea maisha yatakuwa magumu hasa kwa vizazi vyetu vipya, michango ya harusi imewekewa viwango, ukiwa peke yako unachangia kidogo ukiwa na mwenza unachangia kikubwa,” anasema.
Anasema kwa mwezi anapokea kadi mbili hadi tano na kuna miezi kama January hadi Machi kadi huwa nyingi na Septemba hadi Novemba pia unajikuta kwa mwezi unakuwa na kadi kumi au zaidi.
Mambo yanayoongeza gharama
Timu ya Mwananchi Jumapili ilitembelea kumbi nyingi maarufu jijini Dar es Salaam ambako harusi hufanyika na kubaini kwamba gharama zake ni kubwa.
“Aise! Nilishika kichwa pale niliambiwa gharama ya ukumbi kwa harusi ni Sh7 milioni hadi Sh10 milioni,” anasema mwandishi wetu aliyekwenda ukumbi wa Diamond Jubilee kuulizia gharama.
Cha kushangaza, pamoja na gharama hizo kumbi nyingi zimeshajaa kwa hadi miezi mitatu ijayo kutokana na wanaharusi kulipia mapema kuhofia hali ya hapo baadaye.
“Hapa kumbi kwanza ni gharama kwa sababu watu wengi wanakuja kufanyia hapa harusi. Hivi ninavyongea kila siku kuna harusi,” anasema mmoja wa wafanyakazi wa ukumbi huo huku akikataa jina lake lisitajwe kwa kuwa si msemaji.
“Watu wameweka oda ya kumbi mpaka Desemba, kwa miezi hii hakuna nafasi kabisa hasa Jumamosi na Jumapili. Labda mtu akitaka afanye siku za kawaida na zenyewe ni kubahatisha,” anasema mfanyakazi huyo wa Diamond Jubilee ambao pia hutumika kwa shu burudani na maonyesho ya biashara.
Mkurugenzi wa ukumbi wa Lulu uliopo Sinza jijini Dar es Salaam, Rebeca Maganga anasema gharama za ukumbi ni Sh1 milioni hadi Sh2 milioni na bei inapanda kulingana na mahitaji ya watu.
“Mwezi wa sita wote hadi Oktoba umeshabukiwa (umeshalipiwa). Hakuna nafasi, labda kuanzia Novemba. Kila wiki tunakuwa na harusi tano hadi sita, hasa miezi miezi ya Juni hadi Oktoba na Aprili hadi Juni,” anasema.
Unaweza kuepuka michango?
Wakati uchangiaji kwa ajili ya sherehe ukizidi kupamba moto, wataalamu wanasema mwako ni mkubwa kwa kuwa wachangaji hutegemea kitu kutoka kwenye sherehe hizo.
Mwanasaikolojia Rabikira Mushi anasema kuna mwamko mkubwa kwa jamii, hasa watu waishio mjini, katika kutoa michango ya sherehe za aina mbalimbali ikiwamo za harusi. “Kumekuwa na ushirikishaji wa familia, ndugu wengine wa karibu na marafiki katika kuchangishana michango na wengi wamekuwa wakijitoa kuchangia zaidi sherehe kuliko ugonjwa, msiba au sherehe,” anasema.
Anesema mwitikio wa kuchangia sherehe kuliko mambo mengine, unaweza kuwa unachochewa na matarajio ya wachangiaji hao ambao hutegemea kula vyakula vinono na vinywaji wavipendavyo na kupata burudani katika sherehe hizo.
“Hali huwa tofauti katika michango ya ugonjwa au elimu, kuna ndugu na jamaa ambao hukwepa wakiamini kwamba hilo ni jambo la binafsi ambalo mtu au familia inatakiwa kulibeba,” anasema Mushi.
Anasema anadhani jamii inatakiwa kubadilisha mfumo wa maisha kwa kuhakikisha sehemu kubwa ya mapato yanayotokana na michango hiyo inatumika katika kuwajengea wanandoa msingi mzuri wa kiuchumi wanapoanzisha familia yao.
“Tanzania kuna harusi nyingi za kifahari, pengine zipo zinazozidi hata zinazofanywa nchini Uingereza, licha ya kwamba wenzetu kule wapo juu kiuchumi, na pia gharama hubebwa na familia na wageni waalikwa huwa wachache kulingana na uwezo walionao. Sasa huku hata kiwango cha michango ni kikubwa,” anasema.
Source:Mwananchi
ZeroDegree.
Michango ya harusi sasa ni balaa.
Reviewed by Zero Degree
on
6/05/2016 12:47:00 PM
Rating: