Loading...

Mikataba ya wapangaji kuambatana na picha ya mpangaji husika.


Mtiririko wa mauaji na vitendo vya uhalifu umeanza kudhibitiwa kupitia wapangaji na wenye nyumba ambao sasa wanalazimika kuingia mikataba itakayoambatana na picha ya mpangaji.



Mei 18, mwaka huu askari wa usalama barabarani, Ally Kinyogoli aliuawa na watu waliokuwa wameziba nyuso ambao walimfyatulia risasi.

Mei 26, dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth aliuawa kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake eneo la Kibada, Kigamboni ambako inaelezwa kuwa wauaji hao hawakuchukua kitu chochote ndani ya nyumba yake. 

Kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewataka wenye nyumba wanapotengeneza mikataba waweke picha za wapangaji wao na nakala zipelekwe kwenye ofisi za Serikali za mitaa kwa ajili ya usalama.

Hatua hiyo imekuja baada ya jeshi hilo kubaini kuwa kila linapokwenda kuwakamata watuhumiwa wanakoishi linakosa taarifa kamili kutoka kwa wenye nyumba wao.

Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro alisema jana kuwa utafiti wao umeonyesha wanapowafuatilia watuhumiwa, wengi wao huwa wamechukua chumba kimoja ambacho hukaa miezi miwili hadi mitatu na baadaye wanahamia kwenye nyumba nyingine.

Sirro aliwatahadhalisha wenye nyumba ambao hawatafuata utaratibu huo watachukuliwa hatua za kisheria.

“Ninawaomba viongozi wa Serikali za mitaa kutoa elimu hiyo kwa wenye nyumba itasaidia kuwatambua wakazi wote na watawabaini waharifu,” alisema.

Kamanda huyo alisema mtiririko wa matukio ya uhalifu unaonekana kuwa huanzia katika makazi ya wahusika, hivyo udhibiti wa vitendo hivyo unapaswa uanzie katika maeneo hayo.



Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Mikataba ya wapangaji kuambatana na picha ya mpangaji husika. Mikataba ya wapangaji kuambatana na picha ya mpangaji husika. Reviewed by Zero Degree on 6/25/2016 12:17:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.