Loading...

Sheria ya kuanzishwa MAHAKAMA YA MAFISADI yapitishwa Bungeni.


BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana lilipitisha kwa kauli moja Sheria ya Marekebisho Mbalimbali, ambayo pamoja na mambo mengine, yamempa Jaji Mkuu mamlaka ya kuanzisha Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ya Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa muswada huo uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, adhabu kwa watakaokutwa na hatia zimeongezwa, huku mahakama hiyo ikiwekewa mazingira wezeshi ili iendeshe kesi hizo kwa haraka.



Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.

Mazingira wezeshi Muswada huo wa sheria ambao kwa sasa utakuwa ukisubiri Rais ausaini ili iwe sheria kamili, umekusudia kuanzisha divisheni hiyo ya mahakama, ambayo itakuwa na majaji wake na watumishi wake wanaojitegemea.

“Divisheni Maalumu ya Mahakama Kuu, itakuwa na majaji pamoja na watumishi wengine, ambao wanahusika moja kwa moja na kesi za rushwa na uhujumu uchumi tu. “Hatua hii itawezesha kesi za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi kusikilizwa kwa urahisi, ufanisi na kwa haraka,” alisema Masaju wakati alipokuwa akisoma muswada huo kabla ya kupitishwa na Bunge.

Hatua hiyo ya kuwa na majaji maalumu na wafanyakazi wake, Masaju alisema imelenga kuondoa udhaifu uliojitokeza wakati wa kushughulikia kesi za rushwa na uhujumu uchumi, kwa kuwa majaji waliokuwa wakisikiliza mashauri hayo, walikuwa hao hao wanaosikiliza mashauri mengine ya jinai, madai, katiba na mengine yanayofunguliwa Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa Masaju, hali hiyo ilisababisha uendeshaji wa kesi za rushwa na uhujumu uchumi, kutokuwa na tofauti na uendeshaji na usikilizwaji wa kesi zingine. Mazingira mengine wezeshi yanayotengenezwa na sheria hiyo kwa divisheni hiyo, ni thamani ya fedha inayohusishwa na makosa hayo, kuwa inaanzia Sh bilioni moja.

“Inapendekezwa kuwa pale makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yanapohusisha thamani ya fedha, basi makosa yatakayofunguliwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, yawe ni yale ambayo thamani yake haipungui Sh bilioni moja,” alisema Masaju.


ZeroDegree.
Sheria ya kuanzishwa MAHAKAMA YA MAFISADI yapitishwa Bungeni. Sheria ya kuanzishwa MAHAKAMA YA MAFISADI yapitishwa Bungeni. Reviewed by Zero Degree on 6/25/2016 12:01:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.