Loading...

Watumishi waliochanganya maiti Hospitali ya Taifa Muhimbili [ MNH ], watumbuliwa.


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha.

Dar es Salaam. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi, Dk Praxeda Ogweyo ili kupisha uchunguzi dhidi yake kutokana na kushindwa kusimamia vizuri wafanyakazi walioko chini yake na kusababisha kuchanganya maiti.

Pia, Profesa Museru ametengua uteuzi wa Mkuu wa Kitengo cha kuhifadhi maiti, Dk Innocent Mosha na kuwaondoa katika chumba cha maiti wahudumu waliohusika katika matukio hayo kuanzia jana ili kupisha uchunguzi.

Katika taarifa yake kwa umma jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa hospitali hiyo, Aminiel Aligaesha alisema utenguzi wa Dk Ogweyo umetokana na kushidwa kusimamia vizuri wafanyakazi walioko chini yake na kusababisha kitengo cha kuhifadhi maiti cha MNH kuzichanganya wakati wa kuzitoa kwa ndugu.

Alisema jambo hilo limejitokeza mara mbili kwa kipindi kisichozidi miezi mitatu, ambapo maiti zilichanganywa wakati wa kuzitoa kwa ndugu hali iliyosababisha usumbufu kwa wafiwa na hospitali pia.

Itakumbukwa kuwa Aprili 9, mwaka huu tukio kama hilo lilitokea na kusababisha usumbufu kwa ndugu.

“Tukio hilo limejitokeza tena Juni 20, 2016.”

“Katika uchunguzi huu, kamati maalumu, imeundwa kuchunguza kwa kina utendaji wa kitengo cha kuhifadhi maiti ili kutoa mapendekezo ya jinsi ya kurekebisha utendaji wa kitengo hicho ili matukio kama haya yasijitokeze tena,”alisema Aligaesha.

Kutokana na utenguzi huo, Profesa Museru amemteua Mkuu wa Idara ya Radiolojia, Dk Flora Lwakatare kukaimu nafasi hiyo na Dk Herbert Nguvumali kukaimu nafasi, mkuu wa kitengo cha kuhifadhi maiti.

Aligaesha alisema kurugenzi ya tiba shirikishi inasimamia Idara ya mionzi na Idara ya maabara kitengo cha kuhifadhi maiti kipo chini ya maabara.

Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Watumishi waliochanganya maiti Hospitali ya Taifa Muhimbili [ MNH ], watumbuliwa. Watumishi waliochanganya maiti Hospitali ya Taifa Muhimbili [ MNH ], watumbuliwa. Reviewed by Zero Degree on 6/24/2016 11:59:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.