Loading...

Mikoa mitano yaongoza kwa umaskini Tanzania.


Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amewasilisha bungeni Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa Fedha wa 2016/17, huku akitaja mikoa mitano inayoongoza kwa umaskini nchini.

Dk Mpango alisema mikoa hiyo imebainika katika Tathimini ya Hali ya Umaskini kimaeneo iliyofanyika kwa kutumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 na utafiti wa Hali ya Kipato na Matumizi katika kaya ya mwaka 2012.

Aliitaja mikoa hiyo na asilimia ya umaskini kwenye mabano Kigoma (48.9), Geita (43.7), Kagera (39.3), Singida (38.2) na Mwanza (35.3).

Kwa upande wa wilaya umaskini mkubwa upo katika Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma na Biharamulo mkoani Kagera na takribani asilimia 60 ya watu wapo chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya kimsingi.

“Hii ina maana kuwa maeneo ya vijijini hususan pembezoni bado Watanzania wengi wanaishi kwenye umaskini na uwezo wao wa kupata mahitaji ya msingi mdogo,” alisema.

Dk Mpango aliitaja mikoa mitano yenye ahueni ya umaskini wa kipato kuwa ni Dar es Salaam (5.2), Kilimanjaro (14.3), Arusha (14.7), Pwani (14.7) na Manyara (18.3).

Pia, Dk Mpango alisema utafiti wa Hali ya Afya ya Mama na Mtoto, uliofanyika mwaka 2015 unaonyesha idadi ya wasichana waliopata watoto katika umri wa miaka 15 hadi 19 imeongezeka na kufikia asilimia 27 mwaka 2015 kutoka asilimia 23 mwaka 2010.

“Kuongezeka kwa wasichana wanaopata watoto wakiwa na umri mdogo, yaani miaka 15 hadi 19 siyo dalili nzuri kwani inaashiria kuongezeka kwa utegemezi na kudumaza jitihada za kuondoa umaskini katika jamii,” alisema.

Kuhusu wastani wa pato la kila mtu, Dk Mpango alisema pato la wastani la mtu limepungua kutoka Dola 1,047 za Marekani kwa mwaka 2014 hadi Dola 966.5 mwaka 2015.

Alisema hali hiyo imetokana na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania. “Hivyo ni dhahiri kuwa bado kunahitajika msukumo zaidi wa kuongeza ukuaji wa Pato la Taifa ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya kufikia Dola 3,000 za Marekani kwa pato la kila mtu na kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025,” alisema.

Kuhusu urahisi wa kibiashara, Dk Mipango alisema taarifa ya urahisi wa kufanya biashara ya Benki ya Dunia (WB) ya mwaka 2015 , Tanzania ilipanda kwa nafasi moja katika vigezo vya urahisi wa kufanya biashara kwa kushika nafasi ya 139 kati ya nchi 189 duniani ikilinganishwa na nafasi ya 140 mwaka 2014. Alisema mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imetenga Sh11.8 trilioni sawa na asilimia 40 ya bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Source: Mwananchi
Mwananchi
Mikoa mitano yaongoza kwa umaskini Tanzania. Mikoa mitano yaongoza kwa umaskini  Tanzania. Reviewed by Zero Degree on 6/09/2016 05:14:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.