Kodi zote Nchini kukusanywa na Mamalaka ya mapato Tanzania [ TRA ].
Dar es Salaam. Serikali imetangaza mabadiliko makubwa yanayolenga kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kikodi baada ya kuikabidhi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), rungu la kukusanya kodi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kutokusanywa ipasavyo.
Uamuzi huo mpya unazivua mamlaka zilizokuwa zikikusanya mapato hayo ambazo ni Wizara, idara na halmashauri.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alieleza hayo jana wakati akisoma mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2016/17.
Alisema kuwa TRA itakusanya mapato hayo kuanzia Julai Mosi, ikiwamo kodi ya majengo.
Alisema hatua hiyo imefanywa kutokana na TRA kuwa na uzoefu na mifumo mizuri ya ukusanyaji wa mapato waliyonayo nchi nzima na mafanikio yaliyopatikana kutoka nchi za Rwanda na Ethiopia zinazotumia mfumo huo.
“Miongoni mwa makusanyo yanayolengwa ni pamoja na tozo, faini kama vile za mahakama na usalama barabarani, ada, viingilio kwenye hifadhi za Taifa na viwanja vya michezo pamoja na vibali vya kuvuna maliasili,” alisema.
Mbali na uamuzi huo, Serikali pia imeendelea kupunguza zaidi misamaha ya kodi ili kuondoa matumizi mabaya ya misamaha hiyo ambayo imechochea Serikali kutokusanya ipasavyo mapato hayo.
Katika hatua hiyo, Dk Mpango alisema watafanya mabadiliko ya kisheria yatakayojumuishwa ambayo yanaikosesha mapato na kutangaza kufanyia mabadiliko ya sheria itakayowasilishwa hivi karibuni ndani ya Muswada wa Fedha wa mwaka 2016.
Alisema mambo hayo pamoja na mengine, yamelenga kuwataka wanufaikaji wa misamaha hiyo ambao wengi huwa ni taasisi za dini na asasi za kiraia kulipa kodi kwa bidhaa watakazoagiza na baadaye kuwasilisha maombi ya kurejeshewa kodi hiyo baada ya uhakiki kufanyika.
Pia, Dk Mpango alisema Serikali imefuta utaratibu wa kubakiza maduhuli katika taasisi zake uliokuwa umelenga kuwasaidia kifedha kwa mujibu wa mafungu yao, kwa kuwa umekuwa ukipunguza mapato kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Uamuzi wa kufuta utaratibu huo, alisema unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015 kifungu 58 (a) mpaka (c) na baada ya tathmini iliyofanyika kubaini taasisi zinazohusika na utaratibu huo kujikita zaidi kukusanya maduhuli badala ya kufanya majukumu yao ya kutoa huduma kwa wananchi, kama Wakala wa Misitu na Kitengo cha Usalama Barabarani.
Alisema taasisi hizo pia zimekuwa zikipata fedha nyingi na kuonekana kujinufaisha zaidi wakati wizara, idara, na taasisi nyingine zikilia na ukata.
“Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sababu hizo, kuanzia sasa mapato yote yatakusanywa na kuwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali na kila fungu litatolewa kutokana na bajeti yake,” alisema Mpango.
ZeroDegree.
Kodi zote Nchini kukusanywa na Mamalaka ya mapato Tanzania [ TRA ].
Reviewed by Zero Degree
on
6/09/2016 05:19:00 PM
Rating: