Mkwasa adai Samatta aliwanyima ushindi.
KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Charles Mkwasa alisema penalti waliyokosa katika mchezo dhidi ya Mafarao wa Misri ilipoteza mwelekeo wa timu hiyo kufanya vizuri.
Alisema pia, Misri walistahili kushinda kutokana na uwezo mkubwa waliouonesha katika safu zao zote lakini pia, walionekana kucheza mpira kwa nidhamu na ufundi mkubwa. Katika mchezo huo uliochezwa juzi, Taifa Stars iliaga rasmi mbio za kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kipigo cha mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2017) zitafanyika Gabon mwakani na Misri imefuzu kutoka katika kundi hilo la G.
Mkwasa amesema baada ya Mbwana Samatta kukosa penalti waliyopata kipindi cha pili cha mchezo huo, timu ilipoteza mwelekeo na kuipa nafasi Misri kucheza kwa kujiamini na kufanikiwa kupata bao la pili.
Taifa Stars ilipata penalti dakika 53 baada ya Himid Mao kuchezewa rafu ndani ya eneo la hatari na Amr Mohsen aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mohamed Ibrahim.
“Tulivyopanga imekuwa tofauti, timu ilikwenda vizuri mwanzoni lakini baadaye ikapoteza nafasi kidogo, wenzetu walicheza vizuri kwa nidhamu na walikuwa na nguvu na tatizo letu tulitoka zaidi baada ya kupoteza penalti, kisaikolojia iliwasaidia wenzetu kupambana zaidi na kupata bao la pili,” alisema.
ZeroDegree.
Mkwasa adai Samatta aliwanyima ushindi.
Reviewed by Zero Degree
on
6/06/2016 10:38:00 AM
Rating: