Loading...

Baraza la Vijana CHADEMA walianzisha tena Dodoma.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema Taifa (Bavicha) , Patrobas Katambi akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Msemaji wa baraza hilo Edward Simbeye. Picha na Said Khamis

Dar/Dodoma. Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kusitisha mpango wa vijana wa chama hicho kwenda Dodoma “kuisaidia polisi kuzuia” Mkutano wa Mkuu wa CCM, Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), limeibuka tena safari hii likitangaza kufanya kikao cha kamati yake ya utendaji mjini humo siku tatu zijazo.

Mkakati huo uliotangazwa jana unaonekana wazi kutaka kujibu mapigo kwa CCM na kupima kauli za Jeshi la Polisi lililosema halikupiga marufuku mikutano ya ndani huku wadadisi wa masuala ya kisiasa wakisema huenda ukaibua sintofahamu iwapo watazuiwa na polisi.

Wakati Bavicha wakitangaza kufanya mkutano huo Julai 20, siku tatu kabla ya mkutano huo wa CCM, ambao mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete atakabidhi kijiti kwa Rais John Magufuli, jeshi la polisi mkoani Dodoma limesema halijapokea taarifa kutoka kwa vijana hao, lakini hata likipokea, hautafanyika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema: “Hawatafanya kwa sababu huo ni mwendelezo wa vurugu zao. Lakini sisi hatufanyi kazi kwa magazeti. Hatujapokea taarifa ya kufanyika kwa mkutano huo.”

Julai 10, mwaka huu Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alisitisha mpango wa Bavicha, kwenda Dodoma akihofia maafa ambayo yangeweza kutokea, badala yake alisema watasaka haki yao kwa kufanya mikutano ya ndani na kuchukua hatua katika mahakama za ndani na nje ya nchi.

Msimamo mpya

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi alisema mkutano huo wa kamati ya utendaji utafanyika Julai 20, Dodoma na utahudhuriwa na Mbowe na kwamba tayari wameshatoa taarifa kwenye mamlaka husika.

“Polisi imepiga marufuku mikutano ya hadhara, siyo ya ndani. Sidhani kama kikao hiki watakizuia kwa sababu ni cha ndani,” alisema Katambi.

Alisema kikao hicho, kitajadili na kutoa mwelekeo wa masuala mbalimbali ikiwamo mkakati wao mpya wa kutafuta haki na demokrasia aliyodai inaminywa.

Alisema mpango wa awali wa kutafuta haki haukushindwa, bali waliheshimu mawazo na kauli ya Mbowe ya kusitisha mpango huo, lakini safari hii Bavicha imejipanga kivingine kusaka haki hiyo.

“Kikao hiki kitatupa majibu ni mbinu gani tutaitumia, ndiyo maana tumemshirikisha Mbowe. Zipo mbinu nyingi tu ikiwezekana hata kutuma umati wa nyuki uvuruge mkutano wa CCM,” alisema Katambi.

Hata hivyo, Katambi hakuwa tayari kueleza kwa undani mpango wao mpya wa kile alichokiita “kusaka haki na demokrasia kwa vyama vya upinzani” badala yake alisisitiza kikao hicho ndicho kitatoa majibu.

Ombi kwa IGP Mangu

Katambi amemwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu kujitokeza hadharani na kuueleza umma kuhusu kauli kinzani zinazotolewa na jeshi hilo kuhusu mikutano ya vyama vya siasa.

“Mangu aseme ukweli juu ya kauli hizi ambazo tunaziona zinaipendelea CCM. Kama akishindwa ajiuzulu wadhifa wake,” alisema Katambi.

Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita alisema kikao hicho, hakina nia ya kuvuruga mkutano wa CCM kwa sababu ni kikao cha amani na kitafuata taratibu zote.

Viongozi wanne wa Bavicha, wakiwamo Katambi na Mwita wapo nje kwa dhamana baada ya hivi karibuni kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa mashtaka ya kukutwa na maandishi ya uchochezi.


Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Baraza la Vijana CHADEMA walianzisha tena Dodoma. Baraza la Vijana CHADEMA walianzisha tena Dodoma. Reviewed by Zero Degree on 7/17/2016 12:05:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.