Loading...

Chadema yatangaza vita na polisi Sept 1

KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeamua Septemba Mosi, mwaka huu, kuwa siku ya maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima, kama moja ya maazimio yake.

Hatua hiyo ya Chadema imechukuliwa kukiwa bado na zuio la kufanyika shughuli za kisiasa hadharani mpaka mwaka 2020.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitoa tangazo hilo jana wakati akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu iliyokutana kwa dharura jijini Dar es Salaam Jumamosi na Jumapili iliyopita, ambayo iliunda kamati ndogo ndogo zilizokutana kwenye vikao vya ndani Jumatatu na juzi kabla ya kufikia uamuzi huo.

Alisema kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu imeziagiza ngazi zote za chama kuanzia Msingi, Kata, Majimbo, Wilaya, Mikoa, Kanda, Mabaraza na Taifa, kukaa vikao vyake vya kikatiba mara moja.

“Tumeelekeza vikao hivyo kuongozwa na ajenda ya kujadili hali ya siasa, hali ya uchumi na maandalizi ya mikutano ya hadhara ya Septemba mosi, nchi nzima," alisema Mbowe.

Aliongeza kuwa: "Tunatarajia ushirikiano wa kutosha kutoka kwa vyombo vya dola katika kutekeleza dhamira yetu ya maandamano na mikutano nchi nzima.”

Alisema chama hicho kinafanya mikutano na maandamano hayo kupaza sauti dhidi ya kinachofanywa na Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, walioamua kuiweka demokrasia kuzuizini.

Akizindua Mpango wa Pili wa Maboresho wa Jeshi la Polisi kwenye viwanja vya Biafra, jijini Dar es salaam Juni 25 Rais John Magufuli alivitaka vyama vya siasa kujikita katika kutekeleza ahadi za kimaendeleo na kuachana na mikutano ya hadhara ya kila mara nchini hadi 2020.

Mwaka 2020 ndipo patafanyika Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani baada ya Rais Magufuli kuibuka kidedea kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi Oktoba 25, mwaka jana.

Kutokana na kauli hiyo ya Rais na taarifa zilizoelezwa na Polisi kuptikana kiintelejensia, jeshi hilo limekataza mikutano ya hadhara mpaka hali itakaposomeka vinginevyo.

Makamanda wa Polisi wa wilaya na mikoa kadhaa, ikiwemo Kahama na Mwanza wameikatalia Chadema kufanya mikutano kwa sababu hiyo ya kiitelejensia.

Lakini Mbowe alisema kwa sasa wako tayari kwa lolote, na kutaja azimio jingine kuwa ni kufungua kesi ndani na nje ya nchi juu ya uendeshwaji wa serikali kwa kutumia kauli ya mtu mmoja badala ya kufuata sheria.

Pia, Mbowe alisema Chadema imeunda kamati maalumu ya kuratibu na vingozi wake wako tayari kukamatwa na kuhojiwa na vyombo vya dola kutokana na tamko hilo.

Akifafanua tamko hilo, Mbowe alisema lengo ni kupaza sauti kupinga uendeshaji wa nchi kwa kauli za viongozi pasipokufuata utawala wa sheria.

Alifafanua kuwa kamati kuu imeagiza ngazi zote za chama kuanzia ngazi ya msingi, kata, majimbo, wilaya, mikoa, kanda, mabaraza na taifa kukaa vikao vya kikatiba kwa ajenda ni kujadili hali ya siasa, uchumi na maandalizi ya mikutano ya hadhara.

“Ni wazi sasa kuna tishio kubwa dhidi ya ukuaji wa demokrasia nchini kutoka kwa viongozi wa serikali kukandamiza demokrasia na madhara ya kukandamizwa yameshaanza kulitafuna taifa,” alisema Mbowe.

KAMANDA WA OPERESHENI


Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Polisi, Nsato Marijani, alipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia tamko hilo la Chadema, alisema hajapata taarifa hiyo na kwamba akishaipata atajua cha kufanya.

“Tutaangalia kwa makini na kuona kama hiyo oparesheni yao itakuwa na madhara ama laa kwa sababu tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria," alisema Marijani.

"Kama Chadema wakifuata sheria na sisi tukajiridhisha kwamba haitaathiri usalama, tutawaacha waendelee.” alisema.
Alisema jeshi hilo lina uwezo wa kupambana na kiashiria chochote cha uvunjifu wa usalama wa nchi na kwamba sheria ziko wazi juu ya suala hilo.

Mbowe alisema: “Kama raia wema, tuna wajibu na haki ya kulinda na kuitetea Katiba ya nchi kuhakikisha kuwa haivunjwi na yeyote.”

Mbowe pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni, alijibu maswali ya waandishi wa habari kwa kusisitiza msimamo wao na kutokuwa waoga dhidi ya mkono wa dola.

Mkutano huo ulijumuisha wajumbe wengi wa Kamati Kuu, akiwamo aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa) aliyeshindwa na Rais Magufuli, Edward Lowassa.


Source: IPPMedia
ZeroDegree.
Chadema yatangaza vita na polisi Sept 1 Chadema yatangaza vita na polisi Sept 1 Reviewed by Zero Degree on 7/28/2016 10:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.