Loading...

Dabi kali 6 msimu ujao wa ligi kuu ya vodacom.

MCHAKAMCHAKA wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu mpya wa 2016/17 utaanza Agosti 20.

Hii ni baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa ratiba ya mzunguko wa kwanza.

Ingawa ratiba hiyo inazishirikisha timu zote 16 za Ligi Kuu, lakini kuna baadhi ya mechi ambazo zina mvuto zaidi na kusubiriwa na mashabiki wengi wa soka nchini.

Zifuatazo ni mechi sita za mzunguko wa kwanza ambazo zinatarajia kutazamwa zaidi kwa kuvutia mashabiki wengi nchini.

1. Mwadui FC vs Stand United


Hii ni dabi ya mji wa Shinyanga. Ni moja ya mechi itakayokuwa na mvuto wa aina yake mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu ujao.

Itachezwa Septemba 9 ikiwa ni ya raundi ya nne.

Mashabiki wa mji wa Shinyanga na vitongoji vyake watamiminika kwenye Uwanja wa Mwadui, huku watakaobaki kwenye televisheni watataka kuangalia kama Stand inaweza kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 2-0 mechi ya mzunguko kwa kwanza, pia kipigo cha mabao 2-1 mzunguko wa pili.

2. Azam FC vs Simba

Ni moja kati ya mechi kubwa na yenye mvuto kwa sasa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania zinapocheza timu hizo.

Itakuwa ni mechi ya raundi ya tano itakayochezwa Septemba 17 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zilitoka sare kwenye mechi zote mbili za msimu uliopita wa mabao 2-2 na 1-1 mzunguko uliofuata.

3. Mbeya City vs Prisons

Mechi ya raundi ya tano itakayopigwa Septemba 17 kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya. Ni mechi ya 'dabi' ya Mbeya inayovutia mashabiki wengi kwenye mji huo na vitongoji vyake ambao humiminika kwa wingi kila zinapokutana.

Mbeya City itakuwa inajaribu kufuta uteja wa msimu uliopita ilipochapwa bao 1-0 mzunguko wa kwanza kabla ya kutoka sare mzunguko wa pili.

4. Yanga vs Simba

Dabi Kuu Tanzania itapigwa Oktoba Mosi, wakati mahasimu wawili Simba na Yanga zitakapokutana uso kwa uso kwenye Uwanja wa Taifa ikiwa ni mechi ya raundi ya saba.

Ni mechi inayosimamisha nchi kwa dakika zote 90, ambazo timu hizo zinakuwa uwanjani.

Mechi ya msimu huu inatajiwa kuwa upinzani zaidi, kwani Simba itakata kufuta uteja wa kuchapwa mabao 2-0 kwenye mizunguko yote miwili ya msimu uliopita.

5. Toto African vs Mbao FC

Ni dabi mpya wa mji wa Mwanza. Baada ya kuondoka ile ya Coastal Union na African Sport zote za Tanga, ambazo zimeshuka daraja, badala yake msimu ujao itakuwa ya Mbao na Toto.

Toto iliyonusurika kushuka daraja msimu uliomalizika itakapambana na Mbao Oktoba 12, mechi ya raundi ya tisa ya Ligi Kuu 2016/17.

Mbao ni timu iliyopandishwa Ligi Kuu kwa mgongo wa TFF baada ya timu za Geita FC na Polisi Tabora kudaiwa kupanga matokeo.

Mechi hii nayo inatarajiwa kupata mashabiki wengi hasa wa Mwanza, kuangalia nani zaidi kati timu hizo.

6. Azam vs Yanga

Mechi hii itakuwa ni ya raundi ya 10 na itachezwa Oktoba 16. Zinapocheza Yanga na Azam kwa sasa kwenye soka la Tanzania ni moja kati ya mechi kubwa na inayofuatiliwa na watu wengi nchini.

Pamoja na kuwapo na upinzani mkubwa, lakini matokeo ya mechi baina ya timu hizo mara nyingi hutoa ishara timu gani inaweza kuwa bingwa.

Msimu uliopita katika mechi zote mbili - kwanza bao 1-1, kisha 2-2.


Credits: IPPMedia
ZeroDegree.
Dabi kali 6 msimu ujao wa ligi kuu ya vodacom. Dabi kali 6 msimu ujao wa ligi kuu ya vodacom. Reviewed by Zero Degree on 7/25/2016 10:16:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.