Loading...

Kikosi cha Simba kuwekwa hadharani wiki ijayo.

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Simba, Mcameroon Joseph Omog amesema kikosi kamili cha wachezaji kitakachoingia kwenye ushindani wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2016/2017 kitawekwa hadharani wiki ijayo.

Omog alisema hayo alipozungumza na gazeti hili juzi kwenye uwanja wa Chuo cha Biblia cha Highland cha Kanisa la Baptist mjini hapa baada ya mechi ya kirafiki kati ya timu yake na Polisi inayoshiriki daraja la kwanza. Simba ilishinda mabao 6-0 katika mechi hiyo.

Alisema kikosi cha wachezaji atakachokiunda mwanzoni mwa wiki ijayo anaamini kitakuwa cha kuleta ushindi katika michuano ya Ligi Kuu. Ligi Kuu imepangwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20 mwaka huu ambapo Simba itaanzia nyumbani dhidi ya Ndanda kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

“Bado sijapata kikosi kamili ...ninatumaini kuanzia wiki ijao nitakuwa nimewapata wachezaji wa kikosi cha kwanza kitakachokuwa tayari kwa Ligi Kuu msimu huu na kuweza kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara,” alisema Omog.

Omog alisema kuifunga timu ya Polisi Morogoro kwa bao 6-0 kwenye mchezo wa kirafiki haimaanishi kuwa timu imeiva na kuwa na kikosi imara kwa kuwa bado anahitaji muda zaidi wa kuwapatia wachezaji wake mafunzo na mbinu za kisasa za uchezaji wenye kuleta ushindi kwenye michuano hiyo.

“Mchezo wetu na Polisi Morogoro umekuwa mzuri na nimeutumia kuona mapungufu ya wachezaji wangu na uwezo wao kwa kile walichojifunza kwa zaidi ya wiki mbili na nusu sasa,” alisema Omog.

“Ushindi huu haumaanishi nimemaliza kazi ni mchezo wa kirafiki nimeutumia kuwaangalia wachezaji wangu...nitaendelea kuwafundisha mazoezi zaidi na mbinu za kimchezo imani yangu mwanzoni mwa wiki ijayo nitakuwa na kikosi kizuri kitakachoweza kuleta ubingwa," alisema Omog.

Alisema alifurahi kuona tangu kuanza kwa mazoezi kwenye kambi hiyo wachezaji wamebadilika tofauti na mwanzo alipoanza kuwafundisha walipokuwa wametokea katika mapumziko.

“Wachezaji wamekuwa wepesi kwenye mazoezi tofauti na hapo mwanzo wengi wao walionekana kuwa na uzito mkubwa kutokana na mapumziko waliyokuwa nayo,” alisema Omog.

Omog alisema kuwa licha ya mafunzo na mazoezi yanayotolewa kwa wachezaji hao bado inahitajika michezo mingine mitatu ama zaidi ya kirafiki kabla ya kuanza ligi.

Pamoja na hayo, Omog alimpongeza Kocha msaidizi wa timu hiyo Jackson Mayanja kwa kumpatia ushirikiano mkubwa katika programu za mazoezi kitendo kinachowezesha kuijenga upya timu ya Simba iweze kutwaa ubingwa msimu wa ligi.

“Nipo na furaha kubwa kufanya kazi pamoja na kocha Mayanja ...tunashirikiana vyema ili kuona wapenzi wa Simba na viongozi wake kuwa mwaka huu ni wa kubeba mataji ya ubingwa ...tunaomba ushirikiano wao,” alisema.

ZeroDegree.
Kikosi cha Simba kuwekwa hadharani wiki ijayo. Kikosi cha Simba kuwekwa hadharani wiki ijayo. Reviewed by Zero Degree on 7/28/2016 12:04:00 PM Rating: 5

Powered by Blogger.