Loading...

Lipumba adaiwa kufanya kampeni kiaina msibani.

HARAKATI za aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba kutaka kuwania tena kiti hicho, zimeanza rasmi baada ya kiongozi huyo kuibuka katika msiba wa Ismail Mapande 'Kundambanda' na kuonyesha alikusudia kupiga kampeni.

Prof.Lipumba ambaye aliachia ngazi nafasi hiyo wakati Cuf ikijiandaa na Uchaguzi Mkuu wa Desemba 25 mwaka jana, aliibuka ghafla msibani na kutengeneza fursa kadhaa za kuzungumza na waombolezaji kabla na baada ya Kundambanda aliyekuwa mgombea wa ubunge jimbo la Masasi kupitia Cuf kuzikwa.

Kwanza alitambulishwa kuwa mgeni rasmi, wakati aliyepewa nafasi hiyo ni Mkurugenzi wa Sera na Uchaguzi wa Cuf Taifa, Shaweji Mketto ambaye licha ya kuwapo kwake katika tukio, ugeni rasmi ukaelekezwa kwa Prof.Lipumba.

Akuzungumza katika msiba huo, Prof.Lipumba alikiri kuwa licha ya kufanyakazi kwa kipindi kifupi na marehemu Kundambanda, ilitosha kutambua uwezo na ushawishi mkubwa aliokuwa nao kisiasa.

Mwenyekiti huyo mstaafu alitoa sh.50,000 na kuahidi nyingine 150,000 ili zitumike kufungua akaunti maalum ya mtoto wa miaka mitano wa marehemu Kundambanda ili zimsaidie katika elimu mara atakapoanza elimu ya sekondari.

Hata hivyo, wakizungumza katika tukio hilo baadhi ya waombolezaji na wengi wao wakiwa wafuasi wa chama cha Cuf na
Chadema, walisema hatua hiyo ya Prof.Lipumba ni mpango wake wa kuanza kushawishi wanachama ili wampigie kura wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu,

Muombolezaji Issa Matandu amesema kuwa Prof.Lipumba hafai tena kuchaguliwa kuwa mwenyekiri wa Cuf kwa sababu alikiteleza chama wakati mgumu na dhamira yake ililenga kuona chama kinakufa kabisa.

Sophia Malibiche aliunga mkono kauli hiyo na kuongeza kuwa, Prof.Lipumba hana sifa tena ya kuwa mwenyekiti wa taifa wa chama kikubwa kama Cuf na kwamba anafaa kuendelea kuwa mwanachama wa kawaida tu.

Hata hivyo, Prof. Lipumba alisema hawezi kutumia jukwaa la msiba kuomba kura kwa sababu anatambua wengi kati ya waombolezaji si wapiga kura na kwamba ujio wake Masasi ulitokana na kuheshimu mchango wa Kundambanda katika siasa hasa za kudai haki.

Akitoa salamu za wabunge wa upinzani wa majimbo ya mikoa ya Lindi na Mtwara, mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka aliwataka waombolezaji kuendeleza yote mema aliyoacha Kundambana katika harakati zake za kudai haki kupitia siasa na sanaa.

"Unaweza kusema maneno mengi hapa, lakini muhimu kuliko yote ni kuendeleza harakati za kupigania haki na usawa kisiasa alizokuwa akiamini marehemu. Huo ndio utakuwa mchango wetu mkubwa na urithi wetu kwake," alisema Kuchauka.

Source: Nipashe(IPPMedia)
ZeroDegree.
Lipumba adaiwa kufanya kampeni kiaina msibani. Lipumba adaiwa kufanya kampeni kiaina msibani. Reviewed by Zero Degree on 7/30/2016 08:35:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.