Loading...

Magufuli apokea ‘zigo’ la vigingi 12 CCM.

RAIS John Magufuli amebainisha ‘vigingi’ 12 vinavyohatarisha ustawi wa CCM na kuanika mikakati kadhaa ya kukabiliiana navyo katika kipindi chake cha kukiongoza chama hicho ili mwishowe kiendelee kuwa kimbilio la Watanzania na kushinda kirahisi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Akizungumza kwa dakika 80 mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa wa CCM mjini Dodoma jana, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa asilimia 100 kuwa mwenyekiti wa chama hicho akimrithi Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, Magufuli alisema maeneo hayo ndiyo atakayoanza kuyashughulikia ili kuhakikisha kuwa CCM inazidi kusonga mbele.

Alizungumzia pia tatizo ufisadi, utegemezi wa chama kwa matajiri ambao hupewa vyeo vya ukamanda wa vijana, rushwa katika mchakato wa kupata vyeo ndani ya chama, ufisadi wa mali za chama na pia tatizo la ukosefu wa maadili.

Aidha, maeneo mengine aliyopania kuyashughulikia ni tatizo la kuwapo kwa badhi ya makada wanaojirundikia vyeo, udhaifu wa baadhi ya jumuiya za chama na umuhimu wake kwa Watanzania na pia suala la maslahi kwa watendaji wa chama hicho.

Mambo mengine ambayo baadhi hakuyataja moja kwa moja jana ni unafiki aliowahi kuzungumzia mara kadhaa hapo kabla, kuwavutia vijana wengi zaidi kwa chama hicho na pia kukabiliana na kasi ya upinzani, hasa wanaounda Muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)

Katika mkutano huo maalumu kwenye ukumbi maarufu wa ‘white house’ jana, Magufuli alipigiwa kura za ndiyo 2,398 za wajumbe wa idadi hiyo waliokuwamo ukumbini, hivyo kuchaguliwa kwa asilimia 100.

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Kikwete, aliibua shangwe kubwa ukumbini baada ya kutangaza matokeo hayo na kisha kumkabidhi rasmi ‘kijiti’ cha uongozi wa chama hicho kwa kipindi kijacho cha miaka mitano.

Jambo hilo liliwezekana baada ya Kikwete kung’atuka kabla ya wakati wake kwa nia ya kumpisha Magufuli, ikiwa ni kuendeleza utaratibu wa chama hicho wa kumuwezesha Rais aliye madarakani kushikilia kofia mbili kwa wakati mmoja, yaani urais na pia uenyekiti wa chama.

1. KUIMARISHA CHAMA

Hiki ni kigingi cha kwanza ambacho Magufuli ameahidi kuwa ataanza kukishughulikia. Alisema araanza kuimarisha utendaji wa chama kwa kujenga chama chenye uwezo wa kuisimamia serikali iliyopo madarakani.

Alisema katika kufanikisha hilo, mtu yeyote aliye serikalini ambaye atashindwa kujua kuwa chama ndiye bosi wake ni vyema akaanza kutoka sasa.

Kwa mujibu wa takwimu za NEC, inaonekana kuwa CCM iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Kikwete kabla ya kukabidhiwa kwa Magufuli jana, ilipata ushindi mwembamba zaidi wa asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa, kiwango kinachoashiria matokeo mabovu zaidi kwa CCM katika chaguzi zote za vyama vingi kwa nafasi ya urais nchini. 

Mwaka 1962, katika uchaguzi wa kumpata Rais wa kwanza wa Tanganyika uliohusisha vyama vingi, mgombea wa chama cha TANU kilichoungana na ASP Februari 5, 1977 na kuzaliwa CCM, Julius Kambarage Nyerere, aliibuka na ushindi wa asilimia 99.2 na kumuacha mbali hasimu wake wa karibu, Zuberi Mtemvu wa chama cha ANC aliyepata asilimia 0.8. 

Baada ya hapo, mfumo wa siasa nchini ulikuwa wa chama kimoja na hivyo hakukuwapo na uchaguzi mwingine wa Rais uliohusisha vyama vingi hadi yalipofanyika mabadiliko mwaka 1992 na kuurejesha mfumo wa vyama vingi badala ya ‘chama kushika hatamu’.

Katika uchaguzi mwingine wa vyama vingi mwaka 1995, CCM chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, ilimsimamisha Benjamin Mkapa na kuibuka na ushindi wa asilimia 61.82% licha ya kuwapo kwa ushindani mkali kutoka kwa mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa na nguvu kubwa wakati huo, Augustino Mrema wa NCCR-Mageuzi.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, CCM ikiwa chini ya uenyekiti wa Mkapa ambaye ndiye aliyepitishwa kuwa mgombea, ilikubalika zaidi kwa wapiga kura baada ya kuibuka na ushindi mkubwa zaidi wa asilimia 71.74%.

Aidha, makali ya CCM chini ya uongozi wa Mkapa yaliongezeka zaidi katika uchaguzi wa mwaka 2005 baada ya kumuwezesha mgombea wake, Jakaya Kikwete, kuibuka na ushindi ulioitwa wa ‘kimbunga’ wa asilimia 80.28.

Hata hivyo, kibao kilianza kuigeukia CCM kuhusiana na ushindi wake katika uchaguzi mkuu baada ya ushindi wake kwa nafasi ya urais kuporomoka mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 61.17, ikiwa ni anguko la takribani asilimia 20.

Wakati huo, mwenyekiti alikuwa Kikwete, na ambaye ndiye aliyekuwa akipeperusha bendera ya chama tawala dhidi ya wapinzani.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, CCM ya uenyekiti wa Kikwete ndipo ilipopata matokeo dhaifu zaidi kulinganisha na chaguzi nyingine zote baada ya mgombea wake, Magufuli kupata ushindi wa asilimia 58.46.

Kiwango hicho kiliwapa nafuu kubwa wapinzani ambao waliweka rekodi ya kura baada ya Edward Lowassa kupata asilimia 39.97 ya kura halali zilizopigwa.

Lowassa ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani, alihama CCM baada ya kuenguliwa katika mbio za kuwania urais ndani ya chama hicho na hivyo kwenda kupeperusha bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na vyama washirika vinavyounda muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF) .

2. KUBORESHA KATIBA

Jambo la pili alisema ni kupitia upya katiba ya chama hicho ili kuona uwezekano wa kuboresha baadhi ya maeneo anayoamini kuwa kwa sasa yamepitwa na wakati.

3. UTITIRI WA VYEO

Eneo jingine ambalo Magufuli ameahidi kulishughulikia ni kufanya marekebisho ya katiba ya CCM ili kuondoa uwezekano wa mwanachama mmoja kuwa na utitiri wa vye.

Alisema baadhi ya vyeo hivyo vikiwamo vya chipukizi wa chama wanaoanzia miaka nane hadi 15, hadhani kwamba vina mantiki na badala yake watoto waachwe washughulikie masuala yao ya shule.

Alitoa mfano mwingine wa vyeo kuwa ni pamoja na makamanda wa vijana ambao alisema kwa sasa wanachaguliwa watu wenye fedha na kupewa nyadhifa hizo.

“Baadhi ya vyeo vinakuwa kero wakati wa chaguzi, watu wana vyeo vingi, unakuta waziri ndiyo huyo huyo mbunge na ndiye huyo pia mjumbe wa NEC,” alisema Magufuli.

4. WATENDAJI VIHIYO

Jambo jingine alilosema kuwa atalishughulikia ni kuhakikisha chama kinakuwa na watendaji wenye sifa na kuondoa wale wasio na sifa.

Pia alisema jambo jingine ni kuhakiki mali zote za chama kujua zipo wapi na zinatumiwa na nani.
Katika kuhakikisha suala hilo, alisema ataunda kikosi maalumu kuhakiki mali hizo.

Magufuli alisema pia katika uongozi wake atahakikisha anahamisisha wanachama wanalipa ada zao tena kwa njia za kielektroniki.

Mwenyekiti huyo mpya, alisema jumu lake jingine itakuwa kuongeza idadi ya wanachama wa chama hicho ambao kwa sasa ni milioni 8.7.

Katika kufanya hilo alisema pia wataangalia zaidi kwa vijana ili kupata wanachama wengi na waadilifu.

5. RUSHWA

Jambo jingine alilosema atapambana nalo kwa nguvu zake zote ni rushwa ndani ya chama ambayo alisema kwa sasa bila kuwa na fedha ni vigumu ndani ya CCM kupata wadhifa.

“Niligombea urais niliyaona huko, nakumbuka Iringa nilikuwa natafuta wadhamini wilaya nzima wamenunuliwa ikabidi niende vijijini huko ndo nikaomba kura kwenye Kata moja. Fedha ndo tiketi ya kupata uongozi ndani ya chama, na ndo maana maeneo mengine tukapoteza.

“Mtu yoyote atakayetumia rushwa hatachaguliwa, hatopitishwa,” alisema.

6. MPASUKO

Jambo jingine atakalolishughulikia Magufuli ni kuwaunganisha wanachama baada ya baadhi yao kugawanyika kutokana na makundi ya wakati wa uchaguzi.

Hapo, alizungumzia pia kilichojiri wakati wa mchakto wa urais ndani ya CCM ambapo baadhi ya makada walimuimba Lowassa kwenye kikao.

“Sidhani kama nina moyo wa uvumilivu kama wewe (Kikwete), na siku lie nimeingia pale nikakuta watu wanaimba wana imani na mtu fulani, sidhani kama ningevumilia. Nadhani siku ile ile nusu ama robo wangeondoka,” aliondoka.

7. MASLAHI YA WATENDAJI

Rais Magufuli alisema ili Watendaji wa chama wafanye kazi vizuri wanapaswa kuwa na maslahi bora.
Aliahidi kuangalia na kuboresha maslahi ya watendaji wote ili kuifanya kazi hiyo vyema pamoja na kuwaepusha kuwa ombaomba lakini pia wasinunuliwe.

8. UFISADI MALI ZA CHAMA

Hivi sasa kuna tarifa za kuwapo kwa baadhi ya mali za chama kutumiwa vibaya na baadhi ya watu kwa njia za kifisadi, ikiwamo mikataba ya majengo mbalimbali na viwanja vinavyomilikiwa na CCM

Akizungumzia hilo jana, Magufuli alisema atahakikisha anaimarisha rasilimali zilizopo ndani ya chama ili kukiongezea kipato na kuhakikisha vilevile kuwa mali za wanachama zinaorodheshwa na wanachama

9. ADA YA WANCHAMA

Magufuli alizungumzia pia tatizo la kuwapo kwa mwitikio mdogo wa ada za chama ambalo Kikwete aliligusia wakati wa hotuba yake.

Akizungumzia hilo, Magufuli alisema atahakikisha kuwa wancham wanongezeka.

10. MVUTO KWA VIJANA

Kuhusiana na jambo hilo, Magufuli alisema atahakikisha kuwa chama kinajiimarisha kwa kuwvutia vijana wengi zaidi.

“Tutaongeza idadi ya wanachama… siasa ni mchezo wa idadi, waaminifu watakaoshiriki shughuli za maendeleo hususani vijana, katika kuwavutia… ni kutekeleza ilani yetu,” alisema Rais Magufuli.

11. USALITI

Magufuli alizungumzia pia tatizo la usaliti. Mara kadhaa hapo kabla, Magufuli alishasema ni bora kuwa na wanchama wachache wakweli kuliko wengi walio wasaliti.

“Nitahakikisha suala la wasaliti ndani ya CCM ninalikomesha ili kumaliza tabia ya baadhi ya wanachama mchana kuwa CCM na usiku kuwa upinzani,” alisema.

Alisema wasaliti wa namna hiyo hawatakuwa na nafasi na aliwataka kama wapo ni vyema wakajirekebisha.
“Kama wapo watubu tu maana.. kuliko kuwa na wanachama wengi wanafiki ni bora kuwa na wanachama wachache kwani ni bora kuishi na mchawi kuliko mnafiki,” alisema Rais Magufuli.

12. TISHIO LA UPINZANI

Ijapokuwa Rais Magufuli hakutaja moja kwa moja juu ya tishio la kuimarika kwa upinzani dhidi ya cham tawala, lakini alizungumzia eneo hilo kia aina kwa kusisitiza kuwa kwa kuyafanya yote aliyoyaahidi, lengo ni kuhakikisha kuwa CCM ianshinda kwa kishindo katika uchaguzi wa mwaka 2020 kwa kuhakikisha kuwa CCM inaendelea kuwa chama kimbilio la wanyonge.

AKUMBUSHIA YA LOWASSA

Aidha, katika hotuba yake hiyo, Magufuli alikumbushia wakati mgumu alioupata Kikwete wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais na kugusia namna wajumbe wa walivyokuwa wakiimba kwa kutaja majina ya badhi ya wagombea.

Hakumtaja Edward Lowassa moja kwa moja, ingawa ndiye aliyeibua mtafaruku baada ya kuimbwa kwa kutajwa jina lake kufuatia kamati kuu kufikishiwa majina matano tu, bila kuwamo kwa Lowassa.

JK AFICHUA WALIVYOMBEMBELEZA

Wakati huo huo, mwenyekiti mstaafu, Kikwete alifichua jinsi walivyohaha kumbembeleza Magufuli ili akubali kuwa mwenyekiti wa chama sasa.

Alisema kuwa awali, Magufuli alikataa na kusisitiza kuwa aachwe sasa ili ashughulikie mambo ya serikali hadi mwaka 2017 wakati Kikwete atakapomaliza muda wake.

Hata hivyo, walimbembeleza na mwishowe akakubali, jambo ambalo hata Magufuli mwenyewe alikiri baadaye na kumshukuru Kikwete huku akimpa pole kwa kuzushiwa kuwa ndiye aliyekuwa ‘akimbania’ kuwa mwenyekiti wakati ukweli ni kwamba yeye ndiye aliyekuwa akikataa.

Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuf Makamba, alimtoa hofu Magufuli na kuwaonya wapinzani kuwa sasa amepatikana mtu atakayewabatiza kwa moto badala ya kubatizwa kwap kwa maji enzi za Kikwete.

Source: IppMedia
ZeroDegree.
Magufuli apokea ‘zigo’ la vigingi 12 CCM. Magufuli apokea ‘zigo’ la vigingi 12 CCM. Reviewed by Zero Degree on 7/24/2016 11:26:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.