Loading...

Serikali kuhamishiwa Dodoma kabla ya 2020.

RAIS John Magufuli, ameahidi kuwa ataihamishia serikali Dodoma, kabla ya kukamilisha muhula wa miaka mitano ya uongozi wake, ulionza mwaka jana.

Alitoa ahadi hiyo jana mjini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi ambao ulimpigia kura zote za kuwa Mwenyekiti wa CCM na kukabidhiwa rasmi uongozi huo.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa jukumu hilo baada ya kushinda kwa asilimia 100, Rais Magufuli alisema Ikulu ya Chamwino, Dodoma ina majengo bora ambayo yamemshawishi, serikali ihamie huko.

“Tujipange ndani ya serikali ya awamu ya tano kuhamia hapa, tusitafute visingizio, kama wajumbe wa mkutano mkuu, wamekaa Dodoma, kama Bunge lipo hapa sioni sababu mimi kuendelea kukaa Dar es Salaam,” alisema.

Alisema siku ambayo atahamia Ikulu ya Dodoma, watakaomfuata ni pamoja na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kasssim Majaliwa pamoja na makatibu wakuu wote.

“Siku yeyote tutakapohamia Malecela tuchinjie ng’ombe tule,” alisema, akimtania Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu John Malecele, ambaye anaishi Dodoma.

Mwaka juzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge na Sera aliliambia Bunge kuwa ofisi za serikali zitajengwa eneo la Ihumwa mkoani Dodoma.

Aidha, Lukuvi aliliambia Bunge la Bajeti kuwa pamoja na kujenga makao makuu ya serikali pia, kujengwa eneo rasmi la makaburi ya viongozi wa kitaifa.

ABAKIZA SEKRETARIETI

Katika mkutano huo, Magufuli alisoma barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, aliyomuomba apumzike nafasi hiyo yeye pamoja na viongozi wengine.

Magufuli baada ya kuisoma barua hiyo ya Julai 23, mwaka huu, alisema baada ya kuisoma na kutafakari na kumwangalia Kinana na majukumu yaliyopo mbele yao, ameamua waendelee na kazi ya kukiongoza chama.

“Kama kutakuwa na haja ya kufanya mabadiliko nitaitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa siku nyingine baadaye huko.

Nafahamu wapo waliojipanga kwa nafasi hizi lakini imekula kwao,” alisema.

Akitoa neno la shukrani, Kinana alimshukuru Rais kwa kumwamini pamoja na sekretarieti.

“Tutafanya kazi kwa bidii kwa uadilifu kwa ufanisi na uhodari na tutatekeleza maagizo uliyoyatoa,” alisema na kuongeza kuwa hatalewa sifa badala yake atazifanya kama changamoto katika kutekeleza majukumu yake.

Wajumbe wa sekretarieti.ni Katibu Mkuu Kinana, Manaibu Katibu Wakuu Bara na Zanzibar, Katibu wa Itikadi na Uenezi.

ZeroDegree.
Serikali kuhamishiwa Dodoma kabla ya 2020. Serikali kuhamishiwa Dodoma kabla ya 2020. Reviewed by Zero Degree on 7/24/2016 11:17:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.