Loading...

Mahakama maalumu itakayoshughulikia MAKOSA YA RUSHWA NA UFISADI, Kuanza Rasmi Leo.


Pamoja na kuanza kwa mahakama hiyo, serikali imeanza mchakato kuifanyia marekebisho Sheria Namba 11 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini ya Mwaka 2007 ili kuongeza ukubwa wa adhabu zinazotolewa sasa.

Mahakama hiyo iliyoahidiwa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na imo katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi, itaimarisha zaidi taasisi za uwajibikaji zinazohusika na mapambano dhidi ya rushwa.

Ahadi hiyo ambayo inatimizwa ndani ya kipindi cha miezi isiyozidi saba tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani ni sehemu ya mapambano ya kujenga misingi ya uchumi kwa kudhibiti rushwa na mianya yake na kuleta uwajibikaji.

Akiahirisha Bunge jana mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema utekelezaji wa ahadi hiyo unakwenda sambamba na kuonesha dhamira ya serikali ya kushughulikia makosa ya rushwa na kuweka misingi imara ya uwajibikaji katika sekta zote.

“Mahakama itawafanya watu waliozoea rushwa na ufisadi kujiuliza mara mbili kabla ya kufanya uhalifu huo yaani kuwa deterrent,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza kuwa kuwapo kwake kutahamasisha wafanyabiashara kufanya shughuli zao bila shaka huku umuhimu kwao, ikiwa ni kulipa kodi.

Akielezea umuhimu wa mahakama hiyo, alisema kwamba itasaidia kuendeleza nia ya serikali ya watu kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.

Akielezea umuhimu wa kodi, alisema kuna mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uendeshaji wa shughuli za serikali na hivyo serikali itaendelea ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.

Aidha, alisema serikali itaanzisha Kikosi Maalumu cha kufuatilia kwa karibu matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) za kutoa risiti kila mfanyabiashara anapouza bidhaa au huduma na kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) wanashirikiana na Wakala wa Serikali wa Serikali Mtandao kutekeleza mfumo wa kuwa na dirisha moja na pia kudhibiti kikamilifu mizigo inayoingia na kutoka bandari kavu.

Udhibiti wa matumizi

Akizungumzia matumizi, Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea na kudhibiti matumizi yasiyokuwa ya lazima na kufuatilia bajeti na matumizi ya fedha za umma.

Na ili kufanikisha hilo, itafanya mapitio ya majukumu ya wizara na taasisi za umma ili kuwianisha majukumu ya vyombo vya serikali na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, uhakiki wa wafanyakazi utaendelea na watendaji wakitakiwa wanadhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya fungu husika lililoidhinishwa na Bunge.

Aidha, Waziri Mkuu aliagiza halmashauri zote nchini kuanzia leo kuhakikisha kwamba zinatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato, kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboresha makusanyo iwe yanafanywa na halmashauri au kupitia wakala wake.

Waziri Mkuu alisema wabunge wamepitisha Bajeti ya Serikali inayotegemea sana ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi kutoka nje na kuhimiza uwajibikaji katika kuongeza juhudi za kukusanya na kupanua wigo wa kutoza kodi ili mapato yaongezeke.

Aidha, alisema ipo haja ya wananchi kudai risiti kwa huduma mbalimbali wanazonunua na kushirikiana na serikali kubaini wakwepa kodi na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya serikali.

Aliwataka watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi kwa maadili katika maeneo yao wakijenga utamaduni wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na tija.

Mpango wa Maendeleo

Akizungumzia maeneo manne ya Mpango wa Maendeleo, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imeweka msingi kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa kukuza na kujenga uchumi wa viwanda kwa kuweka mazingira yatakayochochea maendeleo ya viwanda.

Aidha, imejiweka katika hali ya kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu kwa kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa ni bora na inayojenga msingi wa rasilimali watu wanaohitajika kuipeleka nchi katika uchumi wa kati.

Alisema ili kufanikisha hayo serikali itaimarisha mifumo ya kisheria kuwa rafiki na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje huku ikiimarisha miundombinu ili iweze kutumika kirahisi na kupunguza gharama zake.

Ili kufanikisha ufanisi na tija, Waziri Mkuu alisema serikali itaimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya mpango wenyewe wa maendeleo mara kwa mara.

Ili kufanikiwa ametaka tabia ya vijana kushinda katika pombe na kucheza pool table kuachwa na kuwataka viongozi waliochaguliwa sasa wilayani na mikoani kuhakikisha kwamba maeneo ya starehe hayafunguliwi wakati wa muda wa kazi ili vijana washiriki katika uzalishaji mali.

Akizungumzia mkakati wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, Waziri Mkuu alisema serikali itategemea zaidi sekta binafsi kama injini ya ukuzaji uchumi na maendeleo na kwamba serikali haitajiingiza moja kwa moja katika kujenga viwanda na kufanya biashara.

Miradi ya umeme

Akizungumzia uimarishaji wa uchumi kwa kuwa na uhakika wa nichati hadi vijijini, alisema serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuyapatia maeneo yaliyo nje ya gridi ya taifa nishati bora ikiwa ni pamoja na maeneo ya visiwani.

Alisema Serikali ya Uingereza na Sweden zinachangia katika kuhakikisha kwamba mifumo hiyo ya kupeleka umeme maeneo yaliyo nje ya gridi inafanikiwa. Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh trilioni moja kutoka ndani na benki ya dunia kwa ajili ya kuendeleza nishati vijijini.


ZeroDegree.
Mahakama maalumu itakayoshughulikia MAKOSA YA RUSHWA NA UFISADI, Kuanza Rasmi Leo. Mahakama maalumu itakayoshughulikia MAKOSA YA RUSHWA NA UFISADI, Kuanza Rasmi Leo. Reviewed by Zero Degree on 7/01/2016 11:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.