Loading...

Mtaala wa WAJIBU kuanzishwa katika elimu.

Waziri Wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ameahidi kusaidia kuingiza kwenye mtaala wa elimu mpango wa WAJIBU wenye lengo la kuwawezesha watoto na vijana kujua umujimu wa kutumia taasisi za fedha katika kutunza na kujiwekea akiba.



Mpango huo ambao ulizinduliwa rasmi jana katika Shule ya Msingi Mlimani, umeanzishwa kwa ushirikiano wa Benki ya NMB na shirika la kimataifa la Womens World Banking (WWB).

WAJIBU maana yake ni ‘ Wajibika’ inayojumusisha aina tatu za akaunti za akiba ambao ni NMB Mtoto Akaunti, NMB Chipukizi akaunti na NMB Mwanachuo Akaunti.

Katika risala yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti na Ubora wa Shule, Dk. Edicome Shirima, kutoka wizarani hapo, waziri alisema serikali inatambua umuhimu wa elimu hiyo ya kifedha kwa watoto na vijana.

“Nikiwa kama waziri wa elimu nitahakikisha katika kipindi changu WAJIBU inaingia kwenye mtaala wa elimu ili kuwawezesha watoto sasa kufahamu vyema namna ya kupanga matumizi, kuweka akiba kwa ajili ya baadaye,” alisema.

Aidha alisema wakati program hiyo ikizinduliwa, asilimia 20 ya Watanzania, ndio wenye uelewa mzuri wa elimu ya kifedha.

Hivyo alisema program ya WAJIBU ni fursa ya pekee ya kuwawezesha watoto kujengewa msingi wa kujua umuhimu wa kutumia taasisi za fedha katika kutunza na kujiwekea akiba kwa matumizi ya baadaye.

Pia alisema serikali inadhamiria kuboresha na kuendeleza elimu ya fedha katika ngazi zote za Watanzania ili kuziwezesha kutambua umuhimu wa kuweka akiba itakayoinua vipato vyao pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema miongoni mwa mikakati ya kuwezesha elimu hiyo inawafikia Watanzania ni mpango wa miaka mitatu 2014/17 ulioanzishwa na Benki Kuu Tanzania (BoT), ambao umelenga asilimia 80 ya Watanzania kuipata.

Aidha, alisema taarifa ya kifedha ya nusu mwaka inaonyesha asilimia 70 watafikiwa na elimu hiyo ifikapo mwakani.

Alisema jamii inatakiwa kutambua kuwa elimu ya kifedha sio tu kwa wale wenye nacho (matajiri) bali hata wenye kipato cha chini.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji NMB, Ineke Bussemaker, aliiomba serikali iingize WAJIBU kwenye programu zake za elimu ili iwe endelevu na kuwezesha watoto na vijana kunufaika nayo wakiwa kwenye umri mdogo.

Alisema akaunti zimetengenezwa kwa ajili ya kundi hilo ili kuwasaidia wazazi na vijana kujiwekea akiba na kupanga matumizi wao wenyewe au kwa msaada wa wazazi.

Alitaja aina za akaunti na umri wa watoto kuwa ni Mtoto akaunti (0- 18), Chipukizi (13-17) na Mwanachuo (18 na kuendelea).

Aidha alisema zaidi ya shule 20,000 nchini zinatarajia kunufaika na elimu ya mafunzo ya uwekaji akiba kwa manufaa ya baadaye.

Mkurugenzi wa Bidhaa wa WWB, Jennifer McDonald, aliipongeza benki hiyo kwa kupanua zaidi WAJIBU kwa kuongeza kipengele vya mpango wa kuelimisha jamii kuhusu masuala ya kifedha ambayo ni fursa pekee ya kuwajenga vijana kuwa na maarifa ya kumiliki akaunti za akiba wakiwa wadogo.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mlimani, Pendo Kujelwa, aliishukuru benki hiyo kwa kuiweka Mlimani miongoni mwa shule kumi za awali zilizonufaika na mafunzo ya uwekaji akiba.

ZeroDegree.
Mtaala wa WAJIBU kuanzishwa katika elimu. Mtaala wa WAJIBU kuanzishwa katika elimu. Reviewed by Zero Degree on 7/30/2016 09:16:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.