Loading...

Rais Magufuli apiga marufuku Malori ya mizigo kuonekana Jijini Dar, ataka yote yaishie Ruvu.


UCHAMBUZI wa Rais John Magufuli kuhusu gharama za ujenzi wa reli ya kisasa, kuwa kilometa moja itagharimu kati ya dola za Marekani milioni 3.5 mpaka milioni nne, umedhihirisha namna siku za foleni za malori katika jiji la Dar es Salaam, zinavyohesabika.

Akizungumza juzi baada ya kumkaribisha mwenyeji wake, Rais wa Rwanda, Paul Kagame Ikulu Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kama hakutakuwa na matatizo ya ufisadi na utoaji wa hongo wa asilimia kumi ili kupata mradi huo; kilometa moja ya reli hiyo ya kisasa itagharimu si zaidi ya dola hizo za Marekani milioni nne.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, tuta la reli inayotumika sasa ndilo litakalotumika kwa ajili ya reli hiyo ya kisasa, hivyo mkandarasi hatokuwa na kazi ya kujenga tuta jipya na jambo linalofanya gharama hizo kuwa hata chini ya dola za Marekani milioni 3.5 kwa kilometa moja.

Katika uchambuzi huo, Rais Magufuli alisema tayari serikali imetenga dola za Marekani milioni 460 sawa na Sh trilioni moja, ambazo kwa hesabu za haraka, fedha hizo zinatosha kujenga zaidi ya kilometa 115 za reli hiyo.

Kwa hesabu hizo, fedha hizo zilizopitishwa na Bunge, zitawezesha mkandarasi kujenga reli hiyo mpaka eneo la Ruvu mkoani Pwani, ambako ni kilometa 70 kutoka jijini Dar es Salaam na kufika mpaka hata Chalinze, ambako ni kilometa 109 kutoka Dar es Salaam.

Malori kuishi Ruvu

Hesabu hizo na kwa uchambuzi huo, Rais Magufuli atakuwa ametuma ujumbe mkali kwa wamiliki wa malori ya usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam, kwenda mikoani na katika nchi mbalimbali zinazopitishia mizigo yake katika bandari hiyo.

Ujumbe huo unatokana na dhamira yake aliyoitoa Aprili 16 mwaka huu, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kwanza ya juu (Flyover) Tanzania, ambayo ujenzi wake ulishaanza katika makutano ya barabara za Mandela na Nyerere eneo la Tazara, kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema reli hiyo ya kisasa itakapofika Ruvu, kutajengwa bandari kavu kubwa katika eneo hilo ambayo ikikamilika, mizigo yote inayoshuka bandari ya Dar es Salaam, itasafirishwa kwa reli mpaka katika bandari hiyo.

Hatua hiyo ikifikiwa, ambayo kwa uchambuzi wake wa juzi, fedha zilizotengwa zinatosha kuifikia, Rais Magufuli alisema malori yote yanayochukua na kupeleka mizigo katika bandari hiyo, yataishia katika bandari kavu ya Ruvu na kupigwa marufuku kuonekana katika Jiji la Dar es Salaam.



ZeroDegree.
Rais Magufuli apiga marufuku Malori ya mizigo kuonekana Jijini Dar, ataka yote yaishie Ruvu. Rais Magufuli apiga marufuku Malori ya mizigo kuonekana Jijini Dar, ataka yote yaishie Ruvu. Reviewed by Zero Degree on 7/03/2016 10:46:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.