Loading...

Siri ya Kisimiri kuongoza taifa.

MJADALA kuhusu ubora wa shule binafsi, kuchangia kuongoza katika matokeo ya mtihani wa mwisho, ambao umekuwa ukijirudia kila mara wakati wa matangazo ya matokeo hayo, umebadilishwa mwelekeo na shule ya sekondari Kisimiri. Shule hiyo kati ya wanafunzi 63 waliohitimu kidato cha sita, wanafunzi 50 wamepata divisheni ya kwanza na wanafunzi 13 ndio waliopata divisheni ya pili.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa shule hiyo iliyoibuka kinara wa matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha sita, Mwalimu Emmanuel Kisongo, kabla ya kuelezea siri ya mafanikio ya shule hiyo, alisema kuwa akili na fedha ni vitu viwili tofauti.

Mwalimu Kisongo alisema pamoja na jamii na wanasiasa kutukana shule za kata, kwa kuzipa majina pamoja na walimu waliokuwa wakiziongoza; walimu na wanafunzi wa shule hiyo, waliazimia kufanya mapinduzi, ambapo alisema sasa yametimia kwa ada ya Sh 70,000 kwa mwaka, kupindua ada ya Sh milioni 10.

“Si mnajua tulipewa kila aina ya jina, mara shule ya kata na wengine wakatuita yeboyebo, sisi tuliamua kuibadilisha yetu kutoka shule ya kata kuwa shule maalumu, yaani walimu wetu ni maalumu na wanafunzi ni maalumu.

“Miundombinu yetu haijakaa sawa, tunakula maharage na hata baadhi ya wazazi wenye fedha, waliondoa watoto wao na kwa kiburi na dharau wakasema huku kuna mavumbi, lakini tukasema japo tunaletewa divisheni ya tatu, wengine wanakaribia divisheni ya nne, sisi tutatoa divisheni ya kwanza,” alisema Mwalimu Kisongo.

Mifumo imara Mwalimu Kisongo ambaye ni msomi wa Shahada ya Uzamili ya Menejimenti ya Elimu na Uongozi, alisema siri ya kwanza ya ufaulu wa shule hiyo, ilianzia katika kuimarisha idara na mifumo ya shule. Idara na mifumo iliyoimarishwa kwa mujibu wa Mwalimu Kisongo, ilihusu uchakataji wa majaribio yanayopaswa kutolewa kwa wanafunzi, mitihani na ukusanyaji wa ada.

“Katika tovuti ya shule ukifungua, kuna akaunti ya kila mwanafunzi ambayo ukiingia, unakuta matokeo na mahitaji ya kila mwanafunzi na hata mzazi anaweza kuingia, akakuta kila kitu na kama anadaiwa ada, inamuonesha...kwa hiyo sisi hatuandiki chochote kwenye makaratasi,” alisema Mwalimu Kisongo.

Mfumo huo pia unawajibisha walimu, ambapo alisema mwalimu asipotoa majaribio, alitoa mfano kama ni majaribio manne kwa muda walivyokubaliana, mfumo huo unamuonesha mwalimu husika.

Kwa mujibu wa Mwalimu Kisongo, walimu wote walipaswa kuwajaribu wanafunzi kwa kufuata viwango vya Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), ili kuhakikisha kuwa mwanafunzi anaiva kwa viwango hivyo.

Mbinu za uongozi Akizungumzia siri ya pili, Mwalimu Kisongo alisema walimu wote na wanafunzi walipandikizwa mbinu za uongozi, kiasi kwamba Mkuu wa Shule na hata walimu wasipokuwepo shuleni, Kaka Mkuu anatosha kuongoza shule.

Mwalimu huyo alitoa mfano wa mmoja wa wanafunzi waliomaliza shuleni hapo, Madaraka Amos ambaye alikuwa Kaka Mkuu, kwamba mara kwa mara aliongoza shule na kuna wakati alifikia hatua ya kuwa Mkuu wa Shule Msaidizi.

“Kuna wakati tulikuwa na walimu tisa, kati ya hao sita wakapewa kibali kwenda kusoma chuo kikuu, wakabaki watatu nao wakapewa kibali kwenda kusoma, Amos (anataja kampuni moja ya simu anakofanya kazi sasa), alikuwa Second Master,” alisema.

Katika kupandikiza mbinu za uongozi, Mwalimu Kisongo alisema aliwafundisha walimu na wanafunzi kwamba hakuna wajibu mdogo na hakuna serikali nyingine, isipokuwa yeye mwalimu na mwanafunzi, hivyo kila mwalimu na mwanafunzi alijiona kuwa ni sehemu ya uongozi na kila mmoja alijiona ana wajibu mkubwa.

“Kwa hiyo kila mmoja wetu alikuwa na kasi na shinikizo la ndani la kufanikiwa,” alisema na kuongeza hata Kaka Mkuu wa sasa, ‘anatumbua majipu’ kama Rais John Magufuli. Uzalendo Mwalimu Kisongo alisema pia alipandikiza uzalendo kwa wanafunzi hao na walimu kwa kuwaeleza hali halisi ya nchi yao, ili wajue kinachowakabili mbele yao.

“Nilipanda mafundisho ya Mwalimu Julius Nyerere (Baba wa Taifa), niliwaambia Mwalimu alisema kuwa hakuna mtu anayeweza kukulazimisha kupenda wengine, kuliko kujipenda wewe mwenyewe.

“Niliwaambia kuwa wewe (walimu na wanafunzi) na mimi tumepata elimu bora, hivyo tunatakiwa kuhudumia jamii ipate hali bora na huko ndio kujipenda,” alifafanua na kusema wanafunzi wanaotoka Kisimiri, wakiwekwa popote watafanikiwa.

Mwalimu Kisongo alisema walimu wa shule hiyo walifikia hatua wakashindwa kutenganisha mali binafsi na za shule, kwa kuwa walihakikisha hata dawati likivunjika, haliachwi liharibike bali linafanyiwa kazi mara moja.

Taaluma Katika mazingira hayo ambayo walimu wote wanasoma, akiwemo yeye Mwalimu Kisongo na hivyo shule katika baadhi ya nyakati kulazimika kuendeshwa na Kaka Mkuu, Mkuu huyo wa Shule alisema waliamua kumuona kila mmoja wao; mwalimu na mwanafunzi wote wanazo akili za kutosha.

“Walimu wote wanasoma, mimi nasoma na wanafunzi wanasoma, huku tuliko ni kijijini na chuo tunachosoma walimu kiko mjini, Kilometa 80 kutoka shuleni ...kila siku tunakimbizana na bodaboda, lakini Mungu akijalia baada ya muda tutakuwa na walimu wenye shahada za uzamili,” alisema.

Kutokana na ukosefu wa walimu na waliopo kuendelea na masomo, Mwalimu Kisongo alisema wanafunzi wa shule hiyo hawakujitenga kwa tofauti zao za dini, wala hawakuyumbishwa na tofauti hizo, ndio maana walifundishwa na walimu wa kukodi siku ya Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.

“Jumatatu mpaka Alhamisi huwa tunajifunza tulichofundishwa Ijumaa mpaka Jumapili, topiki haisubiri mwalimu, wakati mwingine tunaendelea wenyewe, hivyo walimu wakija Ijumaa mpaka Jumapili, lazima awe amejipanga, maana ataulizwa maswali kwa kuwa wanafunzi wanakuwa wameshapitia kinachofundishwa,” alisema.

Mpaka sasa kwa mujibu wa Mwalimu Kisongo, mbali na changamoto ya miundombinu, shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa walimu wa hesabu na fizikia, ingawa hali ya walimu kwa sasa ni nzuri kuliko shule ilivyoanza.

Mwalimu Kisongo alimpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi, Tekinolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, kwa kutembelea shule hiyo na kuona wanafunzi wanavyojifunza, ambapo alisema walianza kufanya vizuri wakati waziri huyo alipokuwa Katibu Mtendaji wa Necta.

Tandahimba Naye Mkuu wa shule ya sekondari Tandahimba, mkoani Mtwara ambayo imekuwa ya kumi kitaifa, Mwalimu Mathew Andilile, alielezea mazingira ya shule hiyo kuwa ni ya kawaida, yenye changamoto nyingi, lakini wanashukuru Mungu ndani ya changamoto hizo, wamefanikiwa. Shule hiyo imetoa wanafunzi 49 waliomaliza kidato cha sita, kati ya hao 19 ni divisheni ya kwanza, na waliobakia divisheni ya pili.

Mwalimu Andilile alisema hata wanafunzi wanaopokea si wa vipaji maalumu, maana tangu wameanza kufundisha wanafunzi wa kidato cha tano na sita, hawajawahi kupokea mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye divisheni ya kwanza na wanafunzi wengi ambao wamekuwa wakiwapokea, ni wenye divisheni ya tatu.

Alisema mazingira ya kuishi ya wanafunzi hao ni ya kawaida, asubuhi wanakunywa chai, mchana ugali wa maharage na jioni ugali wa maharage isipokuwa Jumatato, ambapo hula nyama mchana na jioni na Alhamisi na Jumapili, ambapo hupata wali maharagwe mchana na usiku.

Katika moja ya changamoto za shule hiyo, Mwalimu Andilile alisema ingawa gharama za kumtunza mwanafunzi ni Sh 1,500 kwa siku; kuna wakati halmashauri ilipungukiwa fedha, Julai na Agosti mwaka jana, ambapo wanafunzi hao walilazimika kuamkia uji wa chumvi asubuhi na kushindia na kulalia ugali maharage kila siku.

Aliwataka wazazi kujenga ushirikiano na walimu akisema baadhi ya wazazi ambao watoto wao wamefaulu, hawakuwahi kufika katika shule hiyo, wala hawafahamu iliko wala mazingira yake, ila watakuwa tu wamesikia watoto wao wamefaulu.

Alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo, kuwa ni pamoja na ukosefu wa madarasa, ambapo kwa sasa wanafunzi wa kidato cha tano, wanasomea katika bwalo la chakula na kusababisha wanafunzi kila mmoja kutafuta eneo la kulia chakula.

Mwalimu Andilile alisema kufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo, ambayo imewahi kuwa na matokeo mabaya katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne, kumetokana na kuzingatia walichofundishwa darasani na kujitafutia wenyewe ya nyongeza nje ya walichopewa darasani. Changamoto zingine alisema ni kutokuwepo kwa maktaba katika shule hiyo na upungufu wa vitabu.


Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Siri ya Kisimiri kuongoza taifa. Siri ya Kisimiri kuongoza taifa. Reviewed by Zero Degree on 7/17/2016 11:32:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.