Loading...

Taarifa zaidi kuhusu kifo cha askari polisi aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiongoza magari Jijini Dar.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime.

ASKARI Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kituo cha Polisi cha Oyesterbay katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, Sajini Mensa Pondibishe (D8254), ameuawa kwa kupigwa risasi kifuani na watu wasiofahamika.

Tukio hilo la kuhuzunisha, limetokea majira ya saa 2:00 usiku katika eneo la mataa ya Sayansi, Kijitonyama ambako marehemu Sajini Mensa alikuwa kazini, kandoni mwa eneo hilo la mataa, kuangalia mwenendo wa usalama barabarani.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime, alithibitishia Nipashe jana juu ya kutokea kwa tukio hilo.

Alisema kuwa Sajini Mensa, alipigwa risasi kifuani upande wa kulia na alifariki dunia wakati akiwa njiani kukimbiziwa Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya matibabu.

“Nilipopata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo nilifika katika Hospitali ya Mwananyamala na kukuta ameshaingizwa katika chumba cha upasuaji… alikuwa ameshafariki,” alisema Fuime.

Fuime alisema uchunguzi wa kuwabaini waliofanya mauaji hayo unaendelea na kwamba watakapobainika, watafikishwa mahakamani ili sheria itwae mkondo wake.

Tukio la aina hiyo linalohusisha kuuawa kwa askari wa usalama barabarani kwa kuviziwa akiwa kazini ni nadra kuwahi kutokea katika Kanda Malaumu ya Dar es Salaam na kwingineko nchini.

Usiku wa kuamkia Mei 20 mwaka huu, askari mwingine wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Makao Makuu Dar es salaam, Sajini Kinyogori, aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake eneo la Mwandege, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

ZeroDegree.
Taarifa zaidi kuhusu kifo cha askari polisi aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiongoza magari Jijini Dar. Taarifa zaidi kuhusu kifo cha askari polisi aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiongoza magari Jijini Dar. Reviewed by Zero Degree on 7/24/2016 10:25:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.