Loading...

Uwekaji alama X katika nyumba wazusha vilio Arusha.

TAHARUKI, vilio na baadhi ya watu kuzimia vilitokea juzi katika kata ya Murriet jijini Arusha, baada ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (AUWSA) kuweka alama ya X kwenye nyumba za kisasa zaidi ya 150 zilizojengwa katika mtaa wa Mlimani.

AUWSA iliamua kuweka X kwenye nyumba zilizo kwenye eneo la ekari 25 la mtu binafsi aliyefahamika kwa jina moja la Hadija chini ya ulinzi wa polisi, baada ya mamlaka hiyo kudai kufanya utafiti na kugundua kuwa nyumba hizo zilijengwa katika eneo ambalo lina vyanzo vya maji.

Baada ya zahma hiyo viongozi wote wa Jiji la Arusha wakiongozwa na mwakilishi wa AUWSA, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athumani Mhamia, Meya wa Jiji la Arusha, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na maofisa wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji walifanya ziara katika eneo hilo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa AUWSA, Mhandisi wa Mamlaka hiyo Mohamed Ismail alipewa nafasi ya kutoa ufafanuzi wa wao kuvamia eneo hilo na kuweka alama ya X katika kiwanja hicho cha Hadija na kusema kuwa walifanya hivyo baada ya kikao cha Bodi ya Maji ambacho Meya na Mkurugenzi ni wajumbe na kupewa amri kutoka ngazi ya juu kufanya hivyo.

Alisema AUWSA ilifanya utafiti mwaka 2013 na kugundua eneo hilo ni vyanzo vya maji na kukaa na mmiliki wa awali wa shamba hilo, mama Mbauda lakini hakuafikiana juu ya ulipwaji wa miaka hiyo, gharama ya Sh milioni nne.

Mhandisi huyo alisema baada ya kutokea uhaba wa maji jijini Arusha na ugumu wa kuchukua maji kutoka Arumeru hadi Murriet, waliamua tena kurudi katika shamba hilo lakini walikuta nyumba zikiwa zimejengwa.

Mbunge wa Arusha, Lema alimkatisha Ismail na kumtaka kumtaja aliyemtuma kwenda kuweka alama za X katika nyumba hizo bila ya ridhaa yao ya wamiliki wa nyumba hizo na hakuna makubaliano yoyote kati ya mamlaka hiyo na waathirika hao hatua ambayo ofisa huyo wa AUWSA aligoma kumtaja.

Baada ya hali hiyo Mbunge Lema alisema uwekaji X katika nyumba hizo ambazo nyingi zinamilikiwa na wachuuzi waliokopa benki, baadhi ya wafanyakazi wa serikali na waliojiunga katika Vyama vya Kuweka na Kukopa(Saccos), ni batili kwani haikufuata taratibu zote za kisheria.

Alisema na kumtaja Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo kuwa ndiye aliyeamuru uendeshaji huo kwa kuwa nyumba yake haina maji safi. Lema aliwataka wakazi wa Mirriet kutokuwa na wasiwasi wa kubomolewa nyumba zao kwani alama zilizowekwa hazitakubalika kwa kuwa kuna figisufigisu ndani yake.

Mbunge alisema na kuitaka AUWSA kukaa na kujitafakari kwani eneo lote la ekari 25 haliwezi kutolewa na kujengwa vyanzo vya maji bali kama inawezekana ni kufanya tathmini ya kina ndani ya siku 14 kuangalia eneo dogo tu katika eneo hilo, kukaa nao na kukubaliana na kuwalipa kwanza.

ZeroDegree.
Uwekaji alama X katika nyumba wazusha vilio Arusha. Uwekaji alama X katika nyumba wazusha vilio Arusha. Reviewed by Zero Degree on 7/31/2016 09:52:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.