Loading...

Vijana Chadema katika vita mpya na polisi.

Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi.

Wakati Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) likitangaza kuandaa mikutano ya hadhara kote nchini kwa siku moja, chama hicho kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu kitakachofanyika leo na kesho kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa nchini na njia za kuiimarisha kuanzia ngazi ya vitongoji.

Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi, akizungumza Dar es Salaam jana, wakati alipotoa maazimio kuhusu mwenendo wa siasa unavyoendelea nchini. Katikati ni Makamu Mwenyekiti Bavicha Bara, Patrick Sosopi na Makamu Mwenyekiti Bavicha Zanzibar, Zeuda mvano. Picha Omar Fungo 
 

Chadema imeitisha kikao hicho wakati kukiwa na taarifa kuwa wanachama waliojiunga na chama hicho wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita, wanatarajiwa kutangazwa kurejea CCM wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho tawala unaofanyika leo mjini Dodoma.

Miongoni mwa wanaotajwa kurejea CCM ni pamoja mwenyekiti wa zamani wa Mkoa wa Singida, Mgana Msindai, mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, mgombea uenyekiti wa Bavicha na ubunge wa majimbo ya kaskazini.

Makada kadhaa wa CCM waliamua kujiunga na upinzani baada ya jina la Edward Lowassa kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha urais ndani ya chama hicho tawala na kusababisha waziri huyo mkuu wa zamani kujiondoa na kujiunga na Chadema.

Walioamua kumfuata Lowassa ni pamoja na waziri mkuu mwingine wa zamani, Frederick Sumaye, mawaziri, wabunge, wenyeviti wa mikoa na madiwani, ambao CCM iliwapachika jina la “makapi”.

Hadi jana majina ya wanachama hao wa Chadema wanaohamia CCM yalikuwa hayajafahamika zaidi ya habari kuenea kuwa Msindai ni mmoja wao.

Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alithibitisha, lakini hakutaja majina akisema wamepokea maombi mengi, lakini kesho ndiyo watayataja.

“Msiwe na haraka, subirini. Ni kweli tumepokea maombi mengi, lakini kesho (leo) mtaujua ukweli,” alisema ole Sendeka.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema jana kuwa kikao hicho kitapokea taarifa na kujadili hali ya siasa nchini.

“Katika siku za hivi karibuni, taifa limekuwa likipitia katika majaribu makubwa, ikiwa ni pamoja na uvunjifu mkubwa wa sheria na taratibu za kuongoza nchi unaofanywa waziwazi na mamlaka za juu. Viongozi waandamizi wa nchi kupitia kauli na matendo mbalimbali kiasi cha kuwashtua Watanzania ambao wangependa kuona nchi yao ikiendeshwa katika misingi ya uwajibikaji wa kisheria na demokrasia,” alisema.

Alisema katika kikao hicho cha siku mbili, Kamati Kuu itapokea taarifa na kujadili kabla ya kufanya maamuzi kuhusu mipango inayoendelea ya kukipanga chama ili kiendelee kufanya shughuli zake kwa ufanisi.

“Hususan kinakwenda kuimarisha misingi kuanzia ngazi ya kitongoji nchi nzima, kupitia usimamizi wa kanda 10 za chama,” alisema.

Jijini Dar es Salaam, Bavicha inaonekana kuingia kwenye vita vingine na chombo hicho cha dola kutokana na uamuzi huo wa kuitisha mikutano ya hadhara kote nchini.

Mikutano hiyo ni kama imezuiwa na Rais John Magufuli ambaye Juni 24 aliwataka wanasiasa kusubiri hadi baada ya miaka mitano ndipo wafanye siasa za ushindani zaidi, akisema hangependa “kuona mtu yeyote akinichelewesha kutekeleza ahadi nilizotoa kwa wananchi”.

Juni 7, Jeshi la Polisi lilipiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa kwa kile ilichoeleza kuwa ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi hadi hali ya amani itakapoimarika nchini.

Hata hivyo, Julai 10, wakati CCM ikiendelea na maandalizi ya Mkutano Mkuu, Jeshi la Polisi lilisema zuio hilo halitahusu mikutano ya kiutendaji na kiutawala itakayofanywa kwa mujibu wa Katiba na kanuni za vyama hivyo.

Pia, likawaonya Bavicha dhidi ya uamuzi wao wa kwenda Dodoma kuzuia mkutano huo likisema limejiandaa vya kutosha.

Lakini Bavicha, ambayo awali ilipanga kufanya kikao chake cha Kamati ya Utendaji mjini Dodoma leo, jana iliibuka na vita nyingine.

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi aliwaambia waandishi wa habari kuwa kikao cha siku mbili cha baraza hilo kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kimeazimia kufanya mikutano ya siku moja nchi nzima.

Alisema Bavicha imeheshimu agizo la mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyewakataza kwenda Dodoma.

“Tunabadili uelekeo. Plan B yetu ni kwa wenyeviti wote wa Bavicha tunakwenda mikoani kufanya mikutano ya chama ya hadhara kwa siku moja. Jeshi la Polisi liheshimu sheria, lisiendeshwe kwa kauli ya mtu mmoja,” alisema Katambi bila ya kutaja mtoa kauli hiyo.

Katambi alisema tarehe ya mikutano hiyo itatangazwa baadaye.

Alisema katika mikutano hiyo wataeleza jinsi Rais Magufuli alivyokosea kufanya uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala wa wilaya.

“Nafasi za ukurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala ni za kitaaluma, lakini kuna watu wamepewa ni vilaza wengine tumesoma nao tunawajua. Vyeo vyenyewe vimetolewa kisiasa na upendeleo,” alisema Katambi na kuongeza:

“Serikali hii inaendeshwa kwa upendeleo wa kisiasa. Jeshi la Polisi linaruhusu mikutano ya siasa, lakini Chadema ikitaka kufanya inazuiwa.”

Alisema katika mikutano hiyo watadai Katiba mpya kwa kuwa iliyopo sasa haijatokana na matakwa ya Watanzania.

Alisema mikutano hiyo itafanyika kwa kufuata Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992.

Katika hatua nyingine, Katambi alisema katibu mkuu wa Bavicha, Julius Mwita juzi usiku alivamiwa na watu wasiojulikana maeneo ya Magomeni na kuporwa mali zake, ikiwamo kompyuta mpakato na simu yake ya mkononi.

“Jana (juzi) usiku wa saa saba baada ya kumaliza mkutano wetu na kila mtu kutawanyika, tulipata taarifa kuwa Katibu wetu amevamiwa na kujeruhiwa na kuporwa mali zake. Tunahisi kulikuwa na mkakati wa kupora nyaraka zetu, lakini tulishazihifadhi mahali salama,” alisema Katambi. Hata hivyo, alisema hawajaripoti tukio hilo polisi hadi watakapokamilisha uchunguzi wao ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo.

Source: Mwananchi
ZeroDegree.
Vijana Chadema katika vita mpya na polisi. Vijana Chadema katika vita mpya na polisi. Reviewed by Zero Degree on 7/23/2016 11:52:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.