Loading...

Viwanja Dodoma vyageuka lulu, Bei zake zapanda maradufu.

WAKATI wizara mbalimbali na taasisi za serikali zikijipanga kuhamia Dodoma kama Rais John Magufuli alivyoagiza, bei za viwanja imepanda maradufu ndani ya siku tano tangu kutolewa kwa agizo hilo.


Pia sekta binafsi nayo imesema imeanza mikakati ya kuhamia kwenye mji huo kwa kuwa inafanya shughuli zake kwa ukaribu na serikali.

Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wiki iliyopita, Rais Magufuli aliahidi serikali itahamia Dodoma ili kutekeleza mpango ulioasisiwa mwaka 1973 na muasisi wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wa kuufanya mji huo kuwa makao makuu ya nchi.

Hata hivyo, akihutubia kwenye siku ya kumbukumbu ya mashujaa, Jumatatu iliyopita mjini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim

Majaliwa, aliwekea mkazo agizo hilo kwa kuahidi kuhamia huko kabla ya Septemba, mwaka huu.

Kufuatia hali hiyo, wizara na taasisi mbalimbali za serikali nazo zimeanza mipango ya kuhamia huko.

BEI ZA VIWANJA DODOMA ZAPAA


Siku tano baada ya Rais Magufuli kutangaza azma ya kuhamishia makao makuu ya serikali Dodoma ndani ya miaka minne ya uongozi wake iliyosalia ya awamu yake ya kwanza, bei za viwanja vya makazi mjini humo imepanda mara dufu.

Mmoja wa wananchi hao, Abel John, amesema kwa sasa viwanja vimepanda bei tofauti na siku za nyuma kabla ya tangazo hilo la kuhamishia makao makuu kutolewa.

“Mfano eneo la Kisasa mjini hapa, viwanja vilikuwa vinauzwa kati ya Sh. milioni 10 hadi Sh. milioni15, lakini sasa hivi ukitafuta kwa madalali wanauza zaidi ya Sh. milioni 20,” alisema.

John alisema pia katika eneo la Nzunguni viwanja vilikuwa vinapatikana kwa Sh. milioni tatu hadi Sh. milioni tano, lakini kwa siku hizi chache vimekuwa shida kupatikana.

Alisema hali hiyo inatokana na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA ) kutokuwa wazi katika kuuza na watu wanapotafuta viwanja wanajibiwa hakuna lakini vinapatikana kwa madalali.

Naye mkazi mwingine wa mjini hapa, Mwanaisha Ali, alisema nyumba za kupanga zimepanda bei kutokana na wenye nyumba kuwa na uhakika wa kupata wapangaji wapya wakati wowote.

Aidha, alisema hata kodi ya vyumba vya kupanga kwa kipindi hiki itapanda bei kutokana na mahitaji makubwa ya wageni.

SEKTA BINAFSI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye, amesema taasisi hiyo imejiwekea lengo kuhamia Dodoma baada ya miaka mitano.

Simbeye alisema kuwa watahamia huko baada ya kukamilika jengo la makao yao makuu.

Alisema katika kutekeleza mpango huo, TPSF imetuma mtu kwenda Dodoma kutafuta eneo ambalo litajengwa jengo hilo.

Alisema TPSF hufanya kazi karibu sana na serikali, hivyo hatua ya kuhamia Dodoma itawalazimu na wao kuhamia huko.

Simbeye alishauri wafanyabiashara na kampuni nyingine zianze kuwekeza Dodoma kwa sababu miaka mitano ijayo utakuwa ni mji wa kibiashara kuliko Dar es Salaam.

WAFANYAKAZI

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholaus Mgaya, alisema wazo la serikali kuhamia Dodoma lilikuwapo tangu utawala wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema kila Rais aliyeingia madarakani baada ya Mwalimu Nyerere kung’atuka Tucta ilikuwa inamkumbusha wazo alilolitoa Mwalimu Nyerere la serikali kuhamia Dodoma.

“Hata Rais Magufuli wakati wa sherehe za Mei Mosi za mwaka huu tulimkumbusha, naye akatujibu mbona nyie hamhami, lakini alikuwa anatutania,” alisema Mgaya.

Mgaya alisema Tucta haina shida ya kuhamia Dodoma kwani ilishaanza maandalizi muda mrefu kwa kuwa wanamiliki hoteli eneo la Uhindini mkoani humo.

Alisema pia wana nyumba zipatazo 22, pamoja na kuwa na ofisi ya mkoa maeneo ya Makore na ofisi ndogondogo.
Mgaya alisema Tucta pia ina kiwanja kikubwa mjini Dodoma ambacho wanaweza kujenga ghorofa refu.

FEDHA ZA KUHAMA

Msemaji Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja, alisema mchakato wa serikali kuhamia mjini Dodoma umetolewa baada ya kupitishwa kwa bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2016/17, hivyo hakukuwa na fungu lolote la fedha lililotengwa katika shughuli hiyo.

Alisema lakini kutokutengewa fungu lolote hakuwezi kuzuia utekelezaji wa agizo la serikali la kutaka kuhamia mjini Dodoma.

Alisema katika bajeti ijayo ya mwaka 2017/18 kutatengwa fedha kwa ajili ya wizara na taasisi kuhamia mjini Dodoma.
Alipoulizwa kwa sasa serikali inapata wapi fedha za kuhamia Dodoma wakati hazikutengwa fedha zozote katika bejeti kuu, Mwaipaja alisema serikali ni kubwa hivyo ina vyanzo vingi vya kupata fedha na inajua wapi sehemu ya kupata fedha.

NYUMBA ZA NHC

Kuhusu hatima ya nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) zilizo Dar es Salaam ambapo asilimia kubwa ya wizara zimepanga, Meneja Uhusiano wa shirika hilo, Yahaya Charahani, alisema hawataathirika kwa kuwa kuna watu wengi wanaomba nafasi kwenye majengo hayo.

Charahani alisema mbali na Dar es Salaam, katika mji wa Dodoma pia shirika hilo lina nyumba ambazo wizara zinatumia.
Hata hivyo, kwa sasa alisema hawana jengo lililo wazi mkoani Dodoma la kupangishwa na wizara zitakazo hamia mkoani humo.

“Sababu kubwa ya sisi kutoathiriwa na hatua ya wizara kuhamia Dodoma ni kwa sababu kodi yetu ipo chini ya asilimia 85 ya bei ya soko, kwa hiyo tuna maombi mengi ya watu wanaotaka majengo,” alisema Charahani na kuongeza:

“Kwa hiyo hata kama wizara zikihama na kuachia majengo, sidhani kama kwa namna yoyote ile tutaathirika, watu wanaohitaji hayo majengo wako wengi sana.”

WIZARA KUHAMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, alisema kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala hilo na kwamba kuna mambo ambayo kwanza yanapaswa kufanyika kabla ya wao kwenda Dodoma.

Alisema kwa sasa wanasubiri mwongozo wa serikali juu ya utekelezaji wa suala hilo.

CDA YAZUNGUMZA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Pascas Muragili, alisema wizara zote zimeshawasilisha maombi ya kupatiwa viwanja na kwamba pia viwanja kwa ajili ya wananchi vipo kwa kila atakayehitaji.

Alisema kutokana na Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, walikwisha weka mipango mji vizuri kwa hiyo maeneo yote yameaanishwa kwa ajili ya matumizi mazuri ya ardhi.

Kuhusu kasi ya upimaji wa viwanja mkurugenzi huyo alisema kuwa mamlaka yake imejipanga na ina timu ya kutosha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

ZeroDegree.
Viwanja Dodoma vyageuka lulu, Bei zake zapanda maradufu. Viwanja Dodoma vyageuka lulu, Bei zake zapanda maradufu. Reviewed by Zero Degree on 7/28/2016 11:04:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.