Loading...

Aliyemuua Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi, amehukumiwa kwenda jela miaka 15.

Mjane wa Marehemu Daud Mwangosi, Itika Mwangosi, akisalia kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa jana baada hukumu ya miaka 15 jela ya Askari Polisi aliyemuua mume wake.

ASKARI wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Pacificus Simon, amehukumiwa miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua kwa risasi aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Chennel Ten, Daudi Mwangosi.

Simon alihukumiwa kifungo hicho na mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.

Akisoma hukumu hiyo jana, Jaji Dk. Paulo Kihwelo alisema katika kutoa adhabu hiyo, mahakama imezingatia mambo manne yakiwemo ya kisheria na ya kijamii pamoja na uzito wa kosa linalomkabili mshitakiwa.

Jaji Dk. Kihwelo alisema mahakama imeangalia mambo manne katika kutoa hukumu hiyo ambayo ni ukubwa wa kesi inayomkabili mtuhumiwa, mazingira ya kosa, maslahi ya familia na ya jamii kwa ujumla.

Alisema mahakama imetoa hukumu hiyo mara baada ya kusikiliza maombi yaliyotolewa juzi na upande wa Jamhuri ambao uliomba mahakama imtie hatiani kwa kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kutumia kifungu namba 195, huku upande wa utetezi ukiomba mahakama kufikiria shufaa tano ambazo zilitolewa mahakamani hapo pia kufikiria adhabu itakayompatia mtuhumiwa ikiwa ni pamoja na kumwachia huru kwa masharti maalumu.

Jaji Kihwelo alisema mahakama inajua itatenda haki endapo itamfunga jela miaka 15 kwa sababu mtuhumiwa ameshakaa miaka minne mahabusu, hivyo atakuwa amekutana na changamoto nyingi, ikiwamo kujutia kosa la kuua binadamu
Mahakama ilisikiliza upande wa utetezi kwamba mtuhumiwa anategemewa si jambo linalozingatiwa na mahakama kwenye makosa ya jinai.

Alisema mahakama inapotoa uamuzi, inaagalia upande wa sheria na si kuyumbishwa na maoni.

Kwa mujibu wa Jaji Dk. Kihwelo, adhabu haitolewi kama kulipiza kisasi bali inatoa kama onyo na kuzuia mambo kama hayo kujitokeza tena kwenye jamii.

“Mahakama inaelewa kwamba marehemu alikufa kifo ambacho si cha kawaida. Inatambua machungu ya familia lakini upande wa Jamhuri ulikiri kuwa mtuhumiwa hilo ni kosa lake la kwanza, hivyo mahakama inaona ni busara kumwadhibu kwa kuzingatia malengo ya adhabu kisheria,” alisema.

Hata hivyo, alisema mahakama haiafiki maombi ya upande wa utetezi kwamba imwachie mtuhumiwa kwa masharti maalum lakini adhabu itakayotolewa itaendana na kosa alilotenda.

“Kwa upande wangu kumwachia mtuhumiwa kwa masharti haitakwenda sawa na siamini kama haki itakuwa imetendeka. Kuua ni kosa kubwa sana na maelezo ya kuwa mtuhumiwa aliua bila kukusudia si sababu ya kumpunguzia adhabu ndiyo maana moja ya adhabu za kosa hilo ni kifungo cha maisha jela.

“Kila kesi inaendana na mazingira yake na adhabu itakayotolewa itaonyesha kutoa funzo kwa wengine kwa kuwa mshitakiwa alifanya kosa hilo kizembe,” alisema Jaji Dk. Kihwelo.

Upande wa Jamhuri, uliwakilishwa na mawakili Sunday Hyera, Ladislaus Komanya na Adolf Maganda wakati upande wa utetezi ukiwakilishwa na wakili Rwezaula Kaijage.

MJANE ANENA



Mjane wa marehemu Daudi Mwangosi Itika Mwangosi mwenye kilemba cheusi akifurahi jambo na ndugu zake.

Akizungumza nje ya mahakama, mjane wa marehemu, Itika Mwangosi, aliishukuru mahakama na waandishi, huku akisema: “Hata kama mtu amekutendea kosa kubwa lenye thamani, Mungu alitupa neno moja tu la asante.”

Itika aliwataka wanahabari wasiogope bali wasonge mbele na Mungu atawapigania katika kutetea haki za jamii.

Naye Deodatus Balile, Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema upande wa mashtaka ulitaka kesi hiyo iharibike kama si ungamo alilolitoa chini ya mlinzi wa amani. Alisema kinyume na hali hiyo, kesi hiyo ingekwishapotea.

Balile alisema kumuua mtu aliyeua hakumrejeshi aliyeuawa lakini kinachotakiwa ni fundisho na hata askari wajue hawako juu ya sheria na wajue wana wajibu binafsi.

Kwa mara ya kwanza, mtuhumiwa alifikishwa mahakamani Septemba 12, 2012 ambako hakutakiwa kujibu chochote hadi kesi ilipofikishwa kwenye mahakama kuu na ilisajiliwa kwa namba 45 ya mwaka 2013.

Mwangosi aliuawa Septemba 2, 2012 katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi akiwa anatekeleza majukumu yake ya kikazi wakati jeshi hilo likiwa kwenye operesheni ya kuzuia wanachama wa Chadema kufungua matawi yake.

Polisi waliwazua wanachama hao kwa madai kwamba kulikuwa na Sensa ya Watu na Makazi iliyokuwa ikiendelea.

Credits: IPPMedia
ZeroDegree.
Aliyemuua Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi, amehukumiwa kwenda jela miaka 15. Aliyemuua Mwandishi wa Habari Daudi Mwangosi, amehukumiwa kwenda jela miaka 15. Reviewed by Zero Degree on 7/28/2016 10:55:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.