Loading...

Wanafunzi 7,400 wafukuzwa rasmi chuo kikuu cha Dodoma [ UDOM ].

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Waziri amesema wanafunzi 7,423 kati ya 7,8050 waliokuwa wakichukua stashahada ya ualimu wa sekondari na msingi ya masomo ya Sayansi na Hisabati, wamebainika kutokawa na sifa za kuendelea na masomo hayo chuoni hapo.

Profesa Ndalichako alisema baada ya wanafunzi hao kusimamishwa kuendelea na masomo Mei 28 kutokana na mgomo uliokuwa ukiendelea chuoni hapo, uchunguzi ulifanywa na kubainika kwamba 382 pekee ndiyo wenye sifa za kuendelea na masomo yao kwenye chuo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Prof. Ndalichako alisema wanafunzi wengine 52 walikuwa wamepata daraja la nne na hivyo kukosa sifa za kusoma stashahada.

Wanafunzi wengine, Prof. Ndalichako alisema, serikali itawapangia vyuo vingine vya ualimu kuendelea na masomo mengine, lakini siyo kozi hiyo maalumu ambayo ililenga kupunguza uhaba wa walimu wa sayansi na hisabati.

Alisema wanafunzi 290 walibainika kukosa vigezo vingine ikiwa ni pamoja na kufeli masomo ya sayansi, hivyo wametakiwa kujiunga na taaluma nyingine kulingana na sifa walizonazo, Prof. Ndalichako alisema.

Waziri huyo pia alibainisha kuwa, sifa za wanafunzi waliotakiwa kusoma masomo hayo ni wale wenye ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu, na kwenye masomo ya sayansi na hisabati wawe wamefaulu kwa alama A mpaka angalau C.

“Kama mnakumbuka mwaka 2014 serikali ilianzisha mpango huo maalum wa kuwadahili wanafunzi wenye sifa za kusoma masomo ya Hisabati na Sayansi, kwa ajili ya kupunguza uhaba wa walimu wa masomo hayo katika Shule za Sekondari nchini," alisema Prof. Ndalichako.

"Lakini wakati wamerudishwa nyumbani, tulibaini kuwa wengine hawakuwa na sifa stahiki za kuendelea na mafunzo hayo.”

Alisema wanafunzi wengine 7,081 waliokidhi vigezo kwa kuwa na ufaulu wa ngazi ya kwanza hadi ya tatu, watapangiwa katika vyuo vingine vya ualimu vya srikali na watalipwa ada.

Alisema katika wanafunzi hao, 4,586 walikuwa wa mwaka wa kwanza na sasa watapelekwa katika vyuo vya Morogoro, Butiama, Mpwapwa, Songea na Tukuyu.

Alisema wengine 1,337 wa mwaka wa pili watahamishiwa katika vyuo vya ualimu vya Korogwe na Kasulu ili kumalizia masomo yao.

ELIMU YA MSINGI


Pof. Nalichako alisema kwa upande wa mpango wa walimu wa elimu ya mingi, wanafunzi waliokuwa wanachukua kozi hiyo, vigezo vilikuwa ni wawe wamemaliza ngazi ya cheti na kufanya kazi zaidi ya miaka miwili.

Lakini hata katika fungu hilo, Waziri alisema, ilibainika kuwa mpango huo haukuwa unaendana na ule wa walimu wa Sekondari na kwamba wamewahamisha wanafunzi 29 kwenda kumalizia masomo yao katika Chuo Ualimu Kasulu kwa gharama zao.

“Hawa hawakuwa kwenye huu mpango na hauendani hivyo kwa sababu hawahususiki, tumewahamishia Chuo cha Ualimu Kasulu na watajilipia ada wenyewe.

"Lakini pia watatakiwa kurejesha mikopo ya fedha walizokuwa wameanza kusomeshewa.”

Alisema kundi lingine la wanafunzi 1,181 waliokuwa wamedahiliwa kusoma masomo hayo, wametakiwa kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo mahali popote.

Prof. Ndalichako alisema Serikali itaendelea kuwapa mikopo wanafunzi waliorejeshwa UDOM na wale watakaohamishiwa vyuo vingine watalipiwa ada ya Sh. 600,000 kwa mwaka ambayo inalipwa moja kwa moja chuoni.

Alisema kwa wale 382 waliorudishwa UDOM, watatakiwa kuripoti chuoni Oktoba na kwa vyuo vya ualimu watatakiwa kuripoti katika vyuo walivyopangiwa Septemba.

VYETI VYAO HALISI


Prof. Ndalichako alisema wanafunzi wote watakaoripoti vyuoni watatakiwa kuwa na vyeti vyao halisi vya kidato cha nne ili kuhakikiwa.

Alisema lengo ni kuhakiki uhalali wa wanafunzi walioomba kujiunga na chuo ili kuondoa udanganyifu uliojitokeza.

Pia alisema hatua stahiki zitachukuliwa kwa waliohusika kuwadahili wanafunzi hao wasio na vigezo.

Pia alisema kuondolewa kwa wanafunzi katika chuo hicho, hakuwezi kuathiri mpango huo wa elimu na kwamba wanafunzi wanaokwenda vyuo vingine hawakuwa na sifa za moja kwa moja za kuendelea kusoma katika vyuo 10 vya Serikali vinavyotoa mafunzo ya Sayansi.

Alisema vyuo vilivyopo vina uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 5,000 lakini hadi sasa waliodahiliwa ni 2,939 hivyo bado kuna upungufu.

“Huu mpango ulikuwa maalum na hata hivyo hautaendelea kwa wale tulioona wana sifa za kusoma masomo hayo tumewahamishia katika vyuo vyetu vya Serikali ambavyo vina uwezo wa kuwafundisha na kupunguza msongamano katika Chuo cha UDOM,” alisema.


ZeroDegree.
Wanafunzi 7,400 wafukuzwa rasmi chuo kikuu cha Dodoma [ UDOM ]. Wanafunzi 7,400 wafukuzwa rasmi chuo kikuu cha Dodoma [ UDOM ]. Reviewed by Zero Degree on 7/20/2016 10:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.