Loading...

Wiki ya CCM iliyotikisa Dodoma.

MISURURU mirefu ya magari, baadhi ya watu kukesha kwenye majumba ya starehe na wengine kulazimika kulala kwenye magari, mzazi na mwanaye mdogo kusafiri kwa siku tatu kuuwahi mkutano na mji kupambwa kwa bendera za kijani, ni baadhi ya mambo yaliyoshuhudiwa hapa kwa karibu wiki nzima iliyopita.

Na si hayo tu. Taarifa zinasema kwa karibu wiki nzima baadhi ya taasisi zililazimika kuhamishia mikutano kwenye Mikoa ya jirani baada ya kukosa kumbi na mahali pa kufikia.

Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) , Christopher ole Sendeka, anasema CCM ilikodi hoteli pamoja na nyumba za kulala 306 zenye vyumba 3,331 kwa ajili ya wageni na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa chama chake.

Si kawaida kwa Dodoma kushuhudia magari mengi barabarani lakini kwa wiki nzima iliyopita hiyo ndiyo iliyokuwa hali ya mji huu ikiwafanya wakazi wake kuanza kuonja adha ya foleni, kama matamshi ya Rais Dk. John Magufuli ya kuhamia hapa kabla ya kipindi chake cha kwanza kwisha 2020, na lile la Jumatatu wiki hii, la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuhamia ifikapo Septemba Mosi mwaka huu yatatimia.

Msongamano huo wa magari uliwapa kazi ya ziada askari wa usalama barabarani kuongoza magari huku wakihakikisha kuwa ajali hazitokei kutokana na watu kuwa na haraka ya kuingia na kutoka kwenye ukumbi wa mkutano.

Lakini pengine kivutio kingine katika mkutano huo ni cha Mohamed Salum aliyesafiri kwa baiskeli kutoka mkoani Singida akiwa na mtoto wake, Yusuf (2) ili wamuunge mkono Magufuli katika kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Huku Salum na Yusuf wakiwa wamezungukwa na kundi la watu nje ya ukumbi, Salum anasimulia kwamba walisafiri kwa muda wa siku tatu kutoka Singida hadi hapa kumshuhudia Dk. Magufuli akikamata uenyekiti, lakini pia kumuandaa Yusuf kuwa rais wa Tanzania mwaka 2050.

“Imetuchukua siku tatu kufika hapa. Ya kwanza tulilala Manyoni. Siku ya pili tulilala Bahi, na siku ya tatu tuliingia Dodoma na leo (Jumamosi iliyopita) tumekuja kwenye mkutano, tupo hapa nje,” alisema Salum.

Na kama kawaida ya mikutano kama hii, wajasiriamali nao walikuwa na wakati mzuri wa kufanya biashara, hasa za sare za CCM katika kila kona ya mji kuufanya mji kuonekana wa kijani zaidi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana awali alikuwa amehamssha wajasiriamali wanaotoa huduma za usafiri, malazi na vyakula na zote za biashara wazitoe katika viwango bora zaidi na kwa ufanisi zaidi kwani ni njia ya kujiongezea kipato.

“Dodoma inapopata ugeni mkubwa namna hii maana yake ni neema kwetu. Mzunguko wa fedha unakuwa mzuri zaidi kwa hiyo tuendelee kuboresha huduma zetu ili wageni waone Dodoma inastahili kwa ajili ya shughuli zao,” alisema.

Huku akiwatia shime wajasiriamali, Rugimbana alitoa tahadhari kwa makundi yenye kusaka shari akisema Dodoma si mahali salama kwa wapenda vurugu na hakika kwa wiki nzima mji ulikuwa shwari katika kipindi chote cha Mkutano hadi wajumbe walipotawanyika.

“Hizi ni zama na nyakati nyingine, kila mtu aheshimu sheria na utaratibu na kuheshimiana katika imani zetu, itikadi zetu na majukumu tunayoyafanya,” alisema Rugimbana.

Kwa ujumla, kuthibitishwa kwa Rais John Magufuli kuwa Mwenyekiti kwa kura za kishindo kulianza kuonekana tangu Julai 21, baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kupendekeza jina lake na kulipelekea katika kikao cha Halmashauri Kuu ili liweze kuthibitishwa na kisha kupelekwa katika Mkutano Mkuu Maalumu.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde anasema CCM kimezaliwa upya baada ya kupata Mwenyekiti mwenye uwezo mkubwa wa kukibadilisha chama na kukifanya kitawale tena zaidi ya miaka 20 kutokana na kuweza kuzimudu changamoto zilizopo ndani ya CCM na hivyo kuwa na matarajio chanya.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa na Raia Mwema wamesema CCM imeonyesha ukomavu mkubwa kwa kumpitisha Magufuli na hivyo kufuta uvumi kwamba hawamtaki kwa kuhofia utendaji wake wa kutumbua majipu kwa wasiofuata maadili. Hali imekuwa tofauti na CCM imefungua ukurasa mpya.

Credits: Raia Mwema
ZeroDegree.
Wiki ya CCM iliyotikisa Dodoma. Wiki ya CCM iliyotikisa Dodoma. Reviewed by Zero Degree on 7/28/2016 10:00:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.