Loading...

Hii hapa sababu ya kupungua kwa idadi ya samaki katika Ziwa Tanganyika.

Watu waliongezeka eneo hilo miaka ya 1990 kutokana na ongezeko la wakimbizi

Utafiti mpya umebaini kupungua pakubwa kwa idadi ya samaki katika Ziwa Tanganyika, mojawapo ya maziwa muhimu zaidi kwa uvuvi duniani, kumetokana na ongezeko la joto duniani katika karne moja iliyopita.


Ziwa Tanganyika ndilo la kale zaidi Afrika na samaki wake huwa muhimu sana kwa lishe katika mataifa yanayopakana na ziwa hilo.

Lakini idadi ya samaki imepungua sana, huku wavuvi wakiendelea kuongezeka.

Ongezeko hili la wavuvi lilidhaniwa kuwa chanzo kikubwa cha kupungua kwa idadi ya samaki.

Lakini utafiti mpya unaonesha chanzo hasa ni ongezeko la joto duniani kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ziwa Tanyanyika ndilo la pili kwa ukubwa duniani miongoni mwa maziwa yenye maji yasiyo na chumvi na maji yake huwa katika mataifa manne: Burundi, Jamhuri ya KIdemokrasia ya Congo, Tanzania na Zambia.

Samaki kutoka kwa ziwa hilo hutoa asilimia 60 ya protini zitokanazo na wanyama ambazo huliwa na watu eneo hilo.

Aidha, ni eneo lenye aina nyingi ya wanyama na mimea.


Samaki kutoka Ziwa Tanganyika hutegemewa sana na wakazi

Ili kufahamu mabadiliko yanayotokea katika ziwa hilo, watafiti wamechukua sampuli za mchanga kutoka kwenye kina cha ziwa hilo.

Baada ya kufanya utathmini wa mchanga huo na visukuku, wamepata viashiria kwamba idadi ya samaki imekuwa ikishuka sambamba na ongezeko la joto duniani.

Wanasayansi wanasema katika maziwa yanayopatikana maeneo yenye joto karibu na ikweta, ongezeko la joto katika maji hupunguza kuchanganyikana kwa maji kutoka sehemu ya juu ya ziwa ambayo huwa na oksijeni pamoja na maji yenye virutubisho vingi sehemu ya chini kwenye ziwa.

Kutochanganyikana vyema kwa maji haya husababisha virutubisho vinavyofika juu kwenye ziwa kupungua, hili hupunguza ukuaji wa miani (mimea ya rangi ya kijani, kahawia au nyekundu inayoota chini ya bahari) na hili hupelekea kupungua kwa lishe ya samaki.

Watafiti waliohusika katika utafiti huo wanasema ongezeko la joto limepunguza kuchanganyikana kwa maji, kupungua kwa ukuaji wa miani pamoja na kupungua kwa maeneo ambayo viumbe waishio chini ya bahari wanaweza kuishi na kustawi.

"Wazo letu lilikuwa kuchunguza visukuku na kubaini kushuka kwa idadi ya samaki kulianza wakati gani," anasema Prof Andrew Cohen kutoka Chuo Kikuu cha Arizona.

"Iwapo hili lilifanyika kabla ya kuanza kwa uvuvi wa kiviwanda miaka ya 1950, basi ungekuwa na ushahidi mkubwa kwamba hili halitokani na ongezeko la uvuvi na hivi ndivyo tulivyobaini."

Wanasayansi hao hata hivyo hawajapuuzilia mbali athari za ongezeko la uvuvi katika miongo sita iliyopita.

Wanasema kumekuwa an ongezeko la watu tangu miaka ya 1990, hasa kutokana na wakimbizi waliotoroka mizozo na kuhamia maeneo yaliyo karibu na ziwa hilo.

Wavuvi hutumia taa kuwavutia dagaa, ambao ndio sana huvuliwa kutoka kwenye ziwa hilo

"Ukizingatia mtindo wa sasa wa kuendelea kugawika zaidi kwa maji kwenye ziwa, idadi ya samaki itaendelea kupungua. Watu wanaosimamia sera wanafaa kuanza kufikiria kuhusu chanzo mbadala cha mapato na lishe kwa watu wanaoishi eneo hilo."

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la kisayansi la Proceedings of the National Academy of Sciences.

Credits: BBC Swahili
ZeroDegree.
Hii hapa sababu ya kupungua kwa idadi ya samaki katika Ziwa Tanganyika. Hii hapa sababu ya kupungua kwa idadi ya samaki katika Ziwa Tanganyika. Reviewed by Zero Degree on 8/10/2016 09:13:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.