Loading...

Lowassa ampongeza Rais Magufuli kwa utendaji kazi.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa amempongeza Rais John Magufuli kwa utendaji wake tangu ashike nafasi ya urais Novemba mwaka jana.


Hata hivyo, Waziri Mkuu huyo wa zamani amebainisha kuwa ingekuwa ni yeye amepata nafasi ya urais, angeanza na vipaumbele vyake ambavyo ni ajira na maslahi ya walimu ili kuboresha zaidi maeneo hayo.

Lowassa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akihojiwa na mtangazaji Tido Mhando kwenye kipindi cha Funguka, kinachorushwa na Televisheni ya Azam.

Alikiri kuwa Dk Magufuli hadi sasa ameonekana kufanya vizuri katika utendaji wake, ikiwemo suala la ufisadi na hatua yake ya kutekeleza kwa vitendo kuhamishia serikali mkoani Dodoma.

“Amefanya kazi nzuri katika maeneo fulani, amefanya vizuri sana. Kuna maeneo amesema mwalimu unaweza kufagia shilingi, na yeye amefagia shilingi. Ila kuuna maeneo kwa maoni yangu ningeyapa kipaumbele zaidi kwa mfano ajira,” alisisitiza.

Alisema suala la ajira bado Serikali ya Awamu ya Tano, haijalipa msukumo wa kutosha kwani Watanzania wengi bado wanataabika na ukosefu wa ajira.

“Hawa mama ntilie, bodaboda na wahitimu wengi wa vyuo vikuu hatuwatazami,” alisema Lowassa aliyeshindwa na Dk Magufuli katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Alisema hata katika kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea nchini Marekani, Rais Barack Obama wakati akihutubia wananchi, alibainisha wazi kuwa kipindi chake cha uongozi amefanikiwa kutengeneza ajira zaidi ya milioni 1.5.

Katika elimu, waziri mkuu huyo wa zamani pamoja na kupongeza hatua ya Magufuli ya kuanzisha operesheni madawati, lakini alibainisha wazi kipaumbele chake kingekuwa katika kuboresha zaidi madarasa na maslahi ya walimu.

Alisema anajivunia kuwa sehemu ya uanzishwaji wa shule za kata nchini, ambazo kwa sasa pamoja na kuanza na changamoto, lakini zimeanza kufanya vizuri na baadhi yake zimeshika nafasi za juu katika mitihani ya kidato cha nne.

Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Tano katika bajeti yake ya kwanza ya 2016/17 imekuwa na mpango kabambe wa mapinduzi ya viwanda kwa kuhakikisha idadi ya viwanda inaongezeka nchini, ikiwemo kufufua viwanda vyote vilivyokufa, lengo likiwa ni kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, lakini pia kuongeza ajira. 

Aidha, katika suala la maslahi ya walimu, tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alibainisha kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha inawawekea mazingira mazuri walimu ikiwemo kuongezea mishahara pamoja na vitendea kazi vya kufundishia. 

Hivi karibuni, Rais Magufuli alitangaza wazi kuwa baada ya kupata mafanikio katika operesheni ya utengenezaji wa madawati nchi nzima, wadau wa maendeleo watumie nguvu na kasi waliyoanza katika madawati, kujenga madarasa ili kupunguza tatizo la upungufu wa madarasa. 

“Nimeanza na madawati kwa kuwa naamini ni muhimu kwa mwanafunzi kwani, mwanafunzi anaweza kuendelea kusoma akiwa na dawati na ubao hata chini ya mti kuliko kukaa chini. Haya si mazingira mazuri ya kusomea,” alisema Magufuli. 

Kuhusu serikali kuhamia Dodoma, Lowassa alisema suala hilo kila rais wa Tanzania aliyepita akianzia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, William Mkapa na Jakaya Kikwete, alikuwa na dhamira ya kulitekeleza.

 “Nashukuru na ninampongeza Dk Magufuli yeye ameamua kulitekeleza kwa vitendo, ila natahadharisha wasilichukulie kwa kasi hiyo wanayokwenda nayo. Kuhamia Dodoma ni jambo zuri, kwani mji ule ni mzuri kwa kweli, lakini twendeni taratibu tu haina haja ya kwenda na kasi hii ya sasa,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais katika mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka jana, alisema bado anaamini hakutendewa haki, kwa kuwa mambo mengi aliyokuwa akituhumiwa ukiwemo ufisadi hayajathibitishwa. 

“Kwa kweli nimechoka sasa kila siku ni jambo hilo, mbona hakuna anayethibitisha. Mimi waliniondoa nashukuru, nilienda Chadema ambako sikujipeleka, bali niliombwa na Kamati Kuu na kupewa kabisa nafasi ya kuwania urais,” alisema Lowassa ambaye Februari 2008, alijiuzulu uwaziri mkuu kutokana na kashfa ya Richmond ambayo katika mahojiano ya jana, alikataa kuizungumzia akisema siyo ajenda tena.

Alikanusha madai kuwa kuhamia kwake Ukawa kupitia Chadema na kuwa mgombea urais, ndio chanzo cha ugomvi ndani ya umoja huo, kiasi cha baadhi ya vigogo wa upinzani kujitoa akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilibrod Slaa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba. 

Alisema anaamini kuwa kwenye vyama vya siasa kuna watu kazi yao ni kuvuruga huku akisisitiza kuwa huo ni utaratibu wa kawaida ambao mtu yeyote akitaka kuvuruga maendeleo anaanza na kuvuruga vyama vya siasa. 

Alisema kuhamia kwake Chadema kwa upande wake anaona kama amechelewa kwani amekuwa akilaumiwa kuwa endapo angetangaza mapema, huenda angehamia kwenye chama hicho na wafuasi wengi zaidi wa CCM. 

Wakati Lowassa akisema hayo, juzi katika Mkutano Mkuu wa CCM wakati Kikwete akimkabidhi madaraka ya uenyekiti wa chama hicho kwa Dk Magufuli, baadhi ya wanachama maarufu waliohamia upinzani wakati wa uchaguzi kwa madai ya kumfuata Lowassa, walirejea na kuomba msamaha. 

Baadhi ya waliorejea CCM wakati waliondoka chama hicho kwa kishindo kipindi cha uchaguzi ni Mgana Msindai, Fred Mpendazoe na Said Mkumba. Mwingine ni Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu aliyerejea CCM mwezi Machi mwaka huu, ambapo alikaririwa akisema “ Yaliyopita si ndwele tugange yajayo”. 

Halikadhalika katika mahojiano hayo ambayo Lowassa alikuwa akijibu kifupi, alisema anaunga mkono hatua ya chama chake Chadema kuendesha operesheni Ukuta, ingawa alishauri kuwa njia ya mazungumzo ingetumika zaidi kumaliza mzozo uliopo wa kisiasa.

“Naona maandamano hayana tatizo. Kinachozungumzwa pale yafanyike mazungumzo kuhusu kinachoendelea, haiwezekani watu wafunge midomo mpaka 2020 wakati chama tawala kinaendelea na masuala ya kisasa kama kawaida,” alisema. 

Pamoja na hayo, Lowassa alibainisha kuwa bado Zanzibar kuna tatizo na kumtaka Rais Magufuli aingilie kati, kwa kuwa baadhi ya vyama kikiwemo CUF vilisusa na kutoshiriki kabisa uchaguzi. 

Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu alipozungumzia suala hilo, alibainisha wazi hakuna chama chochote kilizozuiwa kuendelea na shughuli za siasa, kinachotakiwa ni kufuata taratibu kwa mujibu wa sheria, lakini endapo itaonekana shughuli zake zina mrengo wa uvunjifu wa amani, hakitaruhusiwa.

Aidha, Dk Magufuli juzi akiwa Singida alipiga marufuku operesheni hiyo kufanyika kwa kuwa tayari Jeshi la Polisi limebaini kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani na kusisitiza mtu yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua.

Pia Rais huyo alifafanua kuwa wanasiasa wanaruhusiwa kufanya shughuli zao katika majimbo yao na si kwenda kwenye maeneo ya wenzao na kufanya uchochezi huku akisisitiza kuwa wakati wa siasa umepita na sasa kazi ni moja kujenga nchi. 

Lowassa aliweka wazi kuwa anatarajia kuingia tena kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais ifikapo 2020 na anaamini safari hii atashinda endapo haki itatendeka.

Source: Habari Leo
ZeroDegree.
Lowassa ampongeza Rais Magufuli kwa utendaji kazi. Lowassa ampongeza Rais Magufuli kwa utendaji kazi. Reviewed by Zero Degree on 8/01/2016 08:15:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.