Loading...

Majaliwa azuia mikataba serikalini

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary, wakikagua mtama uliopandwa kwenye eneo la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika maonyesho ya wakulima Nanenane mjini Morogoro jana.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amepiga marufuku halmashauri kutoa ajira za mikataba na kuziagiza kufanya mapitio ya watumishi wa aina hiyo.

Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Morogoro mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.

“Tumeruhusu kuajiri kwa mikataba walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha miaka miwili tena kwa waliostaafu. Kuna kada zilizoko katika muundo wa ajira, hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba wakiwamo madereva. Msiwatumikishe kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema.

Akizungumzia suala la watumishi hewa mkoani Morogoro, Waziri Mkuu alitaka mkoa huo kuendelea kufanya uchunguzi na ifikapo mwisho wa mwezi huu uwe umekamilisha taarifa na kuanza kuchukua hatua kwa waliohusika.

Aidha, Waziri Mkuu alionya serikali haitasita kuwaondoa katika nyadhifa zao wakurugenzi watakaotoa taarifa za uongo kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

“Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo lakini kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakiandika taarifa za uongo imekamilika wakati haijajengwa," alisema. "Hivyo wakurugenzi watakaoshiriki kutoa taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa.”

Alitoa wito kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kutembelea miradi inayojengwa katika maeneo yao ili kujiridhisha kama thamani yake inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe alisema mkoa huo unaendelea kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuzitaka taasisi zote za serikali kufanya uhakiki wa watumishi hewa na malipo batili ya watumishi.

Alisema mkoa huo umebaini watumishi hewa 315 ambao wameisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 2.132 na kwamba timu ya uhakiki bado inaendelea na kazi hiyo na taarifa kamili itatolewa baada ya kazi hiyo kukamilika.

Source: Nipashe
ZeroDegree.
Majaliwa azuia mikataba serikalini Majaliwa azuia mikataba serikalini Reviewed by Zero Degree on 8/02/2016 10:16:00 AM Rating: 5

Powered by Blogger.